Habari za Punde

Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu CCM Mhe. Simai Mohammed Said Amewaasa Watoto Kusoma Quran Ili Iwajenge Kimaadili


Na Salum Vuai
JAMII katika Wilaya ya Kati, imehimizwa kuwasimamia vyema watoto na kuhakikisha wanasoma vizuri elimu zote, dini na dunia.

Akizungumza wakati wa mashindano ya kuhifadhi Kuran kwa madrasa za kanda ya Bungi katika jimbo la Tunguu, Mwakilishi wa jimbo hilo Simai Mohammed Said, amesema elimu ya dini ndio dira ya kuwaongoa watoto wa Kizanzibari.

Amesema vitendo vya udhalilishaji vilivyokithiri nchini, vinaweza kudhibitiwa iwapo kila mzazi atabeba kikamilifu dhima ya uchunga wa familia kwa ushirikiano na wanajamii wote.

Simai alieleza kufurahishwa na utaratibu wa kuandaa mashindano hayo ya kuhifadhi kitabu kitatakatifu cha Mwenyezi Mungu, akisema hicho cha kwanza kwani kimebeba mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu.  

“Usomi wowote unaendana na kusoma vitabu vya aina mbalimbali vikiwemo vya sayansi, lugha na vyenginevyo, lakini Kuran ndio baba wa vitabu kwani hata hiyo sayansi inapatikana humo na wavumbuzi wanaichota,” alieleza.

Kwa hivyo, alisema Kuran ambayo haina mfano wake, inapaswa kufundishwa mtoto katika umri mdogo lakini mafunzo hayo yaendane na kutekeleza kwa vitendo miongozo yake.
  
Kwa upande mwengine, Mwakilishi huyo amewashajiisha watoto na vijana kujitahidi katika masomo, na kuwataka wasitumie mitandao kwa mambo yasiyofaa kimaadili, bali waifanye kuwa ni kisima cha kuchota elimu yenye manufaa.

Mwakilishi huyo alichangia mafeni sita kwa ajili ya zawadi kwa wanafunzi wanatakaofanya vizuri zaidi kwenye mashindano hayo.

Hata hivyo, aliwataka wanafunzi wa madrasa zinazoshiriki mashindano hayo, waepuke kuhifadhi Kuran kwa tamaa ya zawadi, bali wafanye hivyo wakijua kitabu hicho ndicho kitakachowaongoa na kuwapa manusura mbele ya Mwenyezi Mungu.

Simai aliahidi kutoa kila aina ya msaada utakaohitajika ili kuyafanya mashindano hayo yawe bora zaidi kwa faida ya watoto wa kanda ya Bungi na jimbo zima la Tunguu.

Mapema, Katibu wa jumuiya ya Tahfidh Kkuran kanda ya Bungi Amir Juma Mussa Juma, aliwashukuru wahisani waliochangia kufanikiwa kwa mashindano hayo kwa misaada waliyoitoa.

Alisema michango wanayoitoa imesaidia kuyaimarisha licha ya changamoto kadhaa ambazo wanajitahidi kuzitatua kila hali inavyoruhusu.

Alieleza kuwa, wakati mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 1999 kwa kushirikisha wanafunzi wa kike na kiume katika wanaohifadhi kuanzia juzuu tatu hadi 15, yameimarika zaidi kwa kuongeza idadi ya washiriki kutoka 30 hadi zaidi ya 50.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR
10 SEPTEMBA, 2018


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.