Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein Awatakia Waislam Mwezi Mwema wa Ramadhani Kesho.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                                                             26.05.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wafanyabiashara kuwa waadilifu katika kufanya biashara zao katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwani imekuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi yao kupandisha bei za bidhaa kila ifikapo mwezi huu.

Alhaj Dk. Shein, aliyasema hayo katika risala maalum aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwa ajili ya kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu wa 1438 Hijria sawa na mwaka 2017 Miladiya.

Katika risala yake hiyo, Alhaj Dk. Shein amesema kuwa imekuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei za bidhaa kila unapofika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani jambo ambalo huleta usumbufu mkubwa kwa wafungaji na wananchi wote kwa jumla.

Hivyo, aliwasihi wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wanaouza bidhaa zao rejareja na jumla wazingatie wito wake huo na nasaha anazozitoa kwa kuwahurumia wananchi wenzao kwa kuwauzia bidhaa kwa bei za kawaida, zilizo nafuu kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanazishukuru neema za Mwenyezi Mungu na Mola wao atawaongezea Baraka.

Alhaj Dk. Shein, alisema kuwa ni wajibu kujiandaa na kuukaribisha mwezi wa Ramadhani kwa matumaini na matarajio ya kunufaika na fadhila zake hivyo, ni vyema juhudi zikaongezwa katika kutoa sadaka kwa kuwapa wale wanaostahili na wanaohitaji sadaka hizo pamoja na kuwasaidia wenye uwezo mdogo kutafuta futari na daku katika mwezi huu mtukufu.

Aidha, alieleza kuwa ibada ya funga kwa kawaida ina mafundisho mengi ikiwa ni pamoja na kuitaka jamii kuishi pamoja, kuheshimiana na kusaidiana, kustahilimiliana na kuvumiliana, kuwa na subira pamoja na kuwa na uwezo wa kudhibiti matamanio ya nafsi.

Akieleza athari za mvua za masika, Alhaj Dk. Shein alitoa pongezi kwa wananchi wote wkwa imani, mapenzi na huruma walizoonesha kwa kuwa pamoja na wale wote walaioathirika, kwa kuwapa misaada na kuwapongeza wafanyabiashara na viongozi mbali mbali kwa kushirikiana na Serikiali katika kuwapa ndugu zao hao misaada muhimu.


Hata hivyo, aliwaahidi wananchi kuwa Serikali itahakikisha michango na misaada inayotolewa na wananchi, viongozi pamoja na wafanyabiashara kwa ajili ya wananchi walioathirika na maafa, inawafikia wanaostahiki na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaokwenda kinyume na taratibu zilizopangwa za kufikisha na kuigawa misaaada hiyo.

Alhaj Dk. Shein, pia, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujiepusha kujenga katika sehemu za mabondeni pamoja na maeneo ya njia muhimu za maji huku akiwataka wananchi kushirikiana na Serikali yao katika kuvitunza na kuvilinda vianzio vya maji vilivyopo.

Pamoja na hayo, aliwahimiza wananchi pamoja na viongozi wa Manispaa na Halmashauri kuongeza juhudi katika kudumisha na kusimamia usafi ili kuepuka miripuko ya maradhi mbali mbali, hasa ya matumbo katika kipindi hiki cha mvua.

Alisisitiza kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kwani ana taarifa kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wameshaanza kuipuuza miongozo wanayopewa na wataalamu pamoja na sheria za usafi zilizopo kwani ni vyema ikumbukwe kuwa mitihani ya maradhi ikitokea watu wa mwanzo ambao kipato chao huathirika ni wafanyabiashara.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imekuwa ikiimarisha mipango na mikakati iliyokuwepo ya kujikinga na kukabiliana na maafa pamoja na kufanya marekebisho ya sheria iliyokuwepo na kuziimarisha taasisi husika.

Kwa mujibu wa maelezo ya Alhaj Dk. Shein, hivi Serikali inaadaa mpango wa kuliondoa tatizo la mafuriko katika eneo la Mwanakwerekwe na sehemu nyengine kupitia Awamu ya Pili ya Mradi wa ZUSP sambamba na kujenga barabara imara katika barabara ya Kibonde Mzungu ili iweze kupitika bila ya shida katika misimu yote.

Alhaj Dk. Shein, alitoa shukurani zake kwa wananchi wote kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudumisha umoja na mshikamano uliopo na kuwataka kuendeleza utamaduni wao wa kuishi kwa pamoja bila ya kubaguana kwa dini ama kabila.

Aliongeza kuwa mashirikiano ya pamoja yamewezesha kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi ambapo katika mwaka uliopita, uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.5 na mfumko wa bei ulibaki katika tarakimu moja, asilimia 5.7 sambamba na kupiga hatua katika ukusanyaji wa mapato.

Pia, Alhaj Dk. Shein, aliikumbusha Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira iendeleze utaratibu kwa kusambaza maji katika Mwezi huu mtukufu wa Radhamani, katika maeneo mabli mbali ambayo huduma za maji safi salama huwa zina upungufu na kuwataka wananchi kushirikiana na na wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), ili kazi ya kusambaza maji ifanyike vizuri.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.