Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Afunga Kongamano la Nne Katika Viwanja vya Ngeme Kongwe Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alilifunga Kongamano la Nne la Watanzania Wanaoishi Nje Diaspora, akiwahutubia na kutowa nasaha zake kwa Diaspora hao wakati wa ufungaji huo uliofanyika katika viwanja vya Ngome Kongwe Mji Mkongwe wa Zanzibar.  


Na. Mwandishi Wetu.
Kongamano lilodumu kwa siku mbili kwa kuwakutanisha watanzania waishio Ughaibuni (4th Tanzania Diaspora Conference) limehitimishwa hii leo Agosti 24, 2017 huku likiwa limehudhuriwa na Diaspora 350 na kuchagizwa na wahudhuriaji wengine ambao ni watendaji kutoka taasisi za serikali na wadau katika uwekezaji na uchumi.

Kongamano la nne la Watanzania waishio ughaibuni (4th Tanzania Diaspora Conference) lilifunguliwa jana tarehe 4 Agosti 2017 na Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayeshughulikia Mazingira Mhe Januari Makamba (MB)  alipomuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia suluhu Hassan ambapo limefikia ukomo kwa kupatikana majibu ya changamoto mbalimbali ziwahusuzo Diaspora ikiwemo uraia pacha na sera ya utambuzi wao nchini Tanzania.

Akihutubia mamia ya watanzania walioshiriki katika hafla ya chakula cha jioni iliyojulikana kama Swahili Barbeque Night iliyofanyika mji Mkongwe katika ukumbi wa Ngome kongwe-Zanzibara, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd alisema kuwa serikali inawatambua Diaspora kama mabalozi muhimu katika kutangaza utalii Duniani kote jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaongeza kipato cha nchi.

Alisema kuwa serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Diaspora katika kuitangaza nchi ya Tanzania na vivutio vyake hivyo kuwataka kutumia fursa hiyo pia kuwatangaza viongozi wa serikali kwa weledi mpana pasipo kueneza chuki dhidi ya viongozi wao.

Mhe alozi Seif alisema kuwa kumekuwa na watanzania waishio nje ya nchi wasiokuwa na weledi na nidhamu dhidi ya viongozi wa serikali kwani wamekuwa wakiwasema vibaya kwa kuwatukana na kejeli jambo ambalo linarudisha nyuma heshima yao waliyonayo na kutia doa serikali.

Alisema kuwa Diaspora wanapaswa kuendelea kushiriki katika makongamano mengine yajayo kwani kufanya hivyoi kunatoa fursa kwao kuishauri serikali na kuona namna bora ya utambuzi wao.

Alisema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili Diaspora waweze kutumia fursa ya uwekezaji nchini kwa urahisi huku akiwasihi kutumia fursa muhimu za uwekezaji katika Nyanja zote kwani faida itakuwa kwa Diaspora wenyewe, watanzania waishio nchini na Taifa kwa ujumla wake.

Alisema kuwa ushirikiano huo wa Diaspora kupitia makongamano yote yaliyopita umeimarisha zaidi mahusiano chanya bila kujali dini wala kabila jambo ambalo limeongeza utu, umoja na mshikamano.

Mhe alozi Seif alisema kuwa Diaspora wanatakiwa kuheshimu sheria, taratibu na taratibu za nchi wanazoishi ili kue delea kuipatia sifa chanya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Naomba nikukumbusheni nyote mliohudhuria hapa hii leo kutamnbua kuwa mchumia juani hulia kivulini nanyi kivulini kwenu ni hapa nyumbani hivyo tumie fursa ya uwekezaji vizuri huku mkikumbuka kuwa mkataa kwao ni mtumwa zaidi endelezeni umoja na mshikamano kwani inafahamika kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.” Alisema Balozi Seif Ally Idd

Kongamano la nne la watanzania waishio ughaibuni (4th Tanzania Diaspora Conference) linaratibiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusudio la kuwaweka pamoja watanzania hao ili kujadili kwa pamoja namna ya kutumia fursa za uwekezaji.

Kongamano kama hilo linaakisi makongamano matatu ya utangulizi yaliyofanyika mwaka 2014 na 2015 Jijini Dar es Salam huku kongamano la mwaka 2016 na mwaka huu 2017 yakifanyika visiwani Zanzibar huku likiwa limebebwa na dhamira ya “Uzalendo kwa Maendeleo” chini ya kauli mbiu isemayo “Mtu Kwao, Ndio Ngao”

Kongamano la watanzania waishio ughaibuni kwa mwaka 2017 limedhaminiwa na PBZ Bank, ZSSF, Idara ya Uhamiaji, Sea Cliff Hotel, CRDB Bank, Mult Colour, Equity Bank, Zanzibar Cable Television, ZBS, Watumishi Housing Cooparation na Petro.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.