Habari za Punde

Kukithiri kwa Ujinga au Ulimbukeni katika jamii yetu

Na Bi Hekima

 Ingawa kuna tofauti kati ya mtu mjinga na limbukeni ndani ya mji wetu watu wa aina hii wamejaa. Inatupa baadhi yetu shida, tena ku wa maana kama mtu unajiheshimu basi unaweza kujiharibia kwa kutaka kufanya jambo la kheri au kwa kumuelekeza mtu dhidi ya mwenendo wake usiostahili. 

Alimradi ukisema inakuwa tabu na usiposema ndo watu, hususan vijana wanazidi, kuharibikiwa. 

Nitatoa mifano miwili ya yalionikuta karbuni kuonyesha jinsi jamii hii inavyo haribikiwa. Na sote tu waathirika wa hali iliyopo maana kama huioni kwako basi utakumbana nayo ukitoka tu. Hakuna atakayepona!

Hivi sasa nimerudi kwangu nikiwa mwingi wa mawazo. Nilikuwa napita katika mitaa yetu haya membamba yanoyopita kila kitu. 

Kuna vijana wamekodi maduka njia ambazo wengi wetu ndio tunapita lakini ingawa wanayo maduka yao hawakubali isipokuwa kukaa vibarazani au nje ya maduka yao wakisubiri wazungu wa kugombania. 

Kwa vile mitaa ni miembamba na pia waenda kwa miguu na walio katika vyombo ni wengi kwa kukaa nje ya maduka yao wanaleta msongamano mkubwa. 

Mmoja katoka dukani kwake wakati napita akaja kunisimamia mbele yangu nikiwa na mwamvuli wangu nakwepa mvua. 

Sasa alitaka nimwambie nini? Nimuombe au nimseme ingawa kwangu hatua zote mbili hazifai bali kinachofaa ni kumtanabahisha mtu na jambo analolifanya ili ajirekebishe. 

Haiwi kuwa mtu mzima na akili zake hatambui kuwa njia ni ya wapita njia. Waruhusiwe kupita bila bughdha isiyo ya lazima. Yeye kashindwa kunipisha njia labda akitaka tuanze kutukanana. Huu ni ujinga.

Kisa cha pili kinahusu ulimbukeni. Juzi nlienda kutafuta ndara madukani. Nilipokuwa maeneo ya Mtendeni kuja Vikokotoni nkaingia katika duka mmoja. Nkauliza bei na kutaka kujaribu. 

Kijana akawa anataka kunipa jozi njaribu lakini kwa vile wakati nampa maelekezo kanipa mgongo hajaona nlichokuwa namuonyesha. Nkaamua nimwambie "hicho kiloandikwa  'FS' lakini jamaa kakazana ananionesha viatu anavyotaka yeye. 

Baada kumshitua kama mara 3 ikanipitia kuwa labda hajui kusoma na kuandika! Hivyo nkamtajia na rangi ya viatu ndipo aliposhtuka na kunirushia vile viatu halafu akaenda pembeni na zake kuchukua simu anatia story. 

Hakika mabega yakaniteremka. Nkawa namuuliza mwenzake ambaye naona wamefanana "vipi huyu? Mbona ananirushia kiatu halafu huyo?" Jibu la yule mwenzake "si unamuona mtu mwenyewe?" Jibu sijalifahamu na wala halijaniridhisha ingawa najua kuwa siku hizi watoto na vijana hawagombwi wakifanya sivyo.

 Desturi imekuwa au kumezea au kuwapongeza kwa 'ubabe' wao. Alimradi si kafanikiwa kukukera? hili ndilo linakuwa gumzo la baraza, "si umeona? Kaja nkapiga stopu...." kama vile uligoka kwako unafuata ushari. 

Alipomaliza kuongea na simu nkamkabili na kumuuliza kwa nini kanirushia kiatu?. Jibu lake la kifedhuli ni "nkitaka nichukue au nitoke zangu pale hataki kufanyiwa kelele" huyo kaka yake kaka hapo na 'sura ya kusuta' hajathubutu hata kumsemesha au kumnasihi mdogo wake.

Wacha ukweli kuwa aliyenifanyia utovu wa adabu ni mdogo sana kwangu  hata huyo mkubwa mwenzangu ambaye angeweza kumrai naye mtizamo wake na Wa ndugu wake umefanana na ni wa ubabe wa kijinga.

Aidha kwa vijana wanaotaka kuendeleza biashara zao, nimesikitika kuwa hawana ufahamu wa hawaoni umuhimu wa customer care yaani kumjali mteja.

Hivyo na mimi nkaona hakuna haja kuacha pesa yangu. Neno nliloondoka nalo pale ni kumwambia hiyo ni tabu ya kutojua kusoma na kuandika: hata busara mtu unakosa!

Kwa bahati mbaya tabia hii ya ulimbukeni  vijana wa hapa kwetu wanazidi kutiwa na hotuba za wanaojinasibisha na 'usheikh au uustadh' lakini wakawa hawana kauli isipokuwa kukashifu mwengine au kudharau wengine.

Hawana upeo ya mahusiano wala uchu wa kutaka kujiadabisha nafsi, kuheshimu wengine au kuwa waungwana. Kwao wao kila kitu ubabe, ufedhuli au ujinga. Hawa ndio malimbukeni. Mwenyezi Mungu au awaongoe au atukinge nao

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.