Habari za Punde

WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR AZUNGUMZA NA BODI YA HOSPITALI YA MNAZIMMOJA

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja walipofika Ofisni kwake na kuwashauri kusimamia uimarishaji huduma katika Hospitali hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja Dkt. Abdul-Wakil  Idrissa  Abdul-Wakil akieleza mafanikio na changamoto ya Bodi yake  walipokutana na Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Mshauri wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja Kassim Haidar Jabir akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa majukumu ya kazi zao kwa Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed hayupo pichani baada ya kufika ofisini kwa Waziri Wizarani Mnazimmoja  kwa mazungumzo.
Picha na Abdalla Omar Maelezo – Zanzibar.
Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar   17/10/2018.
Mashirikiano ya pamoja kati ya Bodi na Uongozi wa Taasisi husika ndio siri kubwa kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed alieleza hayo Ofisini kwake Mnazimmoja alipofanya mazungumzo na Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja Chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Abdulwakil Idrissa Abdulwakil.
Aliwataka wajumbe wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja kuwa washauri wa karibu na uongozi katika kusimamia utekelezaji wa kazi za Hospitali hiyo ambayo Serikali imepanga kuwa ya rufaa na imekuwa tegemeo kubwa la wananchi wengi wa Zanzibar.
Waziri wa Afya alisema huduma katika Hospitali ya Mnazimmoja kwa sasa ni nzuri tofauti na ilivyokuwa  hapo awali lakini bado zipo baadhi ya sehemu zimekuwa zikitupiwa lawama na wananchi kutokana na lugha kwa baadhi ya wafanyakazi wake.
“Moja ya jukumu lenu mukiwa wajumbe wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja ni kuushauri uongozi ili kuona wagonjwa wanapata huduma bora.” Alikumbusha Waziri wa Afya.
Aliwaeleza wajumbe wa Bodi hiyo kuwa Serikali imejenga matumaini makubwa ya kupata mafanikio kutokana na utaalamu wa miaka mingi walionao katika masuala ya Afya.
Alisema Rais Dkt. Ali Mohamed Shein ametoa msukumu mkubwa katika sekta ya Afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu bila malipo hivyo Bodi inatakiwa kuhakikisha azma hiyo inafikiwa.
“Bodi naitaka muhakikishe utekelezaji wa malengo yaliyopangwa ya  kutoa huduma bora kwa wananchi inafikiwa bila ya usumbufu na Serikali imeweka bajeti ya kutosha kwa ajili ya kununulia dawa,” alisisitiza Waziri wa Afya.
Aliwataka wajumbe wa bodi kusimamia miradi ya Wizara hiyo  na kuhakikisha uongozi unautekeleza  kwa mujibu wa  mkataba ulivyowekwa.

Aliwaambia wajumbe hao kuwa wanapotekeleza majukumu yao na kukutana na kanuni ama sheria inawabana wasisite kupeleka ushauri kupitia  kwake naye ataupeleka kwa Rais kupatiwa ufumbuzi .
Alifamisha kuwa Rais Dkt Shein yuko karibu na Wizara ya Afya na yupo tayari wakati wote kupokea ushauri ili kuhakikisha huduma za afya Zanzibar zinaimarika.
Hata hivyo aliishaauri Bodi kuandaa utaratibu wa kufanya ziara ya mara kwa mara na kusisitiza suala la kuimarisha usafi hasa katika wodi za kulaza wagonjwa kwani zinaonekana haziridhishi kutokana na mizigo na vifurushi vingi ndani ya wodi nyingi za Hospitali.
Aliwahakikishia wajumbe hao kuwa suala la kuongeza madaktari bingwa na wafanyakazi wa kada nyengine na kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa zamani litaendelea kusimamiwa na Serikali.
Mshauri  wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja Kassim Haidar Jabir amezilalamikia kampuni zinazotumia huduma ya bima ya afya kuchelewesha malipo jambo ambalo linapelekea usumbuvu wa utekeleza wa kazi wa Taasisi ya Hospitali ya Mnazimmoja.
Kwa upande wa Mjumbe wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja Dkt. Kassim Hussein alitoa shukrani kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kudhamiria kuinyanyua Sekta ya Afya kwa kuwaongezea bajeti wizara hyo kwa lengo la utekelezaji wa huduma bora kwa wagonjwa.
Aliishauri Wizara kuongeza watendaji na kutoa mafunzo ya mara kwa mara katika kada ya ufundi kutokana na vifaa vingi vya Hospitali vinapoharibika huchukua muda mrefu kufanyiwa matengenezo hata kama maharibiko ni madogo kutokana na kukosekana mafundi.
Alifahamisha madaktari watashindwa kufanya kazi ikiwa vifaa vilivyopo havifanyi kazi ipasavyo, hivyo iko haja ya kampuni ambayo inafunga mkataba wa kuleta vifaa vya mashine mbalimbali za vipimo vya maradhi  kuwepo na utaratibu wa kutolewa elimu kwa watumiaji wa vifaa hivyo
MWISHO
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.