Rundo la taka za Plastiki katika moja ya madampo ya Marekani.
Na Ali Shaaban Juma
Katika kipindi cha miaka
Hamsini iliyopita, dunia imeshuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji wa bidhaa za
plastiki. Katika mwaka 2013, jumla ya tani 299 Milioni za plastiki zimezalishwa
duniani ikiwa ni ongezeka la asilimia 4% ikilinganishwa na uzalishaji wa mwaka
2012. Kwa mujibu wa Shirika la Uhifadhi
Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP, (United Nations
Environmental Programme) matumizi ya
plastiki yameongezeka duniani kutoka tani
Milioni 5.5 katika miaka ya 50 hadi tani Milioni 110 Milioni mwaka 2009.
Licha
ya kuongezeka kwa uzalishaji wa plastiki kwa kiwango kikubwa, kiwango cha taka
za plastiki zinazovurugwa kwa matumizi mengine ni madogo kulinga na uzalishaji.
Matumizi ya bidhaa za plastiki yamekuwa yakiongozeka kwa kasi kwa vile bidhaa
hizo zinachukua nafasi ya bidhaa za chuma na kigae zilizotumiwa kabla.
Taka
na uchafu wa plastini “Plastic pollution”
ni mrundikano wa mabaki ya plastiki za aina mbalimbali zinazotokana na
matumizi ya vifaa vilivyotengenezwa kwa bidhaa hiyo ambazo huleta athari mbalimbali kwa viumbe hai, binaadamu na mazingira. Kuna
aina mbalimbali za palastiki ambapo kutokana na gharama ndogo za kutengeneza
bidhaa za palastiki, matumizi ya palastiki yameongezeka sana duniani na kufanya
bidhaa hiyo kuwa ni miongoni mwa vitu vinavyochafua mazingira.
Uchafuzi
wa mazingira kutokana na taka za plastiki huathiri na kuharibu mazingira ya miji,
ardhini, mito, maziwa, mashambani na hata baharini. Kutokana na kuenea kwa taka
hizo, viumbe kadhaa wa baharini huathiriwa na kemilaki zitokanazo na taka hizo
au kwa kula mabaki ya plastiki. Mara nyingi ng’ombe, mbuzi, kondoo na mifugo
mengineyo huathirika kutokana na kula takataka za plastiki.
Nchi
za viwanda zilizoendelea hasa huzalisha
taka nyingi za palastiki kuliko nchi za ulimwengu wa tatu, hali hiyo inatokana na ukweli kwamba asilimia kuwa ya bidhaa za kawaida katika mataifa hayo ni zile
zilizofungwa katika mikebe au mifuko ya palastiki.
Katika
mwaka 2007, Marekani ndiyo iliyozalisha taka nyingi za plastiki ambapo
ilizalisha tani 230 Milioni za taka hizo.
Taifa
la pili lilikuwa ni Urusi ambayo mwaka huo ilizalisha 200 Milioni na kufuatiwa
na Japan iliyozalisha tani 52.36 Milioni za taka za plastiki. Tani 48.84
Milioni za taka zilizalishwa huko Ujerumani na kufatiwa na Uingereza
iliyozalisha tani 34.85 Milioni, Mexico tani
32.17 Milioni kiwango ambacho pia
kilizalishwa na Ufaransa. Italia kwa
upande wake ilizalisha tani 29.74 za taka hizo.
Utafiti
uliofanywa mwaka 2014 na Chuo Kikuu cha Georgia, Chuo Kikuu cha California na
Shirika liitwalo “Sea Education Association” nchini Marekani na kuchapishwa katika jarida la Sayansi liitwalo “Journal Science” la mwezi wa Februari,2015
umeonesha kuwa zaidi ya tani Milioni 8
za taka za plastiki zinatupwa baharini kila mwaka. Utafiti huo umeonesha
kuwa nchi 192 zilizo kando ya bahari
katika bahari za Atlantiki, Pasifiki, Bahari ya Hindi, Meditereniani na bahari
Nyeusi zinazalisha tani bilioni 2.5 za taka ambapo tani 275 kati ya hizo ni plastini zinazoishia
baharini.
