Habari za Punde

Uzinduzi wa Show Room Blossom.Uuzaji wa Bidhaa za Mbao na Tiles Zanzibar.

Na Abdi Shamnah
Wazanzibar wametakiwa kubadilika na kutumia ipasavyo vifaa vya kisasa vya ujenzi, ili kuleta haiba ya nyumba zao, sambamba na kuishi maisha yalio bora.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Ardhi, nyumba, maji na nishati, Salama Aboud Talib katika uzinduzi wa ‘show room ya Blossom Cheer, uliofanyika katika Hoteli ya Serena Inn mjini hapa.
Show room hiyo inayohusisha na uuzaji wa bidhaa ya mbao (milango) na Tiles, ni ya kwanza kuanzishwa hapa Zanzibar, ikimilikiwa kwa ubia kati ya mwekezaji mzalendo Seif Salum Zahor pamoja na raia wengine kutoka nchini China.
Alisema ufunguzi wa show room hiyo ni fursa adhimu kwa Wazanzibari kupata bidhaa za ujenzi zilizo bora na za bei nafuu, sambamba na kuondokana na usumbufu wa kuagiza bidhaa hizo kutoka nchi za nje, hususan China.
“Uwepo wake unaweza kubadili mfumo mzima wa maisha, husuan katika suala la makaazi kwa kuwa na makaazi bora na yatakayoleta haiba katika mji wetu”, alisema.
Aliwataka wamiliki wa kampuni za ujenzi hapa nchini kushirikiana na wamiliki wa show room hiyo ili kuleta mabadiliko katika mfumo wa ujenzi kwa kuwa na majengo ya kisasa na yenye vifaa vyote muhimu.
Aidha, aliwaomba wawekezaji hao kuzingatia kwa makini hali za maisha ya wananchi na kutimiza ahadi zao kwa kuingiza bidhaa bora, zenye viwango na zitakakavyopatikana kwa bei nafuu ili wananachi waweze kuzimudu.
“Nawaomba sana mzingatie sheria, kanuni na miongozo ya nchi yetu, hususan katika suala la kulipa kodi ili kuwa na biashara isiyo na  utata”, alisema.
Sambamba na kuwataka biashara hiyo kuwa endelevu, aliwaomba kupanuwa wigo wa uingizaji bidhaa kwa kuzingatia  mahitaji ya Soko la Utalii ambalo limeimarika sana hapa nchini, hususan katika ujenzi wa Hoteli za kisasa.
Nae, Meneja wa Show room hiyo Rocky Guo, alisema azma ya kufikisha huduma hizo hapa Zanzibar  ni kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kwa wananchi wa Zanzibar, kutoka kampuni kubwa ya uzalishaji wa vifaa hivyo wanayoimiliki, ilioko jimbo la Guangzhou nchini China.
Alisema pamoja na uingizaji wa vifaa hivyo, pia show room hiyo itajihusisha na shughuli mbali mbali, ikiwemo kusarifu michoro ya ujenzi wa nyumba na majengo mbali mbali, sambamba na kutowa ushauri na miongozo juu ya kupata bidhaa bora kutoka nchini China na kuzifikisha nchini.
Alisema tayari Kampuni yake  ina matawi (showroom) katika nchi zipatazo 20 Barani Afrika, ikiwemo nchi za Rwanda, Ethiopia, Misri, Libya, Sudan, Benin, Cameroon na nyenginezo.
Mapema, Mwekezaji mzalendo Zahor Salum, alisema wananchi na wakandarasi wa ujnezi watakaonunua  vifaa vitokanavyo na mbao  kutoka show room hiyo, watapatiwa huduma za ufungaji katima majengo yao bila gharama zozote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.