Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Marikiti Kuu ya Darajani Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifanya ziara fupi katika Soko Kuu la Darajani kuangalia hali halisi ya Mazingira sokoni hapo ambapo ndio uso wa Zanzibar.Kulia ya Balozi Seif ni  Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud na Kushoto ya Balozi ni Meya wa Manispaa ya Mjini Mstahiki Khatib Abdulrahman.
Balozi Seif akiulizia bei halisi ya samaki katika Soko Kuu la Darajani alipotembelea kuangalia mazingira ya soko hilo.
Balozi Seif akisalimiana na Watalii kutoka Nchini Marekani walioonyesha kufurahia biashara sokoni hapo ambapo walifika kutafuta Bidhaa za Viungo.
Balozi Seif  akifurahia na kuridhika na hali halisi ya mazingira ya samaki wanaouzwa Soko Kuu la Darajani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiulizia bei ya Nyama katika soko Kuu la Darajani.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Watalii kutoka Nchini Uholanzi waliofika sokoni darajani kupata mahitaji.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza Wachuuzi wa Nyama Marikiti kuhakikisha kwamba Nyama wanayouza imekaguliwa na kuthibitishwa na Daktari wa Mifugo ili itakapofika kwa Mlaji iwe na uhakika wa kumuondoshea Mashaka ya Kiafya.
Alisema ziara za ghafla alizozifanya hivi karibuni katika Machinjio tofauti hazikumridhisha katika baadhi ya Machinjio binafsi ambayo huchinjwa Ng’ombe na baadaye nyama yake kusambazwa katika Masoko mbali mbali hapa Nchini jambo ambalo kama haikuzingatiwa ni hatari kwa afya za Wananchi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi katika Soko Kuu la Darajani kuangalia hali halisi ya mazingira yaliyopo kwenye eneo la kuuzia Samaki, Nyama pamoja na Kuku ambalo ni Muono halisi wa mwanzo wa sura ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali kupitia Halmashauri za Baadhi ya Wilaya zimelazimika kuchukuwa hatua za kuyafunga baadhi ya Machinjio Nchini baada ya kukosa vigezo vilivyowekwa hasa usafi wa Mazingira.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameridhika na hali halisi ya usafi wa mazingira aliyoiona katika eneo la Soko la Darajani na kuupongeza Uongozi wa Baraza la Manispaa Zanzibar kwa kusimamia usafi huo.
Balozi Seif aliuomba Uongozi huo kuendelea na utaratibu huo na Serikali ikiona sehemu hiyo itashindwa kutosheleza mahitaji ya Wananchi itaangalia uwezekano wa kutafuta eneo jengine ili kuondosha usumbufu utakaojitokeza hapo baadae.
Mapema akimtembeza Balozi Seif  kwenye Jengo jipya la Marikiti ya Kuku Mkuu wa Idara ya Mipango Miji na Ujenzi ambae pia ni Mhandisi wa Baraza la Manispaa Zanzibar Nd. Mzee Khamis Juma alