NA HAJI NASSOR, PEMBA
JAMII nchini, imetakiwa kufanya kila mbinu, ili kuhakikisha
inafika mahakamani kutoa ushahidi, hasa kwenye mashauri ya udhalilishaji, na
kutovunjika moyo na changamoto zilizopo mahakamani.
Ushauri
huo umetolewa na wadau wa masuala ya kupinga udhalilishaji wa kijinsia kisiwani
Pemba, kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, juu
ya sababu zinazowafanya kutopenda kutoa ushahidi mahakamani.
Wadau
hao walisema iwapo jamii, watachoka kwenda mahakamani kwa sababu mbali mbali
zilizopo mahakamani, inaweza kuwarahisishia na kuwapa mwanya wanaofanya matendo
hayo, ikiwemo ubakaji na ulawiti.
Mratibu
wa wanawake na watoto shehia ya Mchanga mdogo, Siti Khatib Ali, alisema lazima
jamii iungane kisawa sawa kama ilivyokwenye mambo mengine, na kufika mahakamani
kutoa ushahidi.
Alisema
wanaotenda matendo kama ya ubakaji wamekuwa wakifuatilia watu iwapo wanafika
mahakamani kutoa ushahidi, na kama wanachoka, na wao hupata nguvu ya kuyaendeleza
matendo hayo.
“Lazima
jamii ione kuwa, suala la kutoa ushahidi mahakamani ni moja ya haki ya msingi
katika kutokomeza jinai, na kama wakikaa majumbani kwa kukosa nauli,na
udhalilishaji utanoga”,alifafanua.
Sheha
wa shehia ya Kiungoni wilaya ya Wete Omar Khamis Othman, aliitaka jamii ndani
ya shehia yake, kuhakikisha wanajipanga hata kwa kusaidiana na nauli, ili
kufika mahakamani kutoa ushahidi.
“Ushahidi
mahakamani ndio kigezo cha mtuhumiwa kutiwa hatiani, hivyo jamii ikiona ni shida,
wajuwe na udhalilishaji nao unanawirika”,alifafanua.
Mwanasheria
dhamana wa Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Pemba, Ali Rajab Ali alisema,
hakuna mashitaka ambayo mtu atatiwa hatiani, bila ya kuwepo kwa mashahidi.
Alisema
waendesha mashitaka, Polisi na hata mahakimu ni wageni wa makosa yote
yanayotokea, hivyo ili wayafahamu ni lazima mashahidi kufika mahakamani,
kuwaeleza mwanzo hadi mwisho wa tukio.
“Sisi
waendesha mashitaka, hatufahamu lolote iwapo kuna kosa limefanyika huko
vijijini, sasa kama wakija watu kutoa ushahidi au kupinga juu ya tendo fulani,
sasa hapo ndio ukweli hupatikana”,alieleza.
Afisa
miradi kutoka TAMWA, Asha Abdi Makame alisema, wapo wananchi wamekuwa wasugu
kutoa ushahidi, kisha kusingizia vyombo vya sheria, kuchukua rushwa.
“Ijapokuwa
harufu ya rushwa hutajwa kwa mahakimu, waendesha mashitaka na DPP, lakini hata
hivi kukataa kutoa ushahidi ni hatua ya kuziua kesi za
udhalilishaji”,alifafanua.
Katika
hatua nyengine Afisa huyo, alisema TAMWA katika kuunga mkono juhudi za
kupambana na udhalilishaji ndani ya jamii, wamekuwa na mradi endelevu wa GEWE.
Alifafanua
kuwa, ingawa kwa awamu hii ya Mradi huo wa kuwawezesha wanawake na kupinga
udhalilishaji, GEWE, unalenga zaidi kuwawezesha waandishi wa habari kuibua
habari zilizojificha.
“Wapo
waandishi wameshapewa taaluma na sasa wako kwenye shehia mbali mbali za Unguja
na Pemba, wakifanya uchunguuzi wa habari za aina tofauti juu ya udhalilishaji
ndani ya jamii, maana habari za kina ilikuwa hazijaandikwa”,alifafanua.
Afisa
ustawi wa jamii wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed, alisema mradi wa GEWE
umesaidia sana wilaya ya Wete na hasa zile shehia sita, zilizpotiwa na mradi.
Alisema
walau jamii imepata mwamko na kujua wajibu wao, katika mapambano ya kutokomeza
udhalilishaji wa kijinsia, jambo ambalo kabla, walidhani ni kazi za taasisi
husika.
“Sasa
inaonekana jamii, imepata uthubutu wa alau kutoa ushirikianao na wahusika
wanapopita kwenye jamii, maana wanaona kuwa, kushughulikia metendo haya ni
jukumu la kila mmoja”,alifafanua.
Hakimu
wa Mahakama ya mkoa Chakechake Khamis Ali Simai, alisema, mashahidi wote wanaofika
mahakamani, wamekuwa wakipewa nauli zao kama kawaida.
Hata
hivyo alisema, kukosekana kwa nauli hiyo kusiwarejeshe nyumbani mashahidi,
maana suala la kutoa ushahidi ni haki yao, hasa katika kuusaidia muhimili wa mahakama,
kufanikisha kazi zake.
“Jamii
ijipange vyema kuhakikisha wanakuwa na hamu kufika mahakamani kutoa ushahidi,
kwani hakuna kesi ambayo itafikia tamati, pasi na kuwepo kwa
mashahidi”,alifafanua.
Shehia
ambazo zimo kwenye mradi wa GEWE ni Kiungoni, Shengejuu, Mchanga mdogo, Mjini
ole, Kangagani na Kinyikani ndani ya wilaya ya Wete kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment