Habari za Punde

Ufungaji wa Ndoa Vijana 11 Kisiwa cha Tumbatu Zanzibar.

Na Ali Issa - Maelezo.

Upo  umuhimu mkubwa kwa wazazi  wa kiislamu kuwapatia elimu ya ndoa vjana wao wanaoingia katika sunna hiyo ili kupunguza migogoro na kuziwezesha ndoa zao zidumu kwa kipindi kirefu .

Hayo yamesemwa na kadhi wa wilaya ya kusini Sheikh Abubakar Ali wakati akitoa hutuba ya kufungisha ndoa za vijana 11 wa kisiwa cha Tumbatu waliopatiwa msaada na kituo cha Redio cha Adhana FM katika  hafla iliyofanyika msikiti Muhamad wa kisiwa hicho.

Alisema kumekuwa na mwamko kwa vijana wengi kuingia katika ndoa lakini zimekuwa hazidumu kutokana na wanandoa wengi kukosa elimu na hatimae kuongezeka kwa talaka.

“Moja ya njia za kupunguza mizozo ya ndoa ni  wanandoa kupatiwa elimu kabla ya kuingia ndani yandoa na ndio inayopelekea ndoa kudumu,”alisisitiza Sheikhe Abubakar.

Alisema kitendo cha vijana 11 wa Tumbatu kufunga ndoa kwa pamoja kwa msaada wa  Redio Adha FM ni jambo  la kihistoria kwani limewawezesha kukamilisha utu wao ukizingatia ukamilifu wa binaadamu ni kuowa ama kuolewa.

“Binaadamu aliyekamilika, hana matatizo ya afya, anapofikia umri wa mtu mzima  utu wake hawezi kukamilika bila kuowa ama  kuolewa kwani tendo hilo ni sunna na ibada katika uislamu na lilianza na mitume,” alisema Kadhi wa Wilaya.

Aliwataka wanandoa hao kuishi kwa wema, kufanyiana ihisani na kudumisha mapenzi ili kuzifanya ndoa zao kudumu na kuwashauri inapotokea hitilafu ndogo ndogo kurudi kwa wazee kutafuta suluhu na asiwe kuachana.

Nae Sheikh Khamis Abdulhamid kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali zanzibar alikumbusha kuwa asili ya ndoa ilianzia kwa baba wa Ulimwengu Adamu wakati alipo mtoa hawa ubavuni kwake kufuatia amri ya Mwenyezi mungu na kumuwoa.

Alisema hakutakuwa na mapenzi wala kuoneana huruma bila ya kuwa na utulivu, na utulivu unapatikana kwa watu kuingia ndani ya  ndoa hivyo aliishukuru Redoa adhana kuwasaidia vijana hao na kuzishauri taaisi nyengine zenye uwezo  kuiga jambo hilo kwani limeelezwa ndani ya uislamu.

“Ziko baadhi ya nchi zimeweka mifuko ya fedha kwa ajili ya kuwasaidia raia wao wasiokuwa na uwezo katika masuala ya lazima likiwemo suala la ndoa, nasisi tujenge tabia ya kusaidiana,”alishauri Sheikh Abdulhamid.  

Alisema kuwasaidia wa fedha watu  waliokuwa hawana uwezo kwa ajili ya kuowa ni jambo zuri na limeelezwa ndani ya vitabu vya Allah.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Radio Adhana Salum Muhamed Abdisalim alisema wameamua kuwasaidia vijana kuingia katika Suna ya ndoa na haitakuwa mara ya mwisho bali wataendelea kuwasaidia vijana wengine kila hali ya fedha itakaporuhusu.

Alisema Bodi inaamini kuwa kitendo hicho ni kuendeleza imani ya dini ya Kiislamu na malipo yake watayakuta yakiwa makubwa zaidi mbele ya mola wao.

Wazazi wa vijana  waliofunga ndoa waliushukuru uongozi  wa redio adhana kwa kuwaingiza watoto wao katika maisha ya ndoa kwani ni jambo jema kwao na Mwenyezi Mungu ndio atakaewalipa kwa kutekeleza jambo hilo kubwa.                      

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.