Habari za Punde


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia Mkutano wa Tano wa Jumuiya ya Wataalamu wa Figo Tanzania, wakati wa ufunguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Karume Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Zanzibar.23/11/2018. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la 

Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema 

Serikali inaendeleza sera na dhamira ya Mapinduzi 

matukufu ya 1964, kwa kutoa huduma bure za 

matibabu kwa wananchi wa Zanzibar bila ubaguzi.

Alisema hatua hiyo inakwenda sambamba na sera na Ilani ya 

Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020.

Dk. Shein amesema hayo leo, alipofungua mkutano wa tano 

(5)wa Chama cha Wataalam wa Figo Tanzania (NESOT), 

uliofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, nje 

kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Mkutano huo siku tatu unaowashirikisha viongozi, 

wataalam,madaktari,wauguzi, na wadau mbali mbali kutoka ndani na nje ya nchi, unaambatana na kauli mbiu  “Uimarishaji wa matibabu ya figo katika maeneo yenye changamoto za rasilimali tiba”.

Dk. Shein alisema pamoja na kuwepo ongezeko kubwa la 

watu hapa nchini, sambamba na kupanda kwa gharama za 

matibabu ya magonjwa mbali mbali ikiwemo figo, serikali 

itaendelea kusimamia sera hiyo ikiwa ni hatua ya kuyaenzi 

Mapinduzi hayo.

Alisema  kwa mnasaba huo, katika bajeti ya mwaka wa fedha 

wa 2018/2019, Serikali imeongeza bajeti ya dawa hadi 

kufikia shilingi Bilioni 12.7  (sawa na asilimia 81.43) kutoka shilingi Bilioni 7 zilizotengwa katika mwaka 2017/2018.

“Katika juhudi za kuimarisha huduma bora za Afya, 

tumeimarisha bajeti ya Wizara Afya kwa mwaka 2018/2019, 

kwa asilimia 81.43, hatua hii ni utekelezaji wa ahadi ya 

kuwapatia matibabu bure wananchi wote’, alisema.

Alieleza kuwa Tanzania ina wagonjwa wengi wa ugonjwa wa 

figo na kubainisha changamoto kadhaa zilizopo katika 

kuukabili ugonjwa huo, ikiwemo upungufu wa nyenzo na 

rasilimali.

Alisema juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zilianza 

kipindi kirefu na kuwapongeza waanzilishi wake, akiwemo 

Dk. Mohamed Jidawi, Dk. Jamalla Adam na marehemu Dk. 

Malik Abdalla, ambapo kwa ushirikiano na washirika mbali 

mbali wa Maendeleo na Chuo Kikuu cha Haukland cha 

nchini Norway, juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda.

Alisema Serikali itaendelea na juhudi za  kuimarisha 

huduma na kuongeza wataalamu wabobezi katika tiba ya magonjwa ya figo nchini, ili kukabailiana vilivyo na ugonjwa huo hatari.

Aidha, alipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuiliwa na 

NESOT katika kuwashajiisha madaktari wake  katika suala la 

kufanya utafiti na kubainisha kuwa tafiti hizo zitasaidia 

kupatikana ufumbuzi wa matatizo mengi kuhusiana na 

ugonjwa huo.

Dk. Shein aliagiza kuwepo programu maalum, itakayokuwa 

na dhima ya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa 

kuchukuwa tahadhari ili kupunguza ukubwa wa tatizo la 

‘mshtuko wa ghafla wa figo’ (acute kidney injury), ambalo 

alisema ni hatari sana kwa jamii.

Alikitaka chama hicho kuendelea kuishajiisha jamii, hususan 

vijana kusoma taaluma ya fani  ya tiba ya binadamu, ili 

hatimae waweze kupata wanachama wengi zaidi.

Vile vile aliwataka wataalamu hao kutokuvunjika moyo 

kutokana  na changamoto mbali mbali wanazokabiliana 

nazo, na badala yake waongeze juhudi na kufanya kazi kwa kutawaliwa na dhamira, kwa kigezo kuwa hakuna kinachoshindikana.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwataka wanafunzi 

walioshiriki mkutano huo kuwa makini wakati wa 

majadiliano, ili kuongeza uwelewa wao  katika mambo mbali 

mbali. ambapo darasani hawawezi kuyapata.

Nae, Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed, 

aliahidi Wizara yake kushughulikia uanzishaji wa kituo cha 

tiba ya ugonjwa wa Figo kisiwani Pemba ili kupanua wigo wa 

upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Aliwataka wanafunzi walioshiriki kongamano hilo kutumia 

vyema fursa hiyo na kupokea utaalamu kutoka kwa 

madaktari bingwa kutoka nchi mbali mbali duniani. 

Aidha, aliwataka madaktari na wataalamu wa afya nchini, 

kuongeza ushirikiano kati yao ili kuleta ufanisi katika 

utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

”Kumekuwepo na matukio ya wagonjwa kufariki dunia, kwa 

sababu tu daktari mmoja hataki ‘ku- share’ na mwenzake 

kupata mawazo mapya ya tiba”, alisema Waziri Hamad.


Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara Afya, Asha Ali Abdalla 

alisema kuanzishwa kwa huduma ya tiba ya ugonjwa wa figo 

nchini, kumetokana na serikali kutambua na kuthamini 

mahitaji ya wanyonge katika upatikanaji wa huduma hiyo 

inayohitaji gharama kubwa.


“Lengo ni kutanua wigo katika kuwafikia wananchi wengi 

zaidi wenye mahitaji ya huduma hii’, alisema.


Alisema pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa na 

Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo, kumekuwepo 

changamoto mbali mbali zinazojitokeza, ikiwemo uchache 

wa wataalamu na ukosefu wa vifaa.

Aidha, Rais wa Chama cha wataalamu wa Figo Tanzania 

(NESOT), Dk.Onesmo Kisanga, alisema inakadiriwa watu 

wapatao 160, 000 wanakabiliwa na ugonjwa huo hapa 

Zanzibar.

Alisema  utafiti uliofanywa na Chama hicho umebaini kuwa 

asilimia 6.8 ya Watanzania wanakabiliwa na ugonjwa huo, 

wakiwa bado hawajajitambua.


Alibainisha kuwa pamoja na gharama kubwa za tiba ya 

ugonjwa wa figo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 

imefanikiwa kutoa tiba bure kwa wagonjwa wanaojitokeza 

kufuata matibabu.


Alisema kwa kutambua ugumu na gharama za matibabu ya 

ugonjwa huo, NESOT imejipanga kutoa elimu kwa jamii, 

ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Aidha, alipongeza mafanikio makubwa yaliopatikana kwa 

Tanzania kuwa na jumla ya vituo tisa (9) vya kusafishia 

damu (dialysis).

Dk. Kisanga alisema Kongamano hilo lina dhima ya 

kuimarisha huduma za matibabu ya Afya katika maeneo 

yenye changamoto za ugonjwa huo.

“Dhima ya kongamano hili ni kuboresha na kuimarisha 

matibabu ya figo katika maeneo yenye changamoto za 

ugonjwa huu, tutajadili yaliotokea Zanzibar, Tanzania, 

Afrika, India  na dunia kwa jumla, lakini pia mafanikio na 

changamoto zitajadiliwa’, alisema.


Viongozi mbali mbali walihudhuria kwenye mkutano huo, 

akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif 

Ali idd.

Na Abdi Shamnah , Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.