Habari za Punde

Wafanyabiashara Mkoani Manyara Wapigwa Msasa Elimu ya Msamaha wa Kodi.


Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Diana Masalla akitoa elimu ya Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye Malimbikizo ya Madeni ya Kodi  wakati wa semina ya wafanyabiashara iliyofanyika leo mkoani Manyara.
Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Manyara Nicodemus Massawe akijibu baadhi ya maswali ya wafanyabishara wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika leo mkoani Manyara.
Baadhi ya wafanyabiashara wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa mada mbalimbali wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika leo mkoani Manyara. (Picha na Veronica Kazimoto).

Na Veronica Kazimoto.Manyara-24 Septemba, 2018
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu ya Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Madeni ya Kodi kwa wafanyabiashara, washauri wa wafanyabiashara na wakaguzi wa hesabu mkoani Manyara ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha wale wote wenye madeni ya kodi yanayotokana na riba na adhabu kuomba msamaha kabla ya tarehe 30 Novemba, 2018.
Akiwasilisha mada kuhusu msamaha huo, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Diana Masalla amesema kuwa, lengo la kutoa elimu hiyo ni kuhakikisha kwamba, kila mfanyabiashara mwenye malimbikizo ya madeni ya kodi anapata taarifa na kufuata taratibu za kuomba msamaha huo.
"Mpaka sasa TRA imeshatoa elimu hii ya msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi katika mikoa mingi nchini na lengo letu ni kuwahamasisha wafanyabiashara wote wenye malimbikizo hayo kuomba msamaha ili waweze kupata unafuu na kulipa kodi ya msingi tu isiyo na riba wala adhabu," alisema Masalla.
Aidha, pamoja na washiriki hao kupewa elimu ya msamaha wa riba na adhabu ya kodi, pia wameelimishwa kuhusu Mabadiliko ya Sheria za Kodi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018 pamoja na Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma kwa Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Afisa Maadili Mwandamizi wa mamlaka hiyo Adelaida Rweikiza akizungumza na washiriki hao wakati akiwasilisha mada ya maadili amesema kuwa, ni haki ya wateja wote wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhudumiwa vizuri na kwa usawa bila upendeleo.
"Ninyi wateja wetu mna haki ya kupata huduma bora na pia mnatakiwa kupewa haki sawa bila upendeleo wowote na pale ambapo mtumishi yeyote wa TRA akionyesha dalili zozote za uvunjifu wa maadili ikiwa ni pamoja na vitendo vya rushwa, mnatakiwa kutoa taarifa kwa viongozi wake ili hatua zichukuliwe," alieleza Rweikiza.
Mamlaka ya Mapato Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa, wafanyabiashara wenye malimbikizo yenye madeni ya kodi wanapata taarifa na kuomba msamaha huo lakini pia wanapata elimu ya mabadiliko ya sheria za kodi pamoja na namna wanavyopaswa kuhudumiwa na watumishi wa TRA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.