Habari za Punde

Salamu za Rambirambi

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz

Mei 8,2017

SALAMU ZA RAMBIRAMBI

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imepokea kwa majonzi makubwa taarifa ya vifo vya ghafla vya Wanafunzi 32, Walimu wawili (2) wa Shule ya Lucky Vincent pamoja na dereva vilivyotokea Mei 6, 2017 asubuhi baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo la Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaungana na Watanzania wote kuomboleza vifo hivyo vya ghafla vya wapendwa wetu hawa. Huu ni msiba mzito siyo tu kwa shule, wazazi na wanafamilia bali kwa taifa zima.

Vifo hivyo vimekatisha haki ya uhai ya marehemu wote na pia imekatisha haki ya elimu ya wanafunzi hao.

Tunatoa pole kwa wafiwa wote – wazazi, wanafunzi, waalimu, uongozi wa Shule ya Lucky Vincent na Watanzania Wote. Mungu awatie nguvu,  awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Ni wazi kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliotarajiwa kuwa wajenzi wa taifa wa siku zijazo; lakini lililo muhimu kwa sasa ni kuwaombea marehemu wote pumziko jema.  Aidha Tume inawaombea majeruhi uponaji wa haraka.

Tume inaipongeza Serikali kwa jinsi ilivyojitoa katika kusimamia taratibu zote za kufanikisha mazishi ya marehemu hao.Tume inaiomba Serikali kupitia vyombo vyake wafanye uchunguzi wa kina wa ajali hiyo, na  matokeo yake yatumike kuepusha ajali nyingine zinazoweza kutokea.

Mwenyezi Mungu aziweke Roho za Marehemu wote mahali pema peponi, Amina.

Imetolewa na:                             SIGNED
 Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Mei 8, 2017


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.