Habari za Punde

Kamishna Sururu atangaza Neema

• Makaazi ya Askari wa Uhamiaji kuendelea Kujengwa 
• Magari  na PikiPiki kuongezwa 
• Kipaumbele, Elimu ya Uhamiaji na Uraia kutolewa 
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari M Sururu


Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari M. Sururu amewataka Askari na Maafisa wa Jeshi la Uhamiaji kufanyakazi kwa Uweledi na kujituma ili kuweza kutekeleza vyema majukumu yao ya msingi ya kusimamia na kudhibiti Uingiaji, Ukaaji na Utokaji wa Watu Nchini. “Ili kuimarisha utendaji wetu ni vyema kuacha kufanya kazi kwa mazowea na muda wote, tutoe huduma za Uhamiaji bila ya Upendeleo, Unyanyasaji au Ucheleshwaji usio wa lazima. Tumieni lugha nzuri, zingatieni kwa vitendo dhana ya kumjali Mteja na Epukeni vitendo vya Rushwa wakati mkitoa huduma mbali mbali za Uhamiaji kwani Rushwa ni Adui nambari moja wa Haki” alisema Kamishna Sururu.

Kufanyakazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ndio mhimili mkuu wa mafanikio ya Taasisi yoyote ile ikiwemo ya Uhamiaji. Maafisa na Askari wa Uhamiaji wanapaswa kuheshimu na kutii Kanuni zote za kijeshi, “Idara yetu imeingia rasmi kwenye mfumo wa Kijeshi nasi hatuna budi kufanyakazi kwa Kasi, Ari na Mori kuhakikisha kwamba jukumu la Ulinzi na Usalama wa Mipaka ya Nchi yetu linatekelezwa ipasavyo” alisema hayo wakati akizungumza na Askari na Maafisa wa Uhamiaji waliopo Mkoa wa Kaskazini Pemba, akihitimisha ziara ya kikazi katika Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba iliyoanza tarehe 18 – 21 Disemba, 2017.

Aidha katika ziara hiyo, Kamishna Sururu alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali yenye changamoto za uwepo vipenyo na Bandari Bubu zinazotumiwa na wakaazi wa maeneo hayo, kwa shughuli mbali mbali zikiwemo za uvuvi na biashara, baina ya visiwa vya Pemba na Mombasa, Kenya. Kisiwa cha Pemba kinasemekana kuwa na Bandari bubu zaidi ya mia tatu (300) ambapo inaelezwa kuwa ni kimbilio kwa baadhi ya Raia wa Kenya na Raia wa Somalia ndani ya visiwa vidogo vidogo vilivyomo ndani ya Wilaya za Micheweni, Wete na Mkoani, Pemba.

Kamishna Sururu aliwasisistiza Askari wa Uhamiaji kuongeza Doria na Misako ili kuwabaini wale wote wanaojipenyeza na kuishi nchini kinyume cha Sheria za Uhamiaji nchini. “Pamoja na changamoto zilizopo kutokana na Jiografia ya Visiwa vya Unguja na Pemba, hatuna budi kusimamia vyema jukumu la Udhibiti wa Ungiaji na Utokaji wa Watu” “Kama mnavyoelewa jitihada mbali mbali zinazochukuliwa na serikali zetu zote mbili katika kuboresha utendajikazi wetu, Idara inatarajia kupata vitendeakazi pamoja na vyombo vya usafiri yakiwemo Magari na Pikipiki, ambavyo vitasaidia kuboresha utoaji wa huduma zetu kwa Jamii” alifafanua Kamishna Sururu.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bwana Omari Khamis Othman, alisema kutokana na Idara ya Uhamiaji Nchini kuingia rasmi kwenye mfumo wa Kijeshi, aliitaka Idara, kuzingatia uzalendo katika Uajiri wa Askari wake, ili kuhakikisha suala la utunzaji wa siri za serikali linapewa kipaumbele kinachostahiki.

Aidha, alitoa Rai kwa Idara ya Uhamiaji yenye mamlaka ya Kusimamia na Kudhibiti Uingiaji na Utokaji wa Watu Nchini, kuongeza idadi ya watumishi pamoja na kufungua vituo vingi zaidi, ili kuweza kusimamia kwa karibu mipaka ya nchi kwenye visiwa hivyo. “kuna maeneo yanahitaji uangalizi wenu wa karibu, kwa mfano Kigomasha, Shumba, Tumbe na Micheweni ni sehemu zinazohitaji kipaumbele cha kipekee katika Mkoa huu” Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati akizungumza na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari M. Sururu alipofika Ofisini kwake, wakati akiendelea na ziara ya kikazi mkoani humo.

Kwa upande wake Kamishna Sururu, alichukua fursa hiyo kumuomba Mkuu huyo wa Mkoa, kuendelea kushirikiana na Idara yake kutatua changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo, zikiwemo ukosefu wa Makaazi ya Askari wa Jeshi la Uhamiaji Mkoani humo. Alisema “Idara yetu imejikita kufanyakazi kwa Uweledi ili kuleta ufanisi, lakini lengo hilo halitafikiwa ikiwa Askari wetu hawana Makaazi bora, Ofisi na vitendea kazi vya kisasa, Idara imejizatiti kutatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya Usafiri na kuboresha Ofisi zake takriban zote hapa Pemba”.

“Hivyo, nakuomba kwa mamlaka uliyonayo utusaidie kutupatia maeneo na Viwanja ili tujenge makaazi bora ya Askari wetu na nitoe ahadi kwako, kuwa pindi tutakapopata viwanja hivyo, basi utekelezaji wa miradi hiyo utaanza mara moja ili kukamilisha adhma hiyo njema ya kujenga makaazi bora ya Askari wetu hapa Mkoa wa Kaskazini Pemba, kama ambavyo tumefanikiwa kuweka makaazi hayo kwa kujenga Jengo la kisasa eneo la Ndugu Kitu, Wilaya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba” alisema Kamishna Sururu.

Aidha, katika ziara hiyo Kamishna Sururu, alitumia vyema fursa hiyo kwa kuongea na Wananchi na Masheha wa shehia mbalimbali alizotembelea na kuwataka kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, kwani mapambano dhidi ya Uhamiaji Haramu ni makubwa na yanahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Wananchi wote.

“Naomba muelewe kuwa nafasi yenu katika utekelezaji wa majukumu yetu ni kubwa sana, sisi tumepewa dhamana ya Kusimamia na Kudhibiti Uingiaji, Utokaji na Ukaaji wa wageni wote hapa nchini kwetu. Jukumu ambalo utekelezaji wake unategemea sana kupata taarifa sahihi kutoka kwenu. Kwani wageni hawa kwa namna moja ama nyengine tunawapokea na kuishi nao kwenye maeneo yetu. Hivyo ni vyema kutoa taarifa kwetu ili waingie na kuishi kwa mujibu wa Sheria na Taratibu za Uhamiaji. “Tukifanya hivyo tutakuwa tumetimiza wajibu wetu – Mlinda Nchi ni Mwananchi” alisisitiza Kamishna Sururu.


Kwa upande wao Masheha hao waliiomba Idara ya Uhamiaji kuendelea kutoa Elimu kwani huwasaidia kukumbushana na kujenga uelewa wa pamoja katika kusimamia suala hilo nyeti kwa Ulinzi na Usalama wa Nchi na watu wake. Akijibu hoja hiyo Kamishna Sururu alisema, “Idara itaendelea kutoa Elimu kwa Masheha na wanachi wa maeneo yote, huku akiwahimiza kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa za wageni kwa Idara ya Uhamiaji ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia na kudhibiti Uingiaji na Utokaji wa watu Nchini. Tumeanza na Mkoa wa Kusini na Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, na sasa tunajipanga kuendelea na kutoa semina hizo kwa Mikoa yote hapa Kisiwani Pemba”.

Mwishoni mwa ziara hiyo, Mkuu wa Diko “Bandari Bubu” ya Shumba Mjini Bwana Hussein R. Omar, kwa niaba ya manahodha wenzake alioomba Idara ya Uhamiaji kusukuma mbele juhudi za Serikali katika kurasimisha Bandari hiyo. Wakitilia mkazo faida zitakazopatikana kutokana na kuwepo kwa Bandari katika eneo hilo la ukanda wa Micheweni, kupakana kwa karibu zaidi na eneo la Shimoni, Mombasa, Kenya ambapo wakaazi wa maeneo hayo wamekuwa na muingiliano mkubwa wa kijamii na kibiashara.

Kamishna Sururu aliwataka Wananchi hao wa Shumba Mjini kuzingatia Sheria na Kanuni pale wanapotaka kuondoka na kurudi Nchini, kwani hali hiyo hupelekea ongezeko la Uhamiaji usiofata Sheria Visiwani Zanzibar. Sambamba na hilo aliwaasa wananchi hao kutobeza juhudi mbali mbali zinazochuliwa na Idara yake na Serikali kwa ujumla, katika kutatua changamoto kubwa katika suala zima la udhibiti wa Uingiaji na Utokaji wa Watu baina ya nchi mbili hizo.    

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.