Na.Haji Nassor - Pemba.
WANANCHI wa wilaya ya Micheweni
kisiwani Pemba, wameshauriwa kujitenga mbali na viashiria vinavyoweza
kusababisha migogoro na kisha vurugu, kwani gharama ya kuirejesha amani iliotoweka,
ni kubwa kuliko urahisi wa kuichafua.
Ushauri huo
umetolewa na Afisa Mdhamini wa Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali kisiwani
humo, mwalimu Salim Kitwana Sururu, alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja,
wa kujengewa uwezo mpana wa kutatua na kukinga migogoro, uliotayarishwa na Jumuia
ya Zanzibar Youth Forum na kufanyika skuli ya sekondari Micheweni.
Alisema, ni
jukumu la kila mmoja kwa nafasi yake na mahala anapofanyia kazi, kuhakikisha anajikinga
na viashiria vya aina mbali mbali, ambavyo vinaweza kusababisha migogoro na
hatimae vurugu, vinavyoweza kupelekea hata vifo.
Alisema,
kujenga utamduni wa kusameheana, kuvumiliana, kuoneana huruma na kuthamini utu
wa mtu, ni miogoni mwa njia sahihi za kuzuia migogoro na kisha vurugu, ndani ya
jamii.
Hata hivyo,
alisema lazima waelewa kuwa, viashiria hivyo vinaweza kuanzia ngazi ya familia,
jamii, shehia, majimbo, wilaya, mkoa na hata taifa na hatimae, kusababisha
kupotea kwa amani na utulivu.
“Jamii
lazima tujenge utamaduni wa kuheshimiana na kuvumiliana kwa dhati ya moyo, ili
kuhakikisha hatusababishi migogoro yanayoweza kupelekea vurugu hapo baadae”, alifafanua.
Katika hatua
nyengine, Afisa Mdhamini huyo, alisema mradi wa kuwajengea uwezo jamii, kwenye
wilaya nne za Micheweni, Magharibi A, Kaskazini A na wilaya ya Mjini Unguja,
itasaidia kupunguza migogoro na vurugu, kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Mapema
Mratibu wa mradi wa kukuza uwelewa juu ya kuishi kwa amani, maelewano, na ututuzi
wa migogoro katika jamii, kutoka Jumuia ya Zanzibar Youth Forum, Almas Mohamed
Ali, alisema ujio wa mradi huo, utakapomalizika utasaidia jamii kupata uwelewa,
ili wajikinge na migogoro na vurugu.
Alisema
katika mradi huo, Zanzibar Youth Forum imechagua wilaya nne, ili kutekeleza
mradi huo, kwa kuwapa mafunzo waalimu wa skuli za sekondari, waalimu wa
madrassa, wanajumuia za kiraia, vijana na hata watendaji serikali, kwa vile
maeneo yote hayo, hutokea migogoro na kisha vuruga.
Akiwasilisha
mada ya utatuzi na migogoro na viashiria vyake, muwezeshaji Hassan Jani Massoud, alisema migogoro inaweza
kusabishwa na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kukoseshwa huduma, kutengwa,
kujenga dhana ya kukosa haki pamoja na kunyimwa uhuru.
“Wakati
mwengine vurugu na migogoro husababishwa na kutokuwepo kwa taarifa endelevu,
baina ya pande moja na nyengine, jambo ambalo ndio lililotawala katika maeneo
kadhaa”,alisema.
Baadhi ya
washiriki wa mkutano huo, walisema migogoro hijitokeza pindi haki
isipotekelezwa kwa upande mmoja, na hatimae kujitokeza vurugu, inayosababishwa
na migogoro iliodumua kwa muda mrefu.
Mwalimu wa
madrassa Ahmad Hassan Bakar, alisema jambo la kwanza katika kuzuia migogoro na
hatimae vurugu, ni kuhakikisha kwanza haki inatekelezwa kwa mwenye haki, ili
kumuweka akiwa na amani.
Nae Sharif
Ahmad Mwinyi alisema, waalimu wa skuli, madrassa na viongozi wa jumuia za
kirai, ndio watu sahihi wanaoweza kuwaelimisha jamii, juu ya kujitenga na
viashiria vinavyoweza kusababisha migogoro na kisha vurugu.
Jumuia ya
Zanzibar Youth Forum ambayo imaeanzishwa mwaka 2001, tayari imeshawaokoa vijana kadhaa na
utumiaji wa dawa za kulevya, kuwajengea uwezo katika kuingia kwenye safu ya
uongozi, wakiwemo wanawake na wanaume.
No comments:
Post a Comment