Utafiti
huo umeonesha kuwa tani 99.5 za plastiki
huzalishwa katika miji iliyo kando ya bahari, ambapo tani 31.9 kati ya hizo
kutupwa ovyo. Utafiti huo umebainisha kuwa
taka za plastiki zinazoelea baharini
duniani kote ni wastani wa tani
245,000.
Kwa
mujibu wa utafiti huo katika mwaka 2010
nchi ambayo imeongoza duniani kwa kutupa taka nyingi za platiki baharini ni
China ambayo ilitupa baharini tani Milioni
8.8za taka za plastiki na kufuatiwa na
Indonesia iliyotupa tani Milioni 3.2. Nchi ya tatu kwa kutupa kwa wingi taka
hizo ni Philippines iliyotupa baharini tani Milioni 1.9 za taka za plastiki na
kufuatiwa na Vietnam iliyotupa tani Milioni 1.8. Nchi nyengine za bara la Asia zilizotupa kwa
wingi taka hizo ni Sir Lanka iliyotupa
tani Miloni 1.6 za taka hizo na Thailand iliyotupa tani Milioni moja.
Barani
Afrika Misri ndiyo iliyotupa taka nyingi za plastiki bahari ambapo katika mwaka
huo wa 2010, taifa hilo lilitupa tani milioni moja za taka hizo na kufuatiwa na
Nigeria iliyotupa tani Laki tisa. Huko Marekani
ya kusini kinara wa kutupa taka za plastiki baharini ni Brazil ambayo ilitupa
tani laki tano za taka hizo.
Marekani
inazalisha tani 33.6 Milioni za taka za
plastiki kila mwaka ambapo asilimi 6.5% ya taka hizo huvurugwa na kutengenezwa
vitu vyengine na asilimia 7.7% hutumika kuzalisha umeme. Taka zilizobaki
huishia mitaani na baharini.
Kwa
upande wa matumizi ya mifuko na chupa za plastiki, utafiti huo umeonesha kuwa
jumla ya mifuko ya plastiki Trilioni moja hutumika kila mwaka duniani.
Mifuko
ya plastiki bilioni tatu hutumika kila siku huko China. Utafiti huo umeongeza
kuwa nchini Marekani jumla ya mifuko ya
plastiki Bilioni 100 inatumiwa na raia wa taifa hilo kila mwaka. Jumla ya chupa
za plastiki mia tano hutumiwa na kila familia kwa mwaka huko Marekani.
Kutokana
na kuongezeka kwa matumizi makubwa ya bidhaa za plastiki duniani, taka
zitokanazo na bidhaa hiyo huchangia asilimia kumi ya taka zinazotupwa ovyo
mitaani na katika fukwe za bahari. Taka za plastiki hubaki muda mrefu ardhini
na baharini bila kuoza ikitegemea aina ya plastiki iliyotumiwa kutengenezea
bidhaa iliyotupwa.
Plasiki
iliyofukiwa ardhini hutoa kemikali ambazo baada ya muda fulani huharibu maji
ardhini na hivyo kupunguza ubora wa kiwango hicho cha maji hasa kwa
watumiaji. Katika sehemu nyingi duniani hivi sasa kumejitokeza tabia ya kufukia ardhi kwa kutumia takataka
vinazokusanywa katika maeneo ya miji. Nyingi ya taka hizo huwa na mchanganyiko
wa aina mbalimbai za plastiki ambazo baadhi
yake ni hatari kwa mfumo wa udongo.
