Habari za Punde

Wafanyakazi Wapata Mafunzo ya Utengenezaji wa Viungo Bandia Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar

Na Ali Issa    Maelezo     23/10/2017
Visaidizi vya viungo bandia vinavyo tolewa hospitali ya Mnazimmoja kwa msaada wa washirika wa maendeleo vinawasaidia walemavu waliopoteza viungo  katika harakati zao za kila siku za maisha.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mafunzo wa hospitali ya Mnazimmoja Mwinyi Issa Mselem alipokuwa akifunguwa mafunzo ya utengenezaji wa viungo bandia vya miguu na mikono katika teknolojia ya kisasa na yenye ubora kwa wataalamu wa Hospitali hiyo. 

Amesema Zanzibar  imekuwa na walemavu wengi waliopoteza viungo  kwa njia za maradhi na ajali za mara kwa mara, hivyo kupatiwa mafunzo ya kutengeneza vifaa hivyo kwa kutumia teknolojia hiyo itawasaidia  wenye mahitaji kupata vifaa  kwa urahisi.
Amewataka walemavu watakaobahatika kupata msaada huo wa viungo bandia kuutumia katika shughuli zao za kila siku za kujitafutia riziki.

Mkurugenzi mafunzo  alikumbusha kuwa ulemavu sio mwisho wa maisha na kukata tama na alisema  wapo walemavu waliokosa viungo muhimu na wanatumia viungo bandia na wanatoa mchango mkubwa katika jamii yao na taifa kwa jumla na maisha yao yanaendelea vizuri.

Aliwashauri walemavu wa Zanzibar  waache tabia ya kubweteka na waone kuwa hali walionayo kuwa ni mtihani na waendelee kutumia viungo bandia kwa maendeleo yao.

Mtaalamu wa kutengeneza  viungo bandia kutoka kampuni ya Swiss Limbs ya Swizaland Dkt.Helvio  Corli Rossini alisema wamekuja Zanzibar  kuelimisha utengenezaji bora wa viungo bandia kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayoitwa Affordable Technology for Advanced Mobility ambayo viungo vyake vinamfanya mtumiaji kutembea bila matatizo .

Alisema watatoa mafunzo ya siku tano na katika kipindi hicho  watatengeneza viungo na kuwapatia walemavu wenyemahitaji na wataalamu wazalendo wataendelea kutengeneza na kuvigawa  baada ya kupatiwa taaluma hiyo. 

Nae mkuu wa kitengo cha kutengenezaji  viungo hivyo kutoka hospital ya chake chake  Dkt. Salum alisema kuwa watalamu hao wamekuja kwa njia ya kujitolea kwa ushirikiano wa Hospitali ya Mnazi Mmoja na  Mradi wa ZOP. 

Mmoja kati ya wataalamu wanaopatiwa mafunzo hayo Dkt. Munira aliwashukuru wataalamu hao kutoka Swizaland na ameahidi kuwa watafuatialia kwa karibu ili kuhakikisha wanatoa mchango mkubwa katika kuwafariji wenye mahitaji.

Nao walemavu ambao wamepimwa kwa ajili ya kupatiwa msaada huo bila malipo waliishukuru Serikali kwa kuwajali na kuwapatia visaidizi hivyo na kuomba msaada huo usiishie kwao tu bali uendelee kwa walemavu wengine kwani visaidizi vya viungo bandia  ni ghali na baadhi hawana uwezo wa kuvinunua.

Waliahidi kuwa  watakapo kabidhiwa msaada watahakikisha wanavitunza na kuvitumia kwa mahitaji yao ya kila siku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.