Habari za Punde

Ikulu yaiadhibu RAS Iringa kwa kuwachapa magoli 49-8

 Kipa wa timu ya Uchukuzi, Willy Barton jana akidaka mpira katika mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye uwanja wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa wakiajiandaa na mechi za mashindano ya Kombe la Mei Mosi yanayofanyika kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa
Mchezaji  Sharifa Hamis (kulia) akifanya mazoezi ya kucheza bao na Ambakisye Mwasunga (kushoto) wakifanya mazoezi ya kujiandaa na michuano ya Mei Mosi kwa upande wa michezo ya jadi inayofanyika kwenye uwanja wa Somora mkoani Iringa. Katikati ni mchezaji wa mchezo wa draft Bw. Omar Said akiangalia
Beki Nestory Tweve (3) wa timu ya Tumbaku ya Morogoro akitafuta njia ya kuwapita Francis Singa na Abdul Kawamba (wenye jezi nyeusi) wa RAS Iringa, katika mchezo wa mashindano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Samora. Tumbaku walishinda magoli 3-0
 Mfungaji Fatuma Machenga (GS) wa Ikulu akifunga mbele ya mlinzi wa RAS Iringa (GK), Maria Mwita katika mchezo wa netiboli wa mashindano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCO) Iringa. Ikulu wameshinda magoli 49-8.
Mlinzi wa pembeni Ester Turuka (WA) wa RAS Iringa akirusha mpira kwa mfungaji wao Warda Sapal (GS) huku mlinzi Lilian Sylidion (GD) wa Ikulu akijitahidi kuzuia katika mchezo wa netiboli wa mashindano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCO) Iringa. Ikulu wameshinda magoli 49-8.   


Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
TIMU ya Ofisi ya Rais Ikulu imewachapa bila huruma wenyeji RAS Iringa kwa kuwafunga magoli 49-8 katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCO) mkoani Iringa.
Ikulu inayofundishwa na kocha mzoefu Mary Protas ambapo wafungaji wake Fatuma Machenga aliibeba timu yake kwa kufunga magoli 48 huku Irene Elias alifunga bao moja pekee. Magoli ya RAS Iringa yamefungwa na Warda Sapal na Zitaamanzia Kididi kila mmoja manne. 
Katika mchezo wa soka timu ya RAS Iringa ilifungwa na Tumbaku ya Morogoro kwa magoli 3-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja w Samora.
Washindi walipata bao lao la kwanza kupitia kwa Ramadhani Shegodo aliyefunga dakika ya tisa baada ya kupata pasi kutoka kwa Mohamed Mtawal; huku bao la pili lilipatikana dakika ya 29 kwa shuti  kali la Ushindi Nzogela.
Bao la tatu lilifungwa na Salum Idd katika dakika 52 baada ya kupiga krosi murua iliyomshinda kipa Mashaka Peter aliyejikuta akiusindikiza mpira langoni mwake.
Hatahivyo, Tumbaku itabidi wajilaumu kwa kukosa magoli mengi ya wazi, ikiwemo dakika ya 20 mshambuliaji wake Issa Simbaliana kukosa penalti  iliyotolewa na mwamuzi Steven Makuka baada ya Nzogele kuchezewa rafu na Dickson Kiboye wa RAS Iringa, lakini kwa kupaisha mpira juu ya goli,
Timu za mchezo wa netiboli zitacheza kwa mtindo wa ligi kutokana na kuwa tano, ambazo ni Uchukuzi, Ikulu, Hifadhi ya Ngorongoro, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na RAS Iringa, ambapo bingwa atapatikana kwa wingi wa pointi na magoli ya kufunga.
Kwa upande wa soka timu zimegawanywa katika makundi mawili, ambapo kundi ‘A’ linaundwa RAS Iringa, Tumbaku, Tanesco na Hifadhi ya Ngorongoro, huku kundi ‘B’ zipo Geita Gold Mine (GGM), Uchukuzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAO).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.