Habari za Punde

Chuo cha Madini Chapewa Siku Saba Kuwasilisha Ripoti ya Utatuzi wa Changamoto

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ametoa siku saba kwa Chuo cha Madini kuwasilisha ripoti  ya namna watakavyotatua changamoto zilizopo chuoni hapo ili kuboresha elimu katika chuo hicho.
Waziri Kairuki ametoa agizo hilo jana jijini Dodoma wakati wa maadhisho ya Siku ya Madini yaliyofanyika chuoni hapo ambapo wanafunzi walipata wasaa wa kuzungumzia changamoto zao mbele ya Waziri huyo.
Waziri Kairuki amesema kuwa chuo hicho kimekua chuo bora kwa kuendesha mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vijana nchini kwa sababu inajulikana kuwa kufundishwa kwa njia ya vitendo ni msingi mzuri kwa taaluma yoyote hasa kwa wakati huu ambao nchi imekua na mabadiliko ya haraka.
“Nyinyi kama Chuo cha Madini mna mchango mkubwa katika kuufikia uchumi wa viwanda na ili kuhakikisha tunaweza kuchangia katika uchumi huo lazima changamoto zinazojitokeza chuoni hapa zitatuliwe, hivyo natoa wiki moja kwa uongozi wa chuo kuleta taarifa itakayoonesha utatuzi wa changamoto za chuo chetu,’alisema Waziri Kairuki.
Waziri ameongeza kuwa ni vema uongozi wa chuo pamoja na walimu kuhakikisha wanafata misingi ya taaluma inayotolewa na chuo hicho ili vijana hao waweze kuwa na ushindani katika soko la ajira kwani wanafunzi wameonesha moyo wa uvumilivu na uzalendo katika kuhakikisha chuo hicho kinatimiza malengo yake.
Kuhusu upungufu wa miundombinu ya chuo, Waziri amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/19, wizara imetenga fedha kwa ajili ya kujenga jengo jipya la taaluma litakalokua na vyumba vya mihadhara vitakavyokuwa na uwezo wa kubeba watu 200, ofisi za kisasa za wakufunzi pamoja na ukumbi wa mikutano.  
Aidha, kwa kuwa wizara imejipanga kuongeza kiwango cha wanafunzi kwa kudahili wanafunzi wapya 850 na mabweni yaliyopo sasa yanaweza kuchukua wanafunzi 264 pekee ni lazima mabweni mapya yajengwe.          
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Eliah Mwita amesema kuwa chuo hicho ni cha pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kutoa wataalam wenye uwezo wa kufanya kazi katika sekta ya madini kwani wamebobea katika fani za utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
“Ingawa chuo kinatoa wataalam wabobezi wa shughuli za madini lakini tuna changamoto nyingi zinazorudisha nyuma maendeleo yetu zikiwemo za ubovu wa vyoo na miundombinu ya maji, uchache wa mabweni, huduma mbovu za afya, ucheleweshaji wa mafunzo kwa vitendo pamoja na kukosekana kwa vifaa vya kufundishia hivyo tunaleta kwako waziri utusaidie kuyatatua,”alisema Mwita.
Kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Mwita amemuomba Waziri wa Madini kuwapatia mikopo ya kujikimu wakiwa chuoni, kuwatafutia wafadhili wa masomo nje ya nchi ili waweze kujiendeleza katika fani zao, kununua vifaa vya mafunzo kwa vitendo pamoja na kuwakumbuka katika nafasi za ajira.


Maadhimisho hayo yalishirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wa Benki ya CRDB na Mfuko wa Pensheni wa LAPF.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.