Habari za Punde

UZINDUZI WA KAMATI YA PAMOJA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA HATI YA MAKUBALIANO KATI YA ZFDA NA TFDA.

WAZIRI wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizindua Kamati ya Pamoja ya kusimamia hati ya makubaliano kati ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania  Bara ( TFDA) katika Ofisi za ZFDA ziliopo Mombasa Mjini Zanzibar.
MKURUGENZI  wa ZFDA Dkt. Burhan Othman Simai akizungumza  na kuitambulisha kamati ya kusimamia utekelezaji wa hati ya makubaliano kati ya ZFDA na TFDA) katika Ofisi za ZFDA ziliopo Mombasa Mjini Zanzibar.
KAIMU Mkurugenzi TFDA Bi. Agnes  Kijo akitoa maelezo kuhusu mashirikiano na majukumu ya Kamati ya pamoja ya kusimamia hati ya makubaliano kati ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar  na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania katika ukumbi wa ZFDA ulioko Mombasa Mjini Zanzibar.
WAJUMBE wa Kamati ya pamoja ya kusimamia utekelezaji wa hati ya makubaliano  upande wa  Zanzibar.
WAJUMBE wa Kamati ya pamoja ya kusimamia utekelezaji wa hati ya makubaliano  upande wa  Tanzania Bara.
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Hati ya makubaliano ya pamoja kati ya ZFDA na TFDA (Picha na Abdalla Omari Maelezo – Zanzibar).
Na Ramadhan Ali.-Maelezo Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed ameishauri Kamati ya pamoja ya kuratibu utekelezaji wa hati ya makubaliano kati ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Tanzania Bara  (TFDA) kumaliza matatizo wanayowakabili wafanyabiashara wakati wa kusafirisha bidhaa kutoka upande mmoja wa  Muungano.
Waziri Hamad Rashid ameitoa ushauri huo alipokuwa akizindua Kamati hiyo ya wataalamu yenye wajumbe wanne kila upande katika Ofisi ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar zilizopo Mombasa Mjini Zanzibar.
Ameitaka Kamati hiyo  kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa  ili kuhakikisha taratibu za kusafirisha bidhaa za chakula na dawa zinakubalika na pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri wa Afya ameishauri Kamati kuhakikisha inasimamia na kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia  nchini kwa lengo la kuwawezesha watanzania kupata huduma bora za chakula na dawa.
Aidha alielekeza udhibiti huo uendane na utoaji wa elimu ya matumizi bora ya bidhaa hizo na madhara yanayoweza kutokea kwa kutumia bidhaa zilizochini ya viwango, hasa kwa wanafunzi ambao watakuwa walimu watapoanza maisha ya kifamilia.
Hata hivyo Waziri Hamada Rashid ameishauri Kamati  kusimamia pia Taasisi za Serikali zinazoagiza bidhaa kutoka nje kwani  baadhi ya taasisi hizo zinaagiza bidhaa ambazo muda wake wa matumizi unakaribia kumalizika .
Kaimu Mkurugenzi wa TFDA Bi. Agnes Kijo amesema lengo kubwa la Kamati ya pamoja ya Taasisi hizo mbili ni udhibiti wa usalama wa chakula na vipodozi baina ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza ambazo huongeza gharama za usafirishaji.
“Tunatambua kwamba kumekuwepo changamoto katika uingizwaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi  kutoka upande mmoja kwenda mwengine kutokana na sheria za udhibiti wa bidhaa hizo kwa pande hizi mbili kuwa tofauti, ”alisema Bi Agnes.
Alieleza baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa na taasisi hizo mbili kuwa ni kutambua  na kuzikubali hati za usajili zinazotolewa na moja ya taasisis hizo na  kuruhusu uingizwaji Tanzania Bara bila kuhitaji kibali cha TFDA kwa bidhaa za chakula na dawa zilizozalishwa na viwanda vya Zanzibar.
Bi. Agnes ameyataja makubaliano mengine  kuwa ni kufanya ukaguzi wa pamoja kwa viwanda vya kuzalisha bidhaa za chakula na vipodozi ili kujiridhisha juu ya uzingatiaji wa mifumo bora ya uzalishaji na kushirikiana katika kufanya tathmini ya pamoja ya bidhaa za chakula na dawa  kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa hizo kwa watumiaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar Dkt. Burhani Othaman amewataka wafanyabiashara wa Zanzibar wanaosafirisha bidhaa za chakula na dawa kupeleka Tanzania Bara kwenda ofisini kwao kujisajili ili kupatiwa hati rasmi za kusafirishia bidhaa hizo ili kuepuka  usumbufu wanapofika bandari ya Dar es salaam.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.