Habari za Punde

Waziri Mhe Aboud Azungumza na Watendaji wa Wizara Yake.

Na. Othman Khamis OMPR.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed  alisema watendaji wa Wizara hiyo wataendelea kutekeleza majukumu yao waliyopangiwa katika azma ya kusimamia vyema ushirikishwaji wa Wananchi katika shughuli zao za kila siku.
Alisema mazingira ya kazi yataimarishwa zaidi ili utekelezaji wa Mipango iliyowekwa na Taifa ufanikiwe kwa kuzingatia maelekezo yaliyopo na kufikia matarajio ya Bajeti ya Mwaka 2017/2018.
Mh. Mohamed Aboud Mohamed alisema hayo wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Kipindi cha Robo ya kwanza ya kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba Mwaka 2017/2018 kwa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wa Kitaifa hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mh. Aboud alisema Ofisi haitochoka kupokea na kuufanyia kazi ushauri utakaotolewa na Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wowote ili kwa pamoja utowe mwanga mzuri wa kuwahudumia vyema Wananchi na kuleta Tija zaidi kutokana na shughuli wanazofanya.
Akigusia wimbi la udhalilishaji wa kijinsia uliyoigubika jamii hivi sasa Mh. Aboud alisema Ofisi hiyo imefanya mafunzo juu ya Elimu ya uhamasishaji dhidi ya vitendo vya udhalilishaji ndani ya Mkoa Mjini Magharibi kupitia Masheha wa Wilaya zake zote Tatu.
Alisema mafunzo hayo yalilenga kupata mashirikiano na Masheha ili kutoa Taarifa za Udhalilishaji  wa Kijinsia  zinazotokea katika Shehia ambazo hufanyiwa Wananchi hasa Watu wenye ulemavu na kutafuta ufumbuzi wa pamoja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Ofisi yake  inafuatilia kesi za  udhalilishaji  ambazo zimewahusu watu walioamua kuwadhalilisha Watoto hasa wale wenye ulemavu.
Kuhusu Dawa za Kulevya Waziri Aboud  alisema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya imetoa mafunzo juu ya mapambano dhidi ya Biashara na Matumizi ya Dawa za Kulevya.
Alisema mafunzo hayo yalifanywa kwa kutumia vipeperushi kwa Viongozi na Wananchi katika Shehia 31 za Unguja zenye madiko yasiyo Rasmi yaliyokwenda sambamba na utolewaji wa vipeperushi 5,000 vya utoaji wa elimu juu ya madhara ya matumizi ya Dawa za kulevya kwa Jamii.
Wakitoa  mawazo yao baadhi ya Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya  Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wa Kitaifa walisema kazi nzuri inayofanywa na Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inaoneka kiasi cha kuleta faraja kwa Wananchi walio wengi.
Wajumbe hao walipongeza hatua hizo ambazo zinastahiki kuendelezwa kwa faid na ustawi wa Jamii ya Visiwa hivi vya Unguja na Pemba.
Kikao hicho kilichopokea Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Kipindi cha Robo ya kwanza ya kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba Mwaka 2017/2018 cha Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kilikuwa chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wa Kitaifa Mheshimiwa Omar Seif Abeid.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.