Habari za Punde

Ujenzi wa Viwanja Vya Kisasa Katika Uwanja wa Mao Ukiendelea na Ujenzi huo kwa Hatua ya Kuweka Nyasi Bandia.


Maendeleo ya Ujenzi wa Viwanja vya Kisasa katika eneo la Uwanja wa Zamani wa Mao Zanzibar ukiendelea na ujenzi huo unaofanywa na Kampuni kutoka Nchini China wakiwa katika hatu ya uwekaji wa Nyasi za bandia katika mmoja wa Uwanja huo.Kama inavyoonekana picha wafanyakazi wa kampuni hiyo wakiweka nyasi hizo, baada ya hatua za mwazo.

Harakati za Ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mpirani Kikwajuni Mjini Zanzibar zinaendelea chini ya Wahandisi wa Kampuni ya Kimataifa ya Zhengtai Group ya Jamhuri ya Watu wa China na sasa wanaendelea na zoezi la uwekaji wa nyasi bandia katika uwanja wa Soka.
Mtandao huu umeshuhuidia maendeleo ya uwanja huo yanavyoendelea ambapo kwasasa mafundi hao wanatandaza nyasi bandia huku zoezi hilo likitarajiwa kukamilika muda mchache.
Tayari uwanja huo umeshawekwa Taa ambazo zitasaidia  kuchezwa michezo hadi usiku huku baadhi ya vifaa vyengine vinazidi kutoa sura mpya ya kukamilika kwa ujenzi huo kadri ya siku zinavyokwenda.
Ujenzi wa uwanja huo unafuatia msaada mkubwa ulioidhinishwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika azma ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa pande hizo mbili ukizingatia heshima uliopewa Uwanja huo wa kuitwa jina la Muasisi wa Taifa la China Hayati Mao Tse Tung.
Uwanja huo utakuwa na Viwanja viwili vya mpira wa miguu na chengine cha Mpira wa Kikapu, Mpira wa Mikono, Mpira wa Pete na na michezo mengine ya ndani kama vile Mpira wa Meza pamoja na sehemu ya kufanyia mazoezi ya kuinua vitu vizito.
Katika Viwanja hivyo vya Mpira wa Miguu uwanja mmoja utakuwepo upande wa Magharibi ambao utakuwa na Jukwaa moja litakalochukuwa Mashabiki 1500 waliokaa.
Uwanja mwengine wa mpira wa miguu utakuwepo upande wa Mashariki ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua Mashabiki waliokaa 900 katika jukwaa moja ambalo litakuwepo katika Uwanja huo.

Uwanja huo utagharimu Shilingi Bilioni 12.5 kwa fedha za Tanzania ambapo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China itatoa Shilingi Bilioni 11.5 huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachangia zaidi ya Shilingi Bilioni 1 kati ya hizo Bilioni 12.5 ambazo watalipwa Wakandarasi wa uwanja huo ambao ni Kampuni ya Zhengtar Group Company Limited ambayo ina uzoefu mkubwa wa kujenga Viwanja wa Michezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.