Na.Haji Nassor - Pemba.
Wananchi wa wilaya ya Chakechake
kisiwani Pemba, wametakiwa kufanya shughuli zao mbali mbali za kimaendeleo
ikiwemo kilimo, ili kujihakikishia maisha bora, badala ya kukaa barazani na
kupiga soga.
Kauli hiyo
imetolewa na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru, Amour Ahmada Amour kabla ya
kuweka jiwe la msingi la nyumba bora kijiji cha Matuleni, kwenye mbizo za
mwenge zilizoanza wilayani humo, ukitokea wilaya ya Mkoani.
Alisema kila
mwenye uwezo wa kufanya kazi, basi ahakikishe hilo analifanya kwa nafasi yake,
badala kukaa bila ya kujishughulisha, kwani hawatowezi kufikia maendeleo.
Alisema kazi
ndio msingi mkuu wa mwanadamu kuwepo ulimwenguni, hivyo ikiwa wataamua kukaa
barazani na kuachana na hilo, wasitarajie mabadiliko kati yao.
“Mimi
nimefuatana na mwenge wetu huu wa uhuru, kazi kubwa ni kuwakumbusha na
kuwaamsha kuwa, kila mmoja afanye kazi, maana matokeo yake ni manufaa ya
kweli”,alieleza.
Aidha
kiongozi huyo wa mbizo za mwenge, wamewataka wanafunzi kote nchini, kuweka
pembeni anasa na michezo isiokuwa na tija kwao, na badala yake washughulike
masomo yao.
Alisema wazazi
na walezi wao, wamekuwa wakihangaika huku na kule kuhakikisha wanapata mlo,
hivyo kazi iliopo mbele yao ni kusoma na sio vyenginevyo.
Wakati huo
huo kiongozi huyo wa mbio za mwenge na ujumbe wake, mara baada ya kukifungua
kituo cha afya Pujini na kutoa matone ya vitamin ‘A’ kwa watoto waliochini ya
umri wa mwaka, alikataa kugawa vyandarua kwa wazee na watoto hao.
Mara baada
ya tukio hilo la kutoa matone na kukitembelea kituo hicho cha afya,wakati
ukafika wa kugawa vyandarua ndipo, alipomba orodha ya wanaostahiki na
kukosekana.
“Nimemaliza
kutoa matone, sasa naomba orodha (majina) ya wananchi hao 10, wanaopaswa
kugawawi vyandarua, jamani orodha iko wapi, nahitaji hayo majina ili nipate
kugawa, au vipi, mbona sipaji jibu”,alihojia Kiongozi huyo wa mbio za mwenge.
Wakati hayo
yakijiri Afisa wa afya wilaya ya Chakechake, Kombo Omar Abdalla, alikuwa tayari
na vyandarua 10 mkononi mwake, huku akimshawishi kiongozi huyo wa mbio za
mwenge kuvigawa, ingawa ilishindikana.
“Muheshimiwa
vyandarua ndio hivi unavyopaswa uvigawe kwa wananchi hawa wakiwemo na wazee,
lakini orodha hatuna isipokuwa walengwa wenyewe ndio hawa, au unajua majina
yapo, lakini, sasa vipi, hivi vyandarua”,aliomba bila ya mafanikio.
Baada ya
dakika tatu kupitia bila ya kitolewa orodha, kiongozi huyo wa mbio za mwenge
pamoja na wakimbiza mwenge wake na mkuu wa wilaya ya Chakechake, waliondoka kituoni
hapo, na kuendelea na ratiba yao kwenye wilaya hiyo.
Afisa wa
Afya wilaya ya Chakechake, baadae aliwaomba radhi wazee hao waliopaswa
kukabidhiwa vyandarua hivyo, kwa hilo lililojitokeza na kuahidi kukabidhiwa
kwenye mkesha wa mwenge, uwanja wa Gombani.
Ujenzi wa
kutuo hicho cha afya daraja la pili, ulianza mapema Feubuari 11, mwaka jana kwa ushirikiano wa wananchi,
serikali na wafadhili IDC Foundation kutoka Itali, kwa thamani ya zaidi ya shilingi
milioni 138.
Kati ya
fedha hizo shilingi milioni 7, zimetolewa na Serikali, shilingi milioni 4
wananchi na wafadhili husika wametoa shilingi milioni 127, 237,520 ambapo kituo
hicho, kinatarajiwa kuwahudumia wananchi 9,843 kutoka shehia za Pujini na
vijiji jirani.
Awali Mkuu
wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdulla, alimkabidhi mwenge huo Mkuu wa wilaya mwenzake wa
Chakechake Rashid Hadid Rashid, kwa ajili ya kuutembeza wilayani mwake.
Mbio za mwenge wa uhuru
mwaka huu 2017, zilizinduliwa katika viwanja vya Kumbu kumbu mjini Mpanda
mkoani Katavi, April 2, hivyo baada ya kukimbizwa kwenye mikoa 31, na halmashauri 195, utahitimishwa mbizo zake
kwa kuzimwa Mkoa wa mjini Magharibi Unguja hapo Oktoba 14 mwaka huu, ambapo
ujumbe wa mwaka huu’
SHIRIKI KUKUZA UCHUMI
WA VIWANDA KWA MAENDELEO YA NCHI YETU'
No comments:
Post a Comment