Habari za Punde

Balozi Seif akutana Rais wa Bunge la Cuba jijini Havana, CubaMakamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd alipokuwa akizungumza na Rais wa Bunge la Cuba la Cuba, Mheshimiwa Esteban Lazo Hernandez alipokuta nae Havana leo huko kwenye Hoteli ya taifa.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema  Serikali ya Cuba imechangia kwa kiasi kikubwa kufungua milango kwa Zanzibar kuanzisha kitivo chake cha tiba katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)

Balozi Seif ameyasema hayo leo katika hoteli ya Taifa mjini Havana Cuba wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Bunge la Cuba Mheshimiwa Esteban Lazo Hernandez.

Balozi Seif amesema kitivo  cha  tiba kilichokuwepo SUZA ni matokeo ya Skuli ya Tiba iliyokuwepo Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyoanzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Cuba.

Amesema mchango huo wa Cuba kwa Zanzibar umesaidia  kufundisha vijana wengi wa Zanzibar katika fani ya utabibu kwa gharama nafuu na katika mazingira waliyoyazoea. 

Amesema kutokana na mchango huo wa Cuba  baada ya kipindi kifupi kijacho Zanzibar itakuwa na madaktari wa kutosha katika hospitali zake zote za Unguja na Pemba.

Naye Rais wa Bunge la Cuba Mheshimiwa Esteban Lazo Hernandez ameeleza kuridhishwa kwake na uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya Cuba na Tanzania na nchi za Afrika kwa jumla.

Mheshimiwa Esteban amesema Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanya za kiuchumi, kisiasa na kijamii na kusema: "Afrika imo ndani ya mishipa ya damu ya wanaCuba"

Akizungumzia hali ya kisiasa kwa jumla duniani, Mheshimiwa Esteban amewataka viongozi wa nchi mbali mbali duniani kujenga mustakbali mwema kwa wananchi wake na kuachana na siasa zitakazopelekea kuuangamiza utu duniani kutokana na vita, umaskini na uchafuzi wa mazingira unaopelekea kuongezeka kwa joto duniani.

Mheshimiwa Esteban amelipongeza bara la Afrika kwa kuunga mkono Cuba katika Umoja wa Taifa katika kuondolewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani. Amesema Afrika na Cuba ni ndugu na watu wenye asili ya Afrika nchini Cuba walichangia sana kupigania uhuru wa Cuba. 

Wakati huo huo Makamo wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametembelea maonyesho ya picha ya muasisi wa Taifa la Cuba Fidel Castro katika hoteli ya Taifa. 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.