Katika
bahari kuu duniani kuna taka nyingi za
plastiki. Taka hizo ni pamoja na taka
zilizotupwa kwa makusudi na meli kubwa za mizigo zinazosafiri katika bahari
hizo. Vilevile manowari na meli za utafiti hutupa bahari shehena kubwa ya taka za plastiki ambazo
hazina matumizi. Kutokana na udogo wake, mara kadhaa boti za kutembelea baharini
ambazo hukosa nafasi ya kuweka takataka
hutupa baharini mabaki ya plastiki na kuchangia uchafuzi wa mazingira. Mbali ya
aina zote hizo za uchafuzi, mchafuzi mkubwa wa mazingira ya bahari kwa kuputa
taka za plastiki ni meli za uvuvi ambazo hutupa baharini nyavu na aina nyengine za mitego.
Ingawa
taka nyingi za plastiki zinazotupwa baharini hutupwa na vyombo vinavyosafiri au
kuvua baharini, lakini pia kuna taka za plastiki zinazochafua bahari ambazo
hutoka ardhini. Mara nyingi taka za plastiki za aina hii ni mabaki ya chupa,
mifuko na makopo yanayoelea ambayo
hukokotwa na maji hadi baharini. Pia
taka hizo hutupwa kutoka nyumba zilizo
karibu na fukwe za bahari.
Maisha
ya viumbe kadhaa wa baharini wakiwemo kasa, seal, samaki na ndege hufariki
dunia kwa kunasa katika jarife ambazo zilizokwama chini ya bahari.
Ripoti
iliyochapishwa mwaka 2006 iliyopewa jina
“Plastic Debris in the World’s Oceans” imeonesha
kuwa zaidi ya viumbe Laki nne wa aina
mbalimbali wa baharini wanakufa kila mwaka kutokana na kuathiriwa na taka za
plastiki zilizomo baharini. Baadhi ya kasa huishi kwa kula mayavuyavu ya
baharini (jelly fish). Lakini baadhi ya
wakati kasa hao hula vipande vya taka za plastiki vinavyofanana na Mayavuyayu ya baharini na hivyo hufariki kwa
vile kipande hicho cha plastiki huziba njia ya kupitishia chakula ya kasa huyo. Mara kadhaa Nyangumi wanaofariki na
kupwelewa ufukweni na kufanyiwa utafiti hukutwa na vipande vya plastiki katika
matumbo yao ikiwa ni kiashiria kuwa nyangumi huyo amefariki kutokana na kula
plastiki hiyo.
Taka za plastiki zinazotupwa baharini haziathiri
samaki na viumbe wengine wa habarini peke yao, lakini pia huleta madhara kwa
ndege wa pwani. Katika mwaka 2004, Mashakwe kadhaa walokufa katika bahari ya kaskazini walikutwa na
vipande vya plastiki katika matumbo yao. Uchunguzi ulionesha kuwa vipande vya
plastiki vinavyoelea baharini huwababaisha ndege hao na kudhani kuwa ni chakula
na hivyo humeza plastiki hizo.
Wataalamu wa mazingira nchini Marekani wanakisia
kwamba kiasi Mashakwe milioni moja
waitwao’ “Laysan albatrosses” wanaoishi katika kisiwa kidogo kiitwacho
Midway Atoll kilichoko huko Hawaii nchini
Marekani wana mabaki ya plastiki katika matumbo yao. Ndege hao hula vipande vya
plastiki vyenye rangi nyekundu, buluu,waridi na rangi ya udongo kwa vile rangi
hizo hufanana na aina mbalimbali za vyakula wanavyokula . Tatizo hilo
lilijulikana baada ya idadi kubwa ya ndege hao kufa na mizoga ya kukutwa katika
ufukwe wa kisiwa hicho. Baada ya kuchunguzwa, ndipo mabaki mengi ya ndege hao
yalikutwa na vipande kadhaa vidogo vidogo vya plastiki walivyokula.
Mwandishi wa makala haya ni Mwalimu wa
Chuo cha Uandishi wa Habari cha ZJMMC, Kilimani mjini Zanzibar.
E-Mail: Rafikifumba1@hotmail.com
No comments:
Post a Comment