Habari za Punde

Mchezaji Bora wa Ufungaji kwa Mwaka 2016/2017 Aanza Kuonesha Makali Yake Ligi Hii Baada ya Kuaza Kutimua Vumbi Katika Viwanja Vya Amaan na Gombani Pemba.

Na: Abubakar Khatib “Kisandu”, Zanzibar.
Mfungaji bora wa ligi kuu ya Zanzibar kwa msimu uliopita wa 2016/2017 Ibrahim Hamad Hilika anaecheza klabu ya Zimamoto jana ameanza kuonyesha makali yake baada ya kufunga bao pekee Zimamoto walipoichapa Taifa ya Jang’ombe bao 1-0 kwenye mchezo wa ligi kuu ya Zanzibar kanda yaUnguja uliopigwa saa 1 za usiku katika uwanja wa Amaan.
Bao hilo amefunga katika dakika ya 69 kufuatia makosa ya mlinzi wa Taifa Ali Juma (Mabata) pamoja na Mlinda mlango wake Ahmed Ali (Salula) kutoelewana na kumfanya Hilika kufunga kirahisi.
Msimu uliopita wa mwaka 2016/2017 Hilika aliibuka kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Zanzibar baada ya kufunga jumla ya mabao 14 katika hatua ya 8 bora.
Pia katika kanda ya Unguja msimu uliopita Hilika aliongoza kwa kushinda jumla ya mabao 19 katika kanda hiyo, hivyo ukipiga hesabu 19 na 14 utapata 33 ambayo ndio idadi ya mabao aliyofunga msimu mzima wote tangu ligi ilipoanza kanda mpaka kufikia hatua ya 8 bora.
“Malengo yangu ni kucheza soka Tanzania bara au nje ya Tanzania, uwezo ninao naamini ipo siku ntafika kwani jitihada yangu na uwezo wangu unaonekana, pia nimefurahi kuanza kufunga bao katika mechi yangu ya kwanza, msimu huu pia natarajia kuchukua mfungaji bora”. Alisema Hilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.