Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Aongoza Kikao Cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar, kilichofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar,kulia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi na kushoto Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Abdallah Juma Mabodi.
Na.Is-haka Omar - Zanzibar.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein leo ameongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.
Kikao hicho cha Siku Moja kimeanza majira ya saa 4:00 asubuhi katika Ukumbi wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar na kuhudhuriwa na Wajumbe wa Kamati Maalum ya NEC CCM Taifa Zanzibar.
Kupitia Kikao hicho  Makamu Mwenyekiti Dk. Ali Mohamed Shein, aliwapongeza Wanachama, Watendaji na Viongozi wote wa CCM kwa kufanikisha Ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang’ombe ambapo aliyekuwa Mgombea wa CCM Mhe.Ramadhan Hamza Chande alishinda kwa  kura 7,274 sawa na asilimia 90.5.
Dk.Shein alieleza kuwa ushindi huo haukuwa wa bahati mbaya bali ulitokana na ridhaa ya Wananchi wa Jimbo hilo kwa kuridhishwa na kasi ya Utekelezaji kwa vitendo Sera na mipango endelevu ya maendeleo inayotekelezwa kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Katika maelezo yake Dk.Shein aliwasisitiza Wajumbe wa Kikao hicho na Wana CCM kwa ujumla kuwa Ushindi wa CCM Jang’ombe ni sehemu ya maandalizi ya Ushindi wa Kihistoria katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
“Kazi kubwa iliyobaki mbele yetu ni kujipanga vizuri kwa kuhakikisha kila Mwanachama wa CCM atatekeleza wajibu wake kwa sasa kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya Chama chetu, ili 2020 tushinde na kuendelea kuongoza Dola”, alisema Dk. Shein na kuogeza kuwa CCM imekuwa kinara wa kulinda na kuthamini misingi ya Demokrasia.
Pamoja na hayo aliwakumbusha Wajumbe wa Kikao hicho kwamba wanatakiwa kuwa mfano bora wa kulinda maadili, miongozo na kanuni za Chama Cha Mapinduzi.
Baada ya kutoa nasaha hizo Mwenyekiti wa Kikao hicho Dk.Shein alikifungua Kikao na kupokea na kujadili kwa kina taarifa mbali mbali kutoka katika Idara na Vitengo vya Chama Cha Mapinduzi.
Kikao hicho ni cha kawaida kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi mwaka 1977 Toleo jipya la 2017,Ibara ya 108 (2), inayofafanua kwamba Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itafanya mikutano yake ya kawaida mara moja kila miezi mitatu.    
Viongozi wakuu na Wajumbe wa Kikao hicho walioudhuria ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.