Habari za Punde

Wakulima 2,934 wapewa bure miche 90,000 ya mikarafuu Pemba


NA HAJI NASSOR, PEMBA

JUMLA ya wakulima 2,934 wa zao la karafuu kisiwani Pemba, sambamba na taasisi sita zikiwemo za serikali na za watu binafsi, zimeshakabidhiwa miche bure zaidi ya 90, 000 ya mikarafuu kutoka Kitengo cha Mashamba ya Misitu na Vitalu Pemba, ili kuiotesha kwenye maeneo yao.

Awali kitengo hicho katika mwaka huu wa 2016/2017, kilipanga kugawa miche hiyo 89,524, kutoka kwenye vitalu vikuu sita vilivyopo kisiwani Pemba, ingawa lengo hilo limevuukwa.

Taarifa zinaeleza kuwa, wilaya ambayo wakulima wamejitokeza kwa wingi ni Chakechake kwa kufikia 1,390 ambapo waligawiwa miche 29,806, ambapo awali waliomba miche 26,408 na kuvuuka lengo lao.
Wilaya nyengine ambayo wakulima waliojitokeza kwa wingi ni Mkoani 723, sawa na idadi ya miche 20,400, ingawa awali waliomba miche 24,570 na kuwa na upungufu wa miche 4170.

Wilaya ya Wete wakulima 533, wakigawiwa miche 19,146 na Micheweni mkoa wa kaskazini kisiwani Pemba, ni wakulima 288 ambao walibahatika kugawiwa miche 9,369 ingawa waliomba miche 10,728.

Akizungumza kwa njia ya simu, mkuu wa kitengo hicho kisiwani humo, Hamad Omar Said, alisema kabla ya kuigawa miche hiyo, huwataka mabwana shamba wa wilaya husika, kuyangua mashamba ya wakulima husika.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuepusha mkulima kupewa miche mfano 200, wakati shamba lake kitaalamu linahitaji miche 150 au zaidi ya alioomba.

“Jengine tunalilofanya kabla ya kuigawa miche hiyo, wakulima lazima wapitie kwa masheha ili wajaze fomu maalum, ambayo ndio sisi inayotuongoza kwenye maombi’’,alifafanua.

Aidha Mkuu huyo wa Kitengo alisema ingawa wapo baadhi ya wananchi, huomba baada ya kufunga maombi yao ya awali, na hujitokeza wakati wa ugawaji na ndio maana kuna ongezeko la miche.

Hata hivyo alisema Shirika la Taifa la Biashara la ZSCT likiwa ndio mdau mkuu aliomba miche 2,000 ingawa lilikabidhiwa miche 1,000, samba mba na Jumuia za kiraia na zile za serikali zilioomba miche 1,100 na kubahatika miche 1,230.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa Kitengo, alisema hata zoezi la upandaji miti kitaifa, ulitengea miche 400 huku mashamba wa serikali likiwemo la Makuwe, lilitengewa miche 1500 ya mikarafuu, ikiwa ni hatua ya kuyaimarisha.

Mmoja kati ya wananchi wa Wambaa waliokabidhiwa miche hiyo Amina Haji Makame, alisema pamoja na utoaji huo bure wa miche, ni vyema wakapewa na elimu.

“Elimu ya kuitunza na kuiendeleza ni jambo jema, maana inawezekana wapo tunaoichukua tu, kwa sababu inatolewa bure sasa lazima na elimu ya kuitunza tupewe”,alishauri

Nae Khadija Hassnuu Mshamba wa Mizingani, aliipongeza serikali kwa kuendelea na utaratibu huo kwa zaidi ya miaka mitano sasa, jambo ambalo, ni njia moja ya kuliimarisha zao hilo.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wamesema, utaratibu wa kupitia kwa masheha ili kupata miche hiyo, inaweza kuwakosesha wengi kutokana na siiuntafahamu iliopo.


Kitengo cha Mashamba ya Misitu na Vitalu kisiwani Pemba, kimeanza utaratibu wa ugawaji miche ya mikarafuu bila ya malipo kwa zaidi ya miaka mitano sasa, ikiwa ni njia moja wapo ya kunyanyua hadhi ya zao hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.