Habari za Punde

Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya wauguzi Zanzibar

 Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Omar Abdallah Ali akitoa maelezo ya mkutano mkuu wa siku mbili wa uchaguzi wa Jumuiya hiyo  unaofanyika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi Mjini Zanzibar.
  Mwenyekiti wa Jumuiya  ya Wauguzi Zanzibar Valeria Rashid Haroub akieleza mafanikio yaliyofikiwa na Jumuiya hiyo tokea ilipoanzishwa mwaka 1980 katika mkutano mkuu wa uchaguzi unaofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi.
 Baadhi ya wauguzi na wakunga walioshiriki mkutano mkuu wa Jumuiya ya wauguzi Zanzibar wakifuatilia ufunguzi wa mkuno huo unaofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi.

 Muuguzi Said Muhammed Salum akisoma Risala  ya Jumuiya ya ZANA katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi unaofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi Mjini Zanzibar.

Naibu Waziri wa Afya  Harusi Said Suleiman akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya wauguzi Zanzibar unaofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi (kulia) Katibu Mkuu wa wizara hiyo Asha Abdalla Ali na (kati) Mwenyekiti wa Jumuiya ya wauguzi Valeria Rashid.

Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezo 

Wakunga na wauguzi wamekumbushwa umuhimu wa kuitumia fursa iliyotolewa na Serikali ya kujiendeleza kielimu na kuhakikisha elimu watakayoipata inaleta manufaa kwa jamii na taifa kwa jumla.

Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman alipokukwa akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya wauguzi Zanzibar (ZANA) katika Chuo Maendeleo ya Utalii Maruhubi.

Aliwaeleza wauguzi na wakunga kwamba katika kukabiliana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknonlojia duniani wanahitaji kuwa na taaluma ya hali ya juu ya maswali ya kada zao ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Alisema hivi sasa malalamiko ya wananchi juu ya wauguzi na wakunga yameanza kupungua lakini wanahitaji kuongeza juhudi kuhakikisha lawama zinazotolewa na wananchi zinaondoka kabisa.

Naibu Waziri liwataka kuongeza ushirikiano  na kutoa huduma sawa kwa watu wote bila ya kuangalia jinsia, itikadi ya kisiasa na wenye uwezo na wasio na uwezo na kuakikisha wanatumia lugha nzuri kwa wagonjwa na wasaidizi wao wakati wa kuwahudumia.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Valeria Rashid Haroub ameiomba Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu kuhakikisha vyuo vyote vinavyotoa taaluma ya Uuguzi na Ukunga kuhakikisha vinachukuwa wanafunzi wenye sifa na kwa idadi inayokubalika na Baraza la wauguzi.

Aidha walivitaka vyuo vyote kufuata viwango vilivyowekwa kisheria ili kutowa wauguzi bora na kupunguza malalamiko katika jamii.

Katika risala yao iliyosomwa na Said Mohd Salum walisema Jumuiya ya ZANA inalengo la kuinua hadhi ya wauguzi na wakunga pamoja na taaluma yao ili waweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa na wenye kuhitaji msaada wao.

Walisema katika tafiti zilizofanywa katika siku za karibuni zimeonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi waliohojiwa wameeleza kuridhishwa na huduma wanazopata wanapofika hospitali na vituo vya afya.

Hata hivyo walisema kuwepo muundo wa utumishi unaopelekea utaratibu usioridhisha katika nyongeza za mishahara na tafauti iliopo baina ya mishara ya wauguzi na wakunga ukilinganisha na madaktari ni moja ya tatizo linalosababisha kupunguza ari ya utendaji.

Walieleza kuwa kukosekana kwa bima ya afya kunapelekea wauguzi, wakunga na familia zao wanapopata matatizo ya afya kukosa pakukimbilia na hatimae hubeba mzigo mzito wasioweza kuumudu ni changamoto inayowakabili hadi hivi sasa.

Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar inafanya uchaguzi wa viongozi wapya watakao ongoza kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo Mwenyekiti wa sasa Valeria Rashid Haroub anagombea kwa mara nyengine nafasi hiyo.
                            

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.