Habari za Punde

Zanzibar yeteketeza Nyama kutoka Afrika Kusini kuepuka Maradhi ya LISTERIA

 Nyama kutoka Afrika ya kusini zilizoingizwa Zanzibar kinyume na sheria na Kampuni ya Qamar zikiwa zimewekwa katika Maboksi kabla ya kuteketezwa huko Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja
 Mkuu wa Jiko la kuteketezea bidhaa mbovu Khamis wa Khamis Mkanga akiziingiza nyama katika jiko hilo kwa ajili ya kuteketezwa baada ya kuingizwa nchini kinyume na sheria kutoka Afria ya Kusini.
 Nyama kutoka Afrika ya kusini zilizoingizwa Zanzibar kinyume na sheria na Kampuni ya Qamar zikiwa zimeingizwa katika Jiko tayari kwa kuteketezwa huko Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja
 Jiko lililotumika kuteketeza Nyama hizo huko Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja
 Jiko lililotumika kuteketeza Nyama hizo huko Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja
 Mkuu wa kitengo cha Uchambuzi wa hatari zinazotokana na Chakula kutoka Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar ZFDA Aisha Suleiman Akizungumza na Wandishi wa habari mara baada ya zoezi la kuteketeza  nyama zilizoingizwa nchini kinyume na Sheria na Kampuni ya Qamar ya Jijini Dar es Salaam kutoka Afrika ya Kusini
Mkaguzi wa bidhaa za Chakula hususan Nyama Daktari Othman Juma Othman akielezea ugonjwa wa Listeria na madhara yake mara baada ya zoezi la kuteketeza nyama kufanyika.
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 14.03.2018
Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar ZFDA umeteketeza kwa moto kilo 48 za Nyama kutoka Afrika Kusini ambazo ziliingizwa nchini kinyume na sheria.
Nyama hizo zilizokuwa mali ya Kampuni ya Qamar ya Vingunguti jijini Dar es Salaam zilikamatwa Uwanjwa wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza katika zoezi hilo Mkuu wa kitengo cha Uchambuzi wa hatari zinazotokana na Chakula Aisha Suleiman amesema kilichosababisha kuteketezwa kwa nyama hizo ni katazo lililotolewa na ZFDA yenye majukumu ya kuhakikisha wananchi wanapata Chakula na Dawa zilizokuwa salama.
Amesema maamuzi ya katazo hilo yametokana na uwepo wa maradhi ya mripuko ya Listeria nchini Afrika Kusini hivyo Ofisi yao ikapiga marufuku uingizwaji wa Nyama, Maziwa na Samaki kutoka nchi hiyo.
Amesema katazo hilo si kwa Zanzibar pekee bali pia Tanzania bara na nchi nyingine kutokana na utaratibu wa biashara kimataifa.
“Hili katazo siyo sisi tu ni utaratibu wa Kimataifa kwamba kutokana na Maradhi ya Listeria bidhaa za Nyama, Samaki, Maziwa ni marufuku kuingizwa nchini sasa hii Kampuni ya Qamar LTD ya Dar es Salaam wao waliamua kuingiza nyama hizo kwa hiyo tumezikamata na kuziangamaza.” Alisema Aisha.
Hivyo kwa lengo la kulinda wananchi wasipate matatizo wameamua kuitekekeza Nyama hiyo huko maeneo ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Ametoa wito kwa Wafanyabiashara kufuata taratibu zilizowekwa kisheria na kufuatilia taarifa zinazotolewa na Wakala wa Chakula na Dawa ili kuhakikisha wanaingiza bidhaa salama kwa afya ya Wananchi wa Zanzibar.
Aidha amewaomba kufuatilia vyema taarifa za utandawazi ili kujua kinachoendelea Duniani.
Akielezea hatua zilizochukuliwa kwa Kampuni hiyo iliyoingiza nyama hizo amesema Kampuni imelazimishwa kulipia ngamarama zote za uteketezaji wa nyama hiyo na asilimia tano ya uingizaji wa bidhaa hiyo.
Kwa upande wake Mkaguzi wa bidhaa za Chakula hususan Nyama Daktari Othman Juma Othman akielezea ugonjwa wa Listeria amesema ugonjwa wa maambukizi unaosababishwa zaidi na Vimelea vya Bakteria ambapo hupatikana kwa kula vyakula vilivyoshambuliwa na Bakeria hao.
Ugonjwa huo wa mripuko huwaathiri zaidi Watoto na watu wazima ambao afya na kinga za mwili zimetetereka.
Aidha Mama wajawazito ni miongoni mwa waathika wakubwa wa ugonjwa huo na kuwasababishia kuharibu mimba zao pale ambapo utaingia nchini.
Nchini Afrika kusini Ungonjwa wa Listeria uligundulika rasmi mwezi November mwaka jana ambapo tayari umesababisha vifo vya zaidi ya watu 180.
Hivi karibuni Wakala wa Chkula na Dawa Zanzibar ZFDA ulikabidhiwa rasmi Cheti cha mfumo wa uhakikiki ubora wa huduma cha kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015 ikiwa ni kielelezo cha taasisi hiyo kusimamia misingi imara ya kuhakiki ubira wa huduma katika kiwango cha kimataifa.
Imetolewa na Maelezo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.