Habari za Punde

Wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa mbovu waonywa



WIZARA ya Biashara na Viwanda Zanzibar, imeeleza kuwa haitawavumilia wafanyabiashara wanaokwenda kinyume na matakwa ya sheria za nchi kwa kuingiza nchini bidhaa zisizo na ubora na viwango vinavyohitajika.

Akizindua baraza la biashara la mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hassan Khamis Hafidh, alisema kufanya hivyo kunalenga kulinda afya za watumiaji na kuweka usawa katika ushindani wa biashara nchini.

Alisema historia inaitaja Zanzibar kuwa ni kitovu cha biashara mbali mbali hivyo kuna haja ya wafanyabiashara wa ndani na nje kufanya biashara zao kwa haki na uadilifu ili kulinda jina la kibiashara la Zanzibar.

Alisema katika siku za karibuni kumejitokeza baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoingiza nchini bidhaa hizo hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao iwapo watabainika kufanya udanganyifu au kwenda kinyume na matakwa ya sheria.

“Jambo hili halikubaliki na sisi serikalini tutahakikisha tunatekeleza wajibu wetu wa kusimamia sheria kama ilivyowekwa kwa maslahi ya wananchi wetu na wafanyabiashara waaminifu ili kulinda hadhi ya nchi yetu lakini pia ushindani halali wa kibiashara”, alisema.

Aidha aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuzingatika kikamilifu majukumu yao na azma ya kuundwa kwa mabaraza hayo kwa kuwa serikali inaamini uanzishwaji wake utasaidia kuweka mwenendo mzuri wa biashara na kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto zinazohusiana na biashara.

Alisema kwa mujibu wa sheria na aina ya wajumbe wa baraza hilo ambalo ni la kwanza kuzinduliwa, anaamini litafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki, uadilifu na ushindani na litakua darasa katika kuelekea maendeleo ya biashara na kuongeza kasi ya uchumi wa Zanzibar.

Nae Mwenyekiti wa baraza hilo, Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, akizungumza kwa niaba ya wajumbe wengine, aliahidi kuwa baraza hilo litatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na mashirikano ya karibu na baraza la biashara la taifa ili kuondosha changamoto zilizopo.

“Kiasili mkoa wetu ndio wenye shughuli nyingi za kiuchumi kutokana na miundombinu yote ya biashara kama vile bandari na uwanja wa ndege hivyo baraza letu litajitahidi kufanya kazi kwa karibu na taasisi nyengine ili kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zinazowakabili wananchi wetu,” alieleza.

Akiwasilisha mada juu ya baraza hilo kwa wajumbe wateule na waalikwa wengine, mwanasherika kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Zainab Kibwana, alieleza kuwa mabaraza ya biashara ya mikoa yameundwa kisheria chini kifungu cha 21 cha sheria namba 10 ya baraza la taifa la biashara.

Alisema lengo la kuundwa mabaraza hayo ni pamoja na kuibua, kujadili na kutatua chanagamoto na matatizo yanayoikabili sekta ya biashara na wafanyabiashara ili kuweka kuimarisha mwenendo wa biashara.

“Kwa mujibu wa sheria baraza la biashara la taifa linakutana mara moja kwa mwaka hivyo inakuwa vigumu kuweza kuzishughulikia changamoto zote zinazoibuliwa ndipo ilipoonekana haja ya kuanzisha mabaraza haya ambayo yanatarajiwa kushughulikia kwa kadiri ya uwezo wake hizo changamoto na zile ambazo zitakuwa juu ya uwezo wao ndio zitapelekwa katika baraza la taifa,” alifafanua.

Baraza lililozinduliwa linaundwa na wajumbe 12 ambao ni Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohammed Mahmod, anaekuwa Mwenyekiti, Katibu Tawala wa Mkoa, Hamida Mussa Khamis, anaekuwa Katibu wa baraza na wajumbe 6 wanaowakilisha sekta ya umma na wengine 6 wanaowakilisha sekta binafsi.

Wajumbe wanaotoka katika sekta ya umma na Khamis Suleiman Mwalim, Mohammed Walid Fikirini, Khamis Ahmada Shauri, Miza Herman Mgaza, Yahya Mohammed Shauri na Sharif Ali Sharif wakati wajumbe wanaotoka katika sekta binafsi ni Hassan Ali Mzee, Taufiq Salim Turky, Said Nassir Nassor ‘Bopar’, Mkurugenzi wa kampuni ya CPS-lives Ltd Sebastian Dietzold, Remy Eddington Kisasi na Mwenyekiti wa kundi la kampuni ya Bakhresa, Said Salim Bakhresa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.