Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein Awaapisha Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akimuapisha Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Lulu Msham Abdallah, hafla hiyo imefanyika Ikulu Zanzibar leo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  leo amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hafla hiyo, ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ambapo viongozi walioapishwa ni Lulu Mshamu Abdalla kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Joseph Abdalla Meza kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB).
Dk. Shein amewaapisha Makatibu Wakuu ambao ni Ali Khalil Mirza kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Omar Hassan Omar aliapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Idrissa Muslim Hija ameapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Pia, Dk. Shein amemuapisha Khadija Bakari Juma kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Juma Ali Juma ameapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda,

Aidha, Dk. Shein amemuapisha Maryam Juma Abdalla Saadalla kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Shaaban Seif Mohamed kuwa Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

Kwa upande wa Naibu Makatibu Wakuu, walioapishwa ni Tahir Mohammed Khamis Abdulla kuwa Naibu Katibu Mkuu katika   Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Ali Khamis Juma kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda, Ahmad Kassim Haji kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.

Pia, Dk. Shein amemuapisha Dk. Amina Ameir Issa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale anaeshughulikia masuala ya Utalii na Mambo ya Kale, Mwanajuma Majid Abdulla ameapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto anaeshughulikia masuala ya Wazee, Wanawake na Watoto.

Wengine ni Maua Makame Rajab ameapishwa kuwa Naibu katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wanawake na Watoto anaeshughulikia masuala ya Kazi na Uwezeshaji, Amour Hamil Bakari kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Dk. Saleh Yussuf Mnemo kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale anayeshughulikia masuala ya habari.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar  Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri na Manaibu Mawaziri.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Mkuu wa  Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih,Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Washauri wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Nao viongozi hao walioapishwa waliahidi kuendelea kumsaidia Rais Dk. Shein katika kuhakikisha Zanzibar inazidi kupata maendeleo endelevu na kusisitiza ushirikiano katika utendaji wa kazi ili malengo yote yaliokusudiwa yaweze kufikiwa ikiwa ni pamoja na kuwatumikia wananchi na kuwasogezea huduma zote muhimu za kijamii.

Kufuatia mabadiliko ya Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliofanyika hivi karibuni, Rais Dk. Shein alifanya uteuzi na kuwabadilisha wadhifa baadhi ya watendaji wakuu katika taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.