STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 01.07.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Rais wa Benki ya Maendelea
ya Afrika (AfDB) Dk. Akinwumi Adesina,kufutia kifo cha Mkurugenzi Mkuu wa Benki
hiyo Kanda ya Afrika Kusini, Dk. Tonia Kandiero,kilichotokea Juni 28, 2017 huko
mjini Pretoria nchini Afrika Kusini.
Katika salamu hizo za
rambi rambi, Dk. Shein alieleza kuwa ameshtushwa sana na kifo cha hafla cha
Mkurugenzi huyo wa (AfDB) katika Kanda ya Afrika ya Kusini Dk. Tonia Kandiero
ambacho kimeigusa sana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na jamii mbali mbali
za Bara la Afrika.
Dk. Shein alisema kuwa
kwa niaba yake binafsi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote
wa Zanzibar, wanatoa mkono wa pole kwa Rais Adesina, kwa Benki ya AfDB, wafanyakazi wote wa Benki hiyo pamoja
na ndugu na familia ya marehemu Tonia kutokana na msiba huo.
Salamu hizo za Dk.
Shein zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar pamoa na Serikali yao wanaendelea
kumkumbuka marehemu kwa mapenzi makubwa aliyonayo kwa Zanzibar ikiwa ni pamoja
na kuitembelea mara kwa mara kwa ajili ya kujumuika pamoja katika kupanga na
kutekeleza mipango ya maendeleo katika sekta muhimu za kiuchumi na kijamii hasa
miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, elimu na miradi ya maji.
“Daima tutaendelea
kutoa shukrani zetu kwake kwa kurahisisha shughuli za uratibu na majadiliano baina
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) pamoja na wahusika wengine muhimu
wa maendeleo kwani alikuwa mchapakazi mzuri na aliyetoa mchango mkubwa katika
nchi hii” zilieleza salamu hizo za rambi rambi alizotuma DK. Shein.
Aidha, salamu hizo za
rambirambi zilieleza kuwa hikma zake, busara zake na mapenzi yake makubwa vyote
kwa pamoja vitaendelea kukumbukwa sio kwa watu wa Zanzibar na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee bali zitakumbukwa na wapenda maendeleo
wote duniani kutokana na mchango wake mkubwa.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein katika salamu hizo za rambi rambi alimuomba Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) Dk. Adesina, kupokea
salamu hizo kwa msiba huo mkubwa uliotokea na kumuhakikishia kuwa mawazo, fikra
na majonzi ya Wazanzibari na Watanzania wote kwa jumla bado yataendelea katika
kumkumbuka kiongozi huyo
Dk. Shein alimuomba Rais huyo wa (AfDB) kuzifikisha salamu hizo za
rambirambi kwa Wanafamilia, Wafanyakazi na viongozi wote wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB).
Pamoja na hayo, salamu
hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira ndugu, jamaa na marafiki wa
Marehemu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu
kumlaza mahala pema kiongozi huyo.
Marehemu Dk. Tonia
kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa AfDB katika Ofisi za
Kanda ya Afrika ya Kusini mwishoni mwa mwaka 2016, alikuwa Mwakilishi wa Benki
hiyo hapa nchini Tanzania ambaye alifanya kazi zake hapa nchini kwa takriban
miaka sita.
Na Mnamo Disemba 21
mwaka 2016 maremu Dk. Tonia, alifika Ikulu mjini Zanzibar kumuaga Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiwa
anaelekea katika kituo chake kipya cha kazi huko Afrika ya Kusini, baada ya
kupewa majukumu ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika katika
Kanda ya Afrika ya Kusini.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment