Habari za Punde

Ni JKU na Miembeni City Kesho Ngao ya Jamii.

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.
PAZIA la msimu ujao wa Ligi Kuu Soka Visiwani Zanzibar linatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho Jumanne Septemba 19 kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya JKU na Miembeni City, utakaofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Mjini Unguja majira ya Saa 10 za jioni.

Kuelekea mchezo huo tumezungumza na katibu wa timu ya JKU Saadu Ujudi ambapo amesema hawana wasi wasi wowote kwenye mchezo huo huku akiamini watatwaa Ngao hiyo.

“Sisi JKU hatuna hofu juu ya Miembeni City mimi niwaombe Mashabiki wafike kwa wingi kuja kuangalia wenyewe mchezo huo”. Alisema Ujudi.

Nae Ali Khamis ambae ni afisa habari wa Miembeni City amesema msimu huu wamekuja kufanya mapinduzi kwa timu za vikosi ambazo zinaonekana kutawala kwa muda mrefu soka la Zanzibar.

“Miembeni City tumekuja kufanya mapinduzi kwa timu za vikosi, na tutaanza kuwaonyesha kwenye mchezo huo wa Ngao”. Alisema Khamis.

Ligi kuu soka Visiwani Zanzibar inatarajiwa kuanza Oktoba 3, mwaka huu, kwa timu mbalimbali kuonyeshana kazi kwenye uwanja wa Amaan Mjini Unguja na Gombani Kisiwani Pemba.

JKU ndio wanaoshikilia ubingwa wa ligi hiyo, inayoshirikisha timu 28 kwa Zanzibar nzima ambapo kila kanda inajumla ya timu 14.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.