Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Azungumza na Wajumbe wa Bodi ya ZECO)

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                           04.07.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelitaka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kufanya biashara isiyo na hasara na badala yake kuhakikisha linapata faida ili kuweza kuendesha vyema Shirika hilo.

Dk. Shein aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) pamoja na uongozi wake.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alieleza kuwa umefika wakati kwa Shirika hilo kuhakikisha linafanya biashara zake kwa lengo la kuleta tija kwani iwapo Shirika hilo litafanya juhudi za makusudi hilo linawezekana.

Aidha, Dk. Shein aliongeza kuwa lazima Shirika hilo la (ZECO) lihakikishe linaendesha vyema huduma zake kwa wananchi na wale wote wanaodaiwa na Shirika hilo ni vyema wakalipa madeni yao na wakishindwa kulipa hatua za makusudi zichukuliwe na Shirika hilo ikiwemo kuwakatia umeme kwa wale wadaiwa sugu.

Alisisitiza kuwa iwapo watafanya kazi vizuri mafanikio makubwa watayapata huku akiwasisitiza kuwa ni lazima deni linalodaiwa na (TANESCO) lilipwe ambapo Serikali kwa upande wake itaendeleza utaratibu ulioweka katika kuhakikisha kila mwezi deni hilo linalipwa.

Sambamba na hayo Dk. Shein alieleza haja ya kushughulikiwa kwa wafanyakazi wakorofi ambao wamo ndani ya Shirika hilo ambao husababisha ukosekanaji wa mapato huku akitumia fursa hiyo kueleza matumaini yake makubwa aliyonayo kwa Bodi ya Wakurugenzi ya (ZECO).

Dk. Shein aliongeza kuwa ni vyema kwa Shirika hilo la Umeme Zanzibar (ZECO) likajitayarisha kufanyakazi katika mazingira ya ushindani kibiashara kutokana na mpango wa Serikali wa kuishirikisha sekta binafsi katika miradi mbali mbali ya maendeleo ambapo wawekezaji wengi wameonesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Nae Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, alieleza haja kwa Shirika hilo kuhakikisha linakusanya vyema mapato yatokanayo na huduma hiyo hasa katika hoteli kubwa kubwa kwani hoteli ni nyingi lakini mapato yanayotokana na hoteli hizo ni kidogo.

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alilitaka ZECO kuangalia vyema umadhubuti wa vifaa vya umeme vinavyotolewa na Shirika hilo ikilinganishwa na bei zake huku akieleza haja ya kuondosha ubinafsi kwa uongozi na wafanyakazi wake, ambao hupelekea kufanya kazi kwa mazoea na hatimae kulitia hasara Shirika hilo.

Nao uongozi wa (ZECO) ulieleza hatua inazozichukua katika kuhakikisha inakusanya mapato yake sambamba na hatua za kusambaza huduma ya umeme kwa wananchi Unguja na Pemba.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la (ZECO) Hassan Ali Mbarouk, alieleza hatua zilizofikiwa kati ya Shirika hilo na Kampuni zitakazouza umeme kwa kufungua vituo katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma hiyo kwa ufanisi tofauti na ilivyo hivi sasa.

Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio na changamoto zilizopo katika Shirika hilo ikiwa ni pamoja na zile za matumizi ya umeme na kueleza haja ya kuendeleza utaratibu wa kuwepo kwa umeme mbadala hasa umeme wa gesi.

Nao uongozi wa Wizara ulieleza hatua za makusudi zinazoedelea kuchukuliwa katika kuhakikisha Shirika hilo linapata mafanikio sambamba na kuimarisha mahusiano na Bodi hiyo ya (ZECO).

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi katika Shirika hilo la (ZECO) Shafi Mussa Haji alieleza majukumu, utendaji wa kazi za Bodi hiyo, mafanikio pamoja na changamoto zilizopo.

Alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Bodi, Shirika limeweza kusambaza huduma ya umeme katika jumla ya vijiji 47 kwa Unguja na Pemba pamoja na kufungua vituo vya Gamba na Makunduchi vinavyotoa huduma za kiufundi kwa wateja wa maeneo ya karibu na hivi karibuni Shirika linatarajia kufungua vituo kama hivyo eneo la Dunga, Wilaya ya Kati.

Wakati huo huo, Dk. Shein ameeleza kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Serikali ndani ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) ikiwemo kutungwa kwa Sheria yamelipelekea Shirika hilo kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa biashara ya karafuu.

Dk. Shein aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) pamoja na uongozi wake.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Shirika la (ZSTC), kwa mafanikio makubwa iliyoyapata tokea kuanzishwa kwa mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Namba 11 ya mwaka 2011 na ile Sheria ya Maendeleo ya karafuu Namba 2 ya mwaka 2014.

Dk. Shein alieleza kuwa azma ya Serikali ya kurekebisha vituo vya kununua karafuu vya ZSTC sambamba na kuimarisha miundombinu ya barabara kwa maeneo yanayozalisha karafuu kwa wingi ni miongoni mwa hatua muhimu za kuliimarisha zao hilo na kukuza bishara ya karafuu.

Alieleza kuwepo Sheria hizo ndani ya Shirika hilo zitalisaidia katika kufikia  lengo la kuimarika kwa biashara ya karafuu pamoja na biashara nyenginezo ambazo zina maslahi na wananchi huku wananchi na wauzaji wa karafuu nao wakiendelea kufaidika.

Pia, Dk. Shein aliutaka uongozi wa (ZSTC) kutambua kuwa maghala yote ya Shirika hilo yaliopo Unguja na Pemba ni mali yao hivyo ni lazima wayasimamie vyema na kuyatunza.
Nae Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, alitoa pongezi kwa Shirika hilo kwan kuendelea kufanya vizuri na kueleza haja ya kuendelea kufanya vizuri kwani ni shirika la zamani na lina historia yake.

Waziri wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali alisema kuwa Shirika hilo ni miongoni mwa mashirika yaliopata mafanikio makubwa nchini Tanzania ambalo halijawahi kupata misuko suko hatua ambayo imetokana na miongozo mizuri ya Rais Dk. Shein.

Balozi Amina alieleza kuwa masoko ya bidhaa zinazozalishwa na ZSTC yapo hata nje ya nchi na kusisitiza haja ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa kuwashirikisha wakulima pamoja na vijana kulima mazao ya biashara yakiwemo viungo huku akieleza uwezekano wa kuzalisha asali, mbazi na dengu badala ya karafuu peke yake.

Aidha uongozi wa ZSTC ulieleza changamoto zilizopo sambamba na mafanikio yaliopatikana huku ukieleza hatua zilizopatikana za mafanikio kwa kupata mununuzi wa bidhaa za kwianda cha makonyo kutoka nchini China ambaye ameahidi kunua bidhaa hizo tani 40 kila mwezi.

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza haja ya kukiangalia kwa mtazamo wa uzalishaji wenye tija kiwanda cha makonyo kilichopo Wawi kwa kukifanyia ukarabati ama kukijenga upya ikiwa ni pamoja na kuweka mashine za kisasa kwa lengo la kuweza kuzalisha bidhaa kwa wingi.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) Kassim Maalim Suleiman, alisifu mashirikiano makubwa yaliopo kati ya Bodi na uongozi wa Wizara huku akieleza miongoni mwa mafanikio yaliopatikana ikiwa ni pamoja na kuwa na hakiba ya TZS Bilioni 5.2 kuanzia Julai mwaka 2016 hadi Machi 2017.

Mwenyekiti huyo alisema kwa mwaka huo wa 2016 hadi 2017 Shirika limeuza karafuu tani 2156 zenye thamani ya TZS Bilioni 36.6 huku akieleza haja ya kutotegemea zao loa karafuu peke na badala tyake kutafuta mazao mengine ambayo yatalipunguzia mzigo zao hilo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.