Habari za Punde

Kongamano la Kuadhimisha Wiki ya Kupambana na Umaskini Zanzibar.

Na Kijakazi Abdalla     Maelezo, Zanzibar.
IDADI ya Vijana wasiokuwa na ajira inazidi kuongezeka hali ambayo inaweza kusababisha upunguaji wa kasi ya mapambano dhidi ya upunguzaji wa umasikini nchini.
Akifungua kongamano la maadhimisho ya wiki ya kupambana na umasikini Zanzibar  Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar Juma Hassan Juma (Reli) huko katika Ukumbi wa Studio ya Muziki na Filamu Rahaleo Zanzibar amesema kuwa hali hiyo imekuwa inapunguza kasi ya umasikini nchini.
Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kulitambua hilo imekuwa ikichukuwa juhudi mbalimbali za makusudi ili kuwasaidia vijana ili kuweza kujikwamua na umasikini.
Aidha alisema kuwa juhudi hizo ni  pamoja na kutekeleza program na miradi ya ajira kwa vijana ambazo zitaweza kuwasaidia katika masuala ya uzalishaji wa kilimo  ufugaji na shughuli za ujasiriamali.
Katibu huyo pia alisema kuwa Serikali kupitia mpango wa kupunguza umasikini ya dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020 ( MKUZA)  imekuwa ikitekeleza mikakati ya kupambana  na umasikini kwa lengo la kupunguza hali duni za kimaisha kwa wananchi wake katika maeneo ya mjini na vijijini.
Hata hivyo alisema kuwa lengo na juhudi za Serikali ni kuchochea ukuaji wa sekta binafsi ili kuwajengea uwezo wananchi wake kwa njia ya kuwaengezea kipato familia ili kuimarisha michakato ya kidemokrasia na kujenga mifumo ya ustawi wa jamii kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu.
Vilevile alisema kuwa kuondokana na hali hiyo ni vyema wananchi waimarishe na kuongeza juhudi zaidi za uzalishaji mali na kuhakikisha huduma zinazotolewa ili miundombinu izidi kuimarika kati ya serikali na sekta binafsi.
Aidha alisema kuwa Serikali uwezo wa kuajiri vijana wote ni mdogo ,hivyo ni vyema kuchangamkia  fursa zilizopo hasa katika soko la utalii badala ya kuwaachia kuzichukua wageni.
Hata hivyo aliwaomba vijana kusimama imara bila ya kubaguana na kuengeza mashirikiano ili kuweza kuunga mkono juhudi za wadau mbalimbali  kufanikisha utekelezaji wa mipango ya serikali na sekta binafsi.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Maryam Ishau Abdalla  aliitaka Serikali iwafikirie vijana katika kupunguza mifumo mingi ya ulipaji kodi kwani hali hiyo inawafanya vijana kushindwa kuendeleza biashara zao.
Hata hivyo aliwaomba vijana kujiendeleza zaidi katika kilimo cha green house kutokana na kutumia sehemu ndogo ya eneo na kupata mavuno mengi zaidi.
Kongamano hilo liliwashirikisha vijana kutoka Unguja na Pemba na mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo hali ya umasikini Zanzibar ,ajira kwa vijana na vijana kuonesha jinsi ya kuweza kujikwamua na umasikini.
CAPTION
Katibu MtendajiTume ya Mipango Zanzibar Juma Hassan Juma (Reli) Akifungua Kongamano la Madhimisho ya wiki ya kupambana na Umasikini Zanzibar huko katika Ukumbi wa Studio ya Muziki Rahaleo Zanzibar (Picha na Kijakazi Abdalla Maelezo)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.