Habari za Punde

Sababu 3 zinazoweza kuifanya migahawa kuhimili ushindani

Na Jumia Food Tanzania
Mabadiliko tofauti ya kijamii na kiuchumi yamechangia kwa kiasi kikubwa kubadilika kwa mifumo ya maisha ya kila siku. Mabadiliko hayo ni pamoja na namna watu wanavyoishi ikiwemo vyakula wanavyokula. Hakuna ubishi kuwa huduma ya chakula ni miongoni mwa sekta kubwa na yenye kuingiza mapato mengi duniani. Hakuna kiumbe yeyote anayeweza kuisha bila ya kula hivyo kupelekea biashara kama migahawa kuzidi kushamiri na kuongezeka. McDonald, Marrybrown, Subway na KFC ni mojawapo ya migahawa mikubwa iliyosambaa sehemu mbalimbali duniani ikiwemo hapa Tanzania.   
Zipo sababu kadhaa ambazo zimepelekea mabadiliko kwenye huduma ya chakula. Kwanza, kuongezeka kukua kwa watu wa daraja la kati, wafanyakazi, wenye uwezo wa kutumia. Watu wa daraja hili mara nyingi huwa hawana muda wa kupika hivyo kutegemea kununua chakula kutoka migahawani. Pili, kukua kwa kipato kwenye familia hivyo kumudu gharama ya kupata huduma ya chakula nje ya nyumba. Sababu ya tatu ni pamoja na kukua kwa maboresho katika huduma za utoaji wa chakula kama vile migahawa ambapo inaongezeka kwa kasi huku ikirahisisha namna ya upatikanaji wa huduma zao.

Kwa hiyo, kiwango cha ushindani kwenye sekta ya huduma ya migahawa ni kikubwa kwa sasa ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Jumia Food inashauri kuwa ili migahawa iweze kufanikiwa kwenye shughuli zao inabidi kuzingatia mambo yafuatayo.       
Utofauti kwenye utoaji huduma. Kwa sasa ambapo soko la huduma ya chakula lina ushindani mkubwa, migahawa inapaswa kuwa na zaidi ya huduma ya chakula au gharama nafuu. Utofauti na upekee katika utoaji huduma unahitajika kwa kiasi kikubwa kwa sasa. Lakini utofauti siyo kitu rahisi. Inahitaji migahawa kuangazia nyanja zote za kuwahudumia wateja kama vile: thamani ya huduma ambayo mteja anaipata, orodha ya vyakula vinavyopatikana, ubora wa huduma, mameneja pamoja na wafanyakazi, lazima vyote hivi viende sambamba.    
Motisha na ushirikishwaji wafanyakazi. Migahawa mingi mikubwa na yenye majina imegundua kuwa na programu za mikakati inayowahusisha wafanyakazi ndiyo misingi ya kuwajua na kuwapatia wateja utofauti wa huduma, kujenga uaminifu, na kukuza soko lao. Wafanyakazi ambao wanapewa motisha na kushirikishwa wana fursa kubwa ya kumpatia mteja huduma bora - kuanzia mteja anapokaribishwa mgahawani, kupeleka huduma kwa wateja wanaoagiza, pamoja na uharaka na namna chakula kinavyoandaliwa na kuhudumiwa. Tafiti kadhaa zinaonyesha kuwa wafanyakazi wanaoshirikishwa na kupewa motisha katika migahawa wanayoifanyia kazi hutoa huduma bora zaidi kwa wateja wao.  

Uwekezaji kwenye huduma ya kuagiza chakula. Teknolojia zinazowawezesha wateja kuagiza chakula na kupelekewa mpaka walipo zimepelekea wateja kujua namna na muda gani chakula kitawafikia. Kwa baadhi ya migahawa, kuamua kushirikiana na mawakala wa nje kuna maanisha kujitangaza zaidi na kuongezeka kwa uhitaji wa huduma. Kwa wengine, ni kupoteza fursa ya kukutana moja kwa moja na wateja wao, kuelewa machaguo yao, na kujenga mahusiano bora zaidi - ukiachilia mbali kupoteza mapato. Wamiliki wa migahawa hawana budi kulitazama suala hili kwa jicho la tatu ili kuleta ustawi kwenye biashara zao.
Kwa kuhitimisha, sekta ya huduma ya chakula inakua kwa kasi nchini Tanzania ambapo tunashuhudia migahawa mashuhuri duniani ikifungua matawi yake. Kutokana na idadi kuongezeka, ushindani nao umekuwa mkubwa. Migahawa inayochipukia imekuwa tishio kwa mikubwa iliyopo na yenye jina kwenye sekta. Hii ni kwa sababu yenyewe inakuja ikiwa imejizatiti zaidi katika ubora wa huduma, teknolojia, aina ya vyakula ilivyonavyo pamoja na namna ya utoaji wa huduma kwa urahisi na haraka. Hivyo basi, kuwekeza nguvu kwenye uvumbuzi na fursa mbalimbali kuna umuhimu mkubwa.      

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.