Habari za Punde

TDB KUIKOPESHA TANZANIA SHILINGI BILIONI 900 KUJENGA RELI YA KATI YA KISASA NA MRADI WA UMEME KILWA

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (katikati) akijadiliana na ugeni wa Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika - TDB (hawamo pichani) kuhusu uboreshaji wa sekta ya nishati ya umeme ili kujenga uchumi wa viwanda.  Kulia ni Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Madeni Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Sauda Msemo.
 Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika –TDB, Bw. Admassu Tadesse (katikati) akitoa ufafanuzi wa mkopo wenye masharti nafuu utakaosaidia ujenzi wa Reli ya Kati ya Kiwango cha Kimataifa(SGR) na nishati ya umeme pamoja na miradi mingine midogomidogo. Kulia ni Mkuu wa Wakala wa Uendeshaji wa Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika –TDB Bi. Neema Siwingwa na kushoto ni Mkurugenzi Mwandamizi wa Masuala ya Kisheria wa Benki hiyo Bw. David Bamlango. 
Ujumbe wa Serikali ya Tanzania (kulia) ukijadiliani na ujumbe wa Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika –TDB (kushoto) namna ya kufadhili ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa -(SGR) na Mradi wa kuzalisha Umeme kwa njia ya Gesi wa Kilwa.
Ujumbe wa Serikali ya Tanzania (kulia) ukijadiliani na ujumbe wa Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika –TDB kwenye picha ya pamoja mara baada ya majadiliano ya namna Benki hiyo itakavyoikopesha Serikali kiasi cha dola milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa pamoja na Ujenzi wa mradi wa Umeme wa Gesi wa Kilwa utakaozalisha megawati 318 za umeme.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (katikati) akiagana na mgeni wake Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara na Maendeleo-Mashariki na Kusini mwa Afrika –TDB Bw. Admassu Tadesse baada ya kumalizika kwa majadiliano yao yaliyolenga Benki hiyo kuikopesha Tanzania mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini katika sekta za miundombinu na nishati. Kushoto ni Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa pili kulia) akifurahia jambo pamoja na Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara na Maendeleo-Mashariki na Kusini mwa Afrika –TDB Bw. Admassu Tadesse wakati  wakiagana mara baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (Trade and Development Bank-TDB), itaikopesha Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 400, sawa na takriban shilingi bilioni 900, kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) na Mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Rais wa Benki hiyo yenye Makao yake Makuu Jijini Nairobi Nchini Kenya, Bw. Admassu Tadesse, alipokutana na kufanya mazungunzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Bw. Tadesse amesema kuwa Benki yake imetenga kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati ya kisasa pamoja na kiasi kingine kama hicho kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa mkoani Lindi.
"Tanzania ni mdau mkubwa wa Benki hii ikiwa inashika nafasi ya 7 kati ya nchi na taasisi 37 zinazomiliki hisa zake ambapo inamiliki hisa asilimia 6.4" alisema Bw. Tadesse.
Bw. Admassu Adesse amesema kuwa hadi machi mwaka 2018, benki yake inatekeleza miradi 11 ya maendeleo nchini Tanzania, katika sekta ya kilimobiashara, huduma za benki na fedha, nishati, ukuzaji miundombinu na viwanda, yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani 284.6 milioni.
"Tuna miradi mingine iliyoidhinishwa na Benki, inayokadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 157 na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 660 ambacho kimepangwa kutolewa kwa Tanzania ili kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za kilimobiashara, ujenzi, kemikali na petroli pamoja na sekta ya nishati" aliongeza Bw. Adesse.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kujiimarisha kimtaji na kiuendeshaji na kwamba Tanzania inapokea kwa mikono miwili ahadi ya Benki hiyo ya kushiriki katika ujenzi wa miradi ya kipaumbele ya Taifa ikiwemo ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) na Mradi wa kuzalisha umeme wa Kilwa, itakayochochea uchumi wa nchi.
Aliahidi kuwa atahakikisha mazungumzo kuhusu upatikanaji wa mkopo huo nafuu yanakamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa ili fedha hizo ziweze kupatikana.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, alisema kuwa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa, utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 318 na utaongeza kiwango cha upatikanaji umeme nchini ambacho hivi sasa kimefikia megawati 1500.
"Lakini pia tuna vijiji 176 vinahitaji umeme ambapo kati yake vijiji 120 viko kwenye visiwa na vinahitaji kupatiwa huduma ya nishati ya umeme na TDB imekubali kusaidia ujenzi wa miradi ya umeme kwa kutumia nguvu ya maji ambapo kila mradi utazalisha megawati 10 za umeme" alisema Dkt. Kalemani
TDB inaundwa na nchi 22 za kiafrika, nchi mbili ambazo si nchi za kiafrika pamoja na taasisi za uwekezaji 13 na kufanya idadi ya nchi na taasisi ambazo ni wana hisa, zinazounda benki hiyo, kufikia 37.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.