Habari za Punde

Ujenzi holela na utupaji taka ovyo sababu kuu ya kutokea athari za mafuriko

 Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Moh’d  aliyesimama akitoa Taarifa ya athari za Mvua za Vuli za Mwaka 2017 zinazoendelea kunyesha Zanzibar na hatua zinazopendekezwa kuchukuliwa mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Wa kwanza Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikiongoza Kikao hicho Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Kilimo Mh. Hamad Rashid Mohamed, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma.
Kulia ya Mkurugenzi Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa ni Waziri wa Hbari Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Rashid Ali Juma ma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Haji Omar Kheir.
Balozi Seif  akikiongoza Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar  kujadili Taarifa ya athari za Mvua za Vuli za Mwaka 2017 zinazoendelea kunyesha Zanzibar na hatua zinazopendekezwa kuchukuliwa.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis , OMPR

Ujenzi holela kwenye njia za asili za maji hasa katika maeneo ya mabondeni, ujenzi wa miundombinu ya Bara bara usiozingatia uwepo wa misingi ya kupitishia maji ya Mvua sambamba na utupaji wa taka taka  ovyo ndio sababu kubwa zinazopelekea kutokea kwa athari za mafuriko ya mavua katika sehemu mbali mbali Nchini.
Mkurugenzi  Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar  Nd. Shaaban  Seif  Moh’d alisema hayo wakati akitoa Taarifa ya Athari za Mvua za Vuli za Mwaka 2017 zinazoendelea kunyesha Zanzibar  katika Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
 Nd. Shaaban Seif  Moh’d alisema  ili kukabiliana na tatizo hilo linalojitokeza kila mwaka  ipo haja ya kuyaekea uzio maalum wa kutoruhusu ujenzi katika maeneo hatarishi ili kupunguza uvamizi na ujenzi holela ambao unaonekana ndio chanzo cha athari hizo.
Alisema wakati umefika kwa Taasisi husika kutekeleza ipasavyo Sheria, Kanuni na Mikakati ya matumizi ya ardhi na mipango Miji sambamba na kuharakisha mpango wa kuyapima maeneo yatakayotumika kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba za Makaazi.
Alieleza kwamba hatua hiyo mara nyingi huenda  sambamba  na ongezeko la idadi ya Watu inayoonekana kupanda kwa kasi hasa katika Wilaya za Magharibi ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alifafanua kwamba Mvua zinazoendelea kunyesha licha ya kusababisha Vifo vya watu, uharibifu na upotevu wa Mali za Jamii lakini pia zilisababisha uharibifu wa Miundombinu ya Barabara Nchini.
Nd. Shaaban alisema Tathmini ya awali iliyofanywa na Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar kwa kushirikiana na Kamati za Maafa za Wilaya imebainisha kwamba jumla ya Nyumba 183 zimeathirika kwa kujaa maji katika Mkoa Mjini Magharibi.
Alisema Mvua hizo zilisababisha kubomoka kwa baadhi ya kuta za nyumba na Makaro ya Maji Machafu hali ambayo inaweza kusababisha kutokea kwa Majanga mengine yakiwemo magonjwa ya miripuko.
Mkurugenzi Shaaban alisema kwa mujibu wa Taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania,  Kanda ya Zanzibar,  kiwango cha Mvua kiliripotiwa kutokea Tarehe 26 Oktoba  Mwaka 2017  kimefikia Milimita  Mia 288.5  kwa muda wa saa Ishirini na Nne.
Alisema Kiwango hicho ni kikubwa zaidi na hakijawahi kuripotiwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi tokea Mwaka 1998 ambapo Mvua ya Milimita Mia 197.6  kwa siku iliripotiwa.
Hata hivyo alifafanua kwamba kwa upande wa Kisiwa cha Pemba Mvua za  msimu huu wa Vuli zinaendelea kunyesha vyema katika kiwango cha kawaida  bila ya kuleta athari yoyote.
Wakichangia Taarifa hiyo ya athari za Mvua za Vuli za Mwaka 2017 zinazoendelea kunyesha Baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo walisema  athari za mafuriko ya Mvua zitaendelea kuripotiwa kila msimu iwapo hatua za kudhibiti maeneo hatarishi hazitachukuliwa ipasavyo.
Walisema mashamba mengi ya Kilimo yamevamiwa kwa shughuli za Ujenzi wa Nyumba  za  Makaazi kiasi kwamba wahusika wa utoaji wa vibali bila ya kuzingatia Sheria  wanastahiki kuwajibishwa sambamba na Baadhi ya Madiwani waliohusika na  uzembe huo kuripotiwa Chamani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Hata hivyo Wajumbe hao walieleza kwamba  ipo hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika kufuata Sheria na Taratibu za Ujenzi kwa baadhi ya Watu waliopitia Taasisi inayosimamia Ardhi kwa kuyatumia vyema maeneo ya ujenzi  wa Nyumba za kuishi na matokeo yake kupunguza  usumbufu pamoja na msongamano.
Akiahirisha Kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema elimu kwa Umma lazima iendelee kutolewa ili kusaidia kupunguza maafa yanayoweza kuepukwa.
Balozi Seif  alisisitiza umuhimu wa  Wafadhili wanaojitolea kusaidia Maendeleo ya Jamii  katika maeneo tofauti wanawajibika kufikiria kuzingatia Sheria, Sera na Taratibu za Nchi ili kupunguza migongano na hitilafu ndogo ndogo. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.