Habari za Punde

James Mwangi: Huyu ndiye mtu anayevalia nadhifu zaidi Afrika

Unamiliki suti ngapi, viatu jozi ngapi, kofia ngapi, mashati mangapi na mikanda mingapi na soksi pea ngapi? Ukihesabu bila shaka hautakosa kugundua kuwa ni mavazi ya kukuwezesha kusukuma wiki moja au mbili hivi bila kurudia.
Lakini kwa mwanamume mmoja mwenye makao yake jijini Nairobi, Kenya hilo si tatizo.
Ana mavazi mengi ajabu, yanayojumlisha suti kamili za rangi tofauti, viatu, kofia, mikanda, saa, pete na hata mifuko ya simu, mavazi ambayo anaweza kuyavaa kwa zaidi ya siku mia moja bila kurudia.
Kila ukikutana naye kwenye mkusanyiko wa watu, hutakosa kumtambua kutokana na mtindo wake wa kipekee wa kuvalia.
 James Maina Mwangi ni mzaliwa wa Muranga kati kati mwa Kenya anasema aliondoka nyumbani kwao na kuelekelea jijini Nairobi kutafuta riziki akiwa na umri wa miaka 12 baada ya kusoma hadi darasa la sita.

Anasema alipata changamoto kubwa za kuweza kupata mavazi ya kutosheleza haja yake, hasa utotoni.
"Nikiwa mdogo nilikuwa na shati moja tu nililokuwa nikilivua likikauka ninalivaa tena, na kuna wakati nilikuwa nikiazima nguo kutoka kwa marafiki kama ninataka kwenda kutembea mahali, nikimuomba rafiki ananijibu vibaya labda ananitusi au ananicheka," anasema.
"Ndipo nikamuomba Mungu anipe taji ambayo watu wengine hawana, ndio wajue kuna Mungu tofauti na yule walikuwa wanamjua," anasema Mwangi
Hadi sasa Bw Mwangi anasema anamiliki zaidi ya suti 150, zaidi ya jozi 200 za viatu na kofia zaidi ya 300 mavazi ambayo amekuwa akiyanunua nchini Kenya na kuagiza mengine kutoka nchini za kigeni zikiwemo Afrika Kusini, Italia, Uhispania, Ufaransa na Ujerumani.
Anasema anamiliki suti za kila rangi inayopatikana duniani na huwa kawaida anavaa rangi moja kuanzia kofia, miwani, shati, tai, suti yenyewe, viatu ,soksi saa, rangi ya simu na hata nguo za ndani.
Mwangi anesema suti moja inaweza kumgharimu kati ya shilingi 10,000 pesa za Kenya au dola 100 na shilingi 80,000 au dola 800.
"Mimi ni kama kioo kwa wananchi, watu wakiniona nimevaa hivi hufurahi sana, wao hunisimamisha, hunisalimia na kuzungumza nami na kunipa moyo kuendelea kuvaa hivi, na pia kuniombea mema, nafikiri ni mimi ndiye mtu maridadi zaidi Afrika," Bw Mwangi anasema.

Anasema kuwa kuvaa nadhifu lilikuwa ni ombi alilomuomba Mungu tangu utotoni na anasema kuwa atazidi kuvalia hivyo hadi ile miaka Mungu atamruhusu kuishi ulimwengu huu.Kando na mavazi ambayo yemechangia Bw Mwangi kujulikana sehemu tofauti duniani, amekuwa pia kiongozi wa vijana katika miradi mbali mbali ambayo imewasaidia vijana tangu mwaka 1993.
Amesema ameongoza kuanzishwa kwa miradi ya vijana tangu uongozi wa rais mstaafu Daniel arap Moi, ikiwemo ya uchukuzi wa mijini maarufu kama 'matatu' iliyowaajiri vijana wengi. Amechangia pia miradi mingine ya kuosha magari.
Bw Mwangi pia anasema alipendekeza kuanzishwa kwa miradi ya ujenzi wa masoko sehemu tofatu za nchi likiwemo soko maarufu la Muthurwa lililo mjini Nairobi, na pia mradi wa umeme ambao uliwawezesha watu kupata umeme sehemu za mashambani maarufu kama Rural Eletrification Project wakati wa utawala wa rais mstaafu Mwai Kibaki.

"Nilipendekeza kuwepo miradi ya kujengwa barabara za mashambani na hadi sasa miradi hii imewaajiri vijana na vijana wako na kazi."
Mwangi anatoa ushauri kwa yeyote ambaye angependa kuiga mfano wake kumheshimu Mungu Kwanza.
"Ukimheshimu Mungu na kufanya yanayostahili, Mungu atakuinua na kukupa taji kushinda watu wengine na utakuwa mfano na kielelezo kwa dunia."
Changamoto ambazo Mwangi anasema anakumbana nazo ni kuweza kupata mavazi ya rangi sawa kwa wakati mmoja.
"Mara nyingi inachukua muda mrefu kuweza kupata mavazi yote kwa pamoja kwa sababu ninaweza kupata suti na kofia lakini viatu viwe vimechelewa kutokana na kukosekana kwa rangi ifaayo, kwa hivyo inanilazimu kusubiri muda mrefu." anasema
Kuna tofauti kati ya mtindo wa kuvaa wa Mwangi na ule wa Sapewa Afrika ya Kati?

Bw Mwangi anasema kuwa hajaiga mtindo wa kimavazi maarufu sana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na maeneo ya Afrika ya Kati kwa jina Sape.
Mambo yalibadilika nchini DRC muda mfupi baada ya uhuru na wakati Joseph Mobutu alichukua uongozi, alibadilisha jina la nchi hiyo na kuiita Zaire na kuanzisha mtindo wa mavazi usio ule wa nchi magharibi.

Hata hivyo mwanamuziki Papa Wemba alionekana kulipinga hilo lakini si kupitia kwa muziki.
Kwa hivyo alibuni mtindo wa kuvaa unaofahamika hadi sasa kama Sepe unaomaanisha jamii ya watu nadhifu au wa kupendeza.

Kwa kuvisha bendi yake mavazi ya mtindo wa Sape watu nchini DRC nao wakaufuata mtindo huo.
Anasema watu umpongeza sana na kumpa motishaHaki miliki ya pichaJAMES MWANGI
Image captionAnasema watu umpongeza sana na kumpa motisha
Watu wapenda mavazi ya madaha DRC
Tangu wakati huo na kutokana na vile mtindo huo umewapa watu uhuru wa kujieleza, umewavutia wafuasi wengi eneo la Afrika ya kati na hata mbali.
Hata gari pia huifananishaHaki miliki ya pichaJAMES MWANGI
Image captionHata gari pia huifananisha
Mtindo wa Sapeur kwa sehemu fulani ni kama utamaduni na kwa sehemu kubwa ni wa kuonyesha mavazi hasa yale ya nembo maarufu na ghali kutoka nchi za ng'ambo na wale wanaovaa mtindo huo hawatili sana maanani kulinganishwa kwa rangi mavazi yote kama suti, kofia na hata viatu.
Basi tofauti iliyowazi katika mtindo na Sape na wa Mwangi ni kwama Mwangi hujaribu kwa vyovyote vile kulinganisha kwa rangi mavazi yake yote yaliyo kwenye mwili wake kwa wakati mmoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.