Habari za Punde

Askari wa KMKM afariki dunia baharini, wanne wanusurika Maziwango'mbe


NA/ ALI  MASSOUD  KOMBO –PEMBA.


ASKARI wa KMKM kambi ya Kojani, Khamis  Yussuf Juma, amefariki dunia na wengine wanne kunusurika kufa  baada ya chombo walichokuwa amepanda kwa ajili ya doria kupata dhoruba na kupinduka baharini.

Katika  ajali hiyo iliyotokea  katika Bahari ya Maziwang’ombe Kisiwani Pemba , Askari wengine wane wa Kikosi hicho  walinusurika kufa na kukimbizwa katika Hospitali ya Micheweni kwa matibabu zaidi.

Akithibitisha kutokea kwa tokeo hilo , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji, aliwataja walionusurika katika ajali hiyo kuwa ni Rashid Kombo Makame , Idd Hamad Othman , Mohammed Mbarouk Salim na Mohammed Ali Ramadhan .

Alisema  Askari wa kikosi maalumu cha kuzuia magendo KMKM ,walikuwa katika safari kuelekea Tumbe kikazi wakiwa na chombo aina ya Fiber , inayomilikiwa na kikosi hicho kambi ya Kojani.

“Kuna tukio la chombo cha KMKM kuzama wakati wakiwa katika doria zao za kawaida na   katika tukio hilo Askari mmoja amefariki dunia huku wengine wanne wakinusurika kufa na walikimbizwa Hospitali ya Micheweni kwa matibabu, ” alifahamisha.

Hata hivyo Kamanda Haji, alielezea kusikitishwa na kitendo cha wananchi wa Maziwan’gombe cha kudai kulipwa fidia ya Tsh, 200,000/= (Tshilingi laki mbili )baada ya kusaidia uokozi .

Alifahamisha  wakati umefika kwa kila mmoja kurejea kwa Mungu na kuamini kwamba kitendo cha kusaidia uokoaji ni fungu  kutoka kwa Mungu na kuwataka kuendelea kusaidia panapo tokea ajali ,

Naye Daktari wa zamu Hospitali ya Micheweni, Khalfan Salim Said, alikiri kupokea mwili wa marehemu na kufahamisha kwamba kifo chake kimetokana na kunywa maji mengi akiwa baharini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.