Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Yaadhimishwa Kitaifa Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiingia kwenye Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni kuhudhuria  kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani akiwa Mgeni rasmi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akijiandaa kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Znzibar Balozi Seif kuzungumza na Wananchi mbali mbali katika kilelecha siku ya Kimataifa ya Watu wenye ulemavu Duniani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani hapo Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni.
Balozi Seif Kulia akimkabidhi Zawadi Bibi Jouaquiline Mohan Mwakilishi wa Shirika la Umojawa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA} kazi kubwa ya usimamizi wa Mpango wa usajili wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar.
Balozi Seif Kulia akimkabidhi Zawadi Bibi Jouaquiline Mohan Mwakilishi wa Shirika la Umojawa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA} kazi kubwa ya usimamizi wa Mpango wa usajili wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar.

Balozi Seif akibonyesha kitufe kwenye Kompyuta kuashiria kuzindua Rasmi Mfumo wa kuhifadhi Taarifa za Watu wenye Ulemavu Zanzibar akishuhudiwa na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA} Bibi Jouquiline Mohan Kushoto yake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwapongeza Vijana Walemavu  wasioona Awena na Jamila baada ya kusoma utenzi katika mahadhi yaliyoleta ladha kwenye sherehe hizo.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Bwana Haidar Hashim Madewea akito salamu za Baraza hilo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani.Wa kwanza Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchini Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdulla Hassan Mitawi.
Baadhi ya washiriki wa kilele cha maadhimisho ya ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani zilizofanyika hapo Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni.
Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania wakifuatilia matukio tofauti yaliyojiri ndani ya Ukumbi huo. 

Balozi Seif akimpongeza Bibi Zeyana Ahmed Mlemavu baada ya kusoma Risala kwa ufasaha ya Shirikisho la Watu wenye ulemavu kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani.


Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema si jambo jema hata kidogo wala haipendezi kwa wana jamii kuona inawatenga, kuwanyanyasa, kwa kuwatendea matendo maovu Watu wenye ulemavu ambayo ni kinyume na Haki za Binaadamu.
Alisema Watu wenye ulemavu wanahitaji kutunzwa, kuthaminiwa na kuenziwa utu wao kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 na Sheria ya Watu wenye Ulemavu.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani sherehe zilizofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa  Sheikh Idriss Abdull Wakil uliopo Mtaa wa Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinmduzi ya Zanzibar imekuwa ikisikitishwa juu ya hali ya kinyama inayokiuka misingi ya Haki za Binaadamu inayofanywa na Watu wasiokuwa na maadili wala huduma kwa kuwafanyia vitendo viovu Watu wenye ulemavu pamoja na Wanawake na Watoto.
Balozi Seif alionya kwamba katika kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia unaowakumba pia Watu wenye Ulemavu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukuwa hatua kali na za kisheria dhidi ya wale wanaobainika kujihusisha na Vitendo hivyo viovu.
“ Serikalio haitamvumilia wala kumuonea aibu mtu ye yote atakayebainika kutenda jambo hilo ovu”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Aliviagiza Vyombo vya Ulinzi, usalama pamoja na vile vya Sheria kutolifumbia jicho suala hilo na badala yake kuchukuwa hatua zinazofaa kwa mujibu wa Sheria zinavyoelekeza ili kukomesha vitendo hivyo.
Balozi Seif  alisisitiza kwamba ni wajibu wa Wananchi na Wana Jamii wote kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha  ili kukabiliana na kadhia hii inayotishia ustawi wa Watu wenye Mahitaji Maalum ambao wanastahiki na wao kuishi kwa amani na upendo.
Akizungumzia suala  la muhimu la usajili wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Idara ya Watu wenye Ulemavu imeanza kutumia Mfumo wa Takwimu aliouzindua Rasmi kwa kujua uzito wa suala hilo katika Taifa.
Balozi Seif alisema Wananchi wanapaswa kuunga mkono Mpango huo ulioanzishwa na Serikali kupitia Idara ya Watu wenye Ulemavu kwa kuwaandikisha Watoto wao wenye ulemavu kupata Elimu itakayowafaa kulingana na mazingira ya Ulemavu wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na mchango mkubwa uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Idadi ya Watu kwa kuwaunga mkono Watu Wenye Ulemavu kwa kufanya Tathmini ya Upembuzi yakinifu kwa Vijana wenye Ulemavu.
Alisema Tathmini ya Upembuzi huo ililenga kutambua uelewa wao juu ya masuala ya Afya ya uzazi wa mpango uliokwenda sambamba na utengenezaji wa mpango Mkakati wa Baraza la Taifa na kutengeneza utekelezaji wa Sera ya Kitaifa ya Watu wenye Ulemavu.
Mapema akisoma Risala ya Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Mmoja wa miongoni mwa Wajumbe wa Shirikisho hilo Bibi Zeyana Ahmed alisema  bado zipo baadhi ya Familia zinarejesha nyuma hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya Watu wanaodhalilisha Watu Wenye Ulemavu.
Bibi Zeyana alisema Familia hizo zimekuwa zikiendeleza tabia za kutoa suluhishi kwa Watu wanaodhalilisha Watu wenye Ulemavu hasa kwenye vitendo vya Ubakaji vinavyosababisha Mimba.
Alisema kwa niaba ya Shirikisho hilo wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zinazondelea kuchukuwa katika kuwajengea mazingira bora Wananchi wakiwemo Watu Wenye Ulemavu hasa katika Sekta muhimu ya Elimu.
Bibi Zeyana alifahamisha kwamba upatikanaji wa Elimu kwa Kundi kubwa la Watu wenye Ulemavu umewezesha kupunguza ujinga wa kutojua kusoma wala kuandika mambo ambayo yalikuwa nadra kupatikana kwa Watu hao ambayo zamani hayakuwa Rafiki.
Hata hivyo Bibi Zeyana alitahadharisha kwamba idadi ya Watu wenye ulemavu Nchini inaonekana kuendelea kuongezeka kwa kasi kutokana na ajali za mara kwa mara, Maradhi pamoja na mashambulizi ya silaha za jadi Mitaani zinazopelekea wajeruhiwa kubakia kuwa vilema.
Alisema Jamii kwa kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi za Ulinzi zinapaswa kuendelea kushirikiana kupunguza wimbi hili linaloweza kusababisha athari zaidi katika miaka ya baadae.
Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa  Idadi ya Watu {UNFPA} Mwakilishi wa Shirika hilo Bibi. Joaquiline Mohan alisema Taasisi hiyo inaendelea kutekeleza Programu ya 18 ya umuhimu wa usajili wa Watu wenye Ulemavu ili kundi hilo lipatiwe huduma za Kibinaadamu kwa Uhakika.
Bibi Joaquiline alisema Programu hiyo iliyoanza mnamo Mwaka 2011 inakwenda sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ulioasisiwa katika kustawisha Jamii ya Watu wenye Ulemavu inayostahiki kupata haki kama zilkivyo jamii nyengine za kawaida.
Alisema Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Idadi ya Watu linaamini kwamba kila Mtu anastahiki kuhesabiwa kwa ajili ya Maendeleo ya Watu wote mahali popote pale.
Bibi Joaquiline aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba Shirika hilo limeahidi kuendelea kufanyakazi pamoja na Serikali zote mbili Tanzania ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuona Ustawi wa Wananchi unaimarika kila wakati.
Naye kwa upande wake akitoa salamu za Mkoa Mjini Magharibi Mkuu wa Mkoa huo Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mkoa huo za kushirikiana na Taasisi nyengine kusaidia Jamii ya Watu wenye Ulemavu lakini bado itakabiliana na tabia ya baadhi ya Watu wanaoendeleza vitendo vya  omba omba katika mitaa ya Mjini.
Mh. Ayoub alisema tabia hiyo ambayo inapaswa kuchukuliwa hatua kwa hadhari kubwa inaleta taswira mbaya hasa kwa Watalii na wageni wanaoamua kutembelea Maeneo ya Mji.
Pamoja na mambo mengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuzindua Rasmi Mfumo wa Kuhifadhia Taarifa za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar ambapo Mkurugenzi wa Idara ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Bibi Abeda Rashid Abdullah alisema Baraza la Taasisi hiyo lilifanya jitihada za kuanzisha Mfumo huo.
Bibi Abeda alisema usajili wa Watu Wenye Ulemavu uliopata msukumo kutoka Shirika la Mpango wa Idadi ya Watu Duniani {UNFPA} ulianza Rasmi Mnamo Mwaka 2012 na kuendelea tena Mwaka huu wa 2018.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani unasema “ Kuwawezesha Watu Wenye Ulemavu na kuhakikisha Ujumuishwaji na Usawa”.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.