Habari za Punde

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
                                                                            
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene anawajulisha wazazi, walezi na wananchi wote kuwa Mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi itafanyika tarehe 6-7/09/2017 kwa kuzingatia sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Baraza la Mitihani Tanzania.
Kwa mwaka huu wa 2017 jumla ya wanafunzi watakaofanya mitihani hiyo ni 917,030 kutoka katika shule za Msingi 16,581 ambazo ni  za Serikali na binafsi  zilizoko Tanzania Bara.
Maandalizi ya uendeshaji na usimamizi wa Mitihani hii umekwishakamilika katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kusafirishwa kwa mitihani na wasimamizi kutoka ngazi ya halmashauri kwenda kwenye vituo vya kufanyia mitihani na fedha kwa ajili ya gharama za usimamizi na uendeshaji wa mitihani.
Gharama zitakazotumika hadi kukamilika kwa zoezi la Mitihani ya darasa la saba ni Tsh Bil 29,474,964,600 na fedha hizo zitatumika kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa mitihani tu.
Waziri Simbachawene amewaagiza Wakurugenzi wote Nchini kutumia Fedha hizo zilizopokelewa kwa ajili ya mitihani kwa kufuata muongozo na kuhakikisha wanakamilisha mahitaji yote na kuwalipa wasimamizi staili zao ili waweze kufanya kazi hii  kwa moyo na kwa uadilifu.
Aidha Waziri Simbachawene amewatakia heri na baraka watahiniwa wote watakaoanza mitihani yao hapo kesho na kuwataka kuwa watulivu katika kipindi chote cha Mitihani na kufuata taratibu na maelekezo ya wasimamizi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano  Serikalini
Ofisi ya Rais
Tamisemi.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.