Habari za Punde

Waziri wa Maji Kamwelwe Atahadharisha Kuwafukuza Wahandisi

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isaack Kamwelwe akikagua chanzo cha maji Itaka katika halmashauri ya Mbozi pamoja na wataalamu wengine kutoka ngazi ya mkoa na wilaya.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isaack Kamwelwe akisisitiza jambo kwa wataalamu alipotembelea mradi wa maji Iyula halmashauri ya Mbozi, kushoto kwake ni Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya maji Mkoa wa Songwe Mhandisi Tanu Deule.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isaack Kamwelwe ametahadharisha kuwafukuza kazi na kuwashitaki wahandisi wa serikali wanaokosa uzalendo na kuhujumu miradi ya maji katika hatua ya usanifu na usimamizi kwa kupitisha vifaa vilivyo chini ya viwango.
Mhandisi Kamwelwe ametoa tahadhari hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Songwe ya kukagua utekelezaji wa miradi mitatu ya maji ya Iyula na Itaka katika halmashauri ya Mbozi, mradi wa Umwagiliaji Naming’ongo katika halmashauri ya Momba na mradi wa Maji Tunduma katika halmasahuri ya Tunduma.
“Miradi mingi inakamilika na kuzinduliwa na viongozi wakubwa wa kitaifa lakini mabomba yanaanza kupasuka muda mfupi tu baada ya wananchi kuanza kupata maji kwakuwa hayana viwango, wahandisi badilikeni na hili likitokea hauna ajira na kushitakiwa juu”, amesisitiza Kamwelwe.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa miradi ya maji hakutakuwa na tija endapo shughuli za utafiti wa vyanzo vingine imara vya maji hazitafanyika pamoja na kutunza vyanzo vya maji vilivyopo kwa ajili ya uendelevu wa miradi hiyo kwa muda mrefu.
“Hatutaki kusikia mradi unatoa maji kwa muda mfupi kisha maji yanaisha kwenye vyanzo, hivyo naagiza taasisi ya bonde la ziwa Rukwa washirikiane na taasisi nyingine pamoja na ofisi za wakuu wa wilaya kutafuta vyanzo vingine vya maji pamoja na ulinzi wa vyanzo vilivyopo”, amebainisha Mhandisi Kamwelwe.
Kwa Upande wao wananchi wameiomba serikali kuwepo kwa uwazi na ushirikishwaji katika hatua zote za ujenzi wa miradi tangu hatua ya usanifu ili kujenga uelewa juu ya miradi hiyo na kuondoa migogoro.
Ujenzi wa miradi ya maji ya Iyula, Itaka na Tunduma inatarajiwa kutoa huduma ya maji kwa wananchi takribani laki moja ambao watakuwa wanapata maji kwa umbali usiozidi mita 400 sawa na mwongozo wa sera ya maji ya mwaka 2002.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.