Habari za Punde

Serikali Kujenga Vituo Vya Polisi 65 Katika Wilaya.


Naibu  Waziri  wa Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi,  Mhandisi  Hamad  Masauni, akiwaongoza  Wajumbe  wa  Kamati  ya  Ulinzi  na  Usalama  ya  Wilaya  ya Kilindi  kuingia  Kituo  cha  Polisi  cha  Songe, ikiwa  ni ziara  ya  kikazi  ya  Naibu  Waziri  kukagua  shughuli  za  ulinzi  na  usalama  wilayani  Kilindi  mkoani Tanga 
Naibu  Waziri  wa Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi,  Mhandisi  Hamad  Masauni, akizungumza katika kikao cha ndani kilichohusisha  Wajumbe  wa  Kamati  ya  Ulinzi  na  Usalama  ya  Wilaya  ya Kilindi  ikiwa  ni ziara  ya  kikazi  ya  Naibu  Waziri  kukagua  shughuli  za  ulinzi  na  usalama  wilayani  Kilindi  mkoani Tanga . Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo na Kulia ni Katibu  Tawala  wa  Wilaya  hiyo,  Warda  Abeid.
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo  akizungumza katika kikao cha ndani kilichohusisha  Wajumbe  wa  Kamati  ya  Ulinzi  na  Usalama  ya  Wilaya  ya Kilindi  ikiwa  ni ziara  ya  kikazi  ya  Naibu  Waziri  wa  Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati) kukagua  shughuli  za  ulinzi  na  usalama  wilayani  Kilindi  mkoani Tanga . Kulia ni  Katibu  Tawala  wa  Wilaya  hiyo, Warda  Abeid.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi , Edward Bukombe, akizungumza katika kikao cha ndani kilichohusisha  Wajumbe  wa  Kamati  ya  Ulinzi  na  Usalama  ya  Wilaya  ya Kilindi  ikiwa  ni ziara  ya  kikazi  ya  Naibu  Waziri  wa  Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (hayupo pichani, ) kukagua  shughuli  za  ulinzi  na  usalama  wilayani  Kilindi  mkoani Tanga.
 Picha  na  Wizara  ya Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi

Na Mwandishi Wetu
Serikali imedhamiria kujenga Vituo vya Polisi 65 katika wilaya mbalimbali nchini ikiwa ni juhudi za kukabiliana  na uchakavu na upungufu wa vituo vya polisi nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni baada ya kutembelea na kukagua Kituo cha Polisi cha Songe ambacho ndio kituo kikuu katika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga

Alisema Serikali inatambua changamoto za vituo vya polisi ikiwemo uchakavu, udogo wa majengo katika vituo mbalimbali nchini na iko katika mpango wa kujenga vituo vya polisi 65 ili kuwepo na ulinzi thabiti wa raia na mali zao.

“Serikali inatambua changamoto ya vituo vya polisi hasa katika wilaya mpya nchini, ikiwepo uchakavu wa majengo, kwahiyo uko mkakati maalumu wa kujenga vituo vya polisi 65 nchi nzima ili kuweza kukabiliana na matukio ya kiuhalifu, lengo la serikali ni kuhakikisha raia wake na mali zao zinakua salama na matukio ya kiuhalifu yanapungua na kutoweka kabisa,” alisema Masauni

Alisema Serikali pia inakaribisha nguvu za wananchi na wadau mbalimbali ambao wako tayari kusaidia ujenzi wa vituo vya polisi huku akipongeza baadhi ya maeneo nchini ambako vituo vya polisi vimejengwa kwa ushirikiano wa michango ya wananchi na serikali.

Awali akitoa taarifa ya Ulinzi na Usalama  ya Wilaya ya Kilindi, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Sauda Mtondoo alisema hali ya uhalifu kuanzia kipindi cha Januari hadi Oktoba 2018 ilikua ya wastani huku kukiripotiwa upungufu wa makosa kwa asilimia 9.8 kati ya mwaka 2018 na 2017.

“Kwa mujibu wa takwimu za uhalifu kulikuwa na jumla ya makosa makubwa ya jinai 163 ndani ya mwaka huu yaliyoripotiwa kwa kulinganisha na makosa 179 yaliyoripotiwa ndani ya mwaka 2017, ukiwepo upungufu wa makosa 16 katika vipindi hivyo viwili,” alisema Sauda

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mbunge wa Kilindi, Omari Kibua alimshukuru  Naibu Waziri kwa kufika jimboni hapo kujionea hali halisi ya kituo hicho kikuu cha wilaya  baada  ya  kumuomba  kufanya  hivyo wakati wa kikao cha bunge kilichomalizika hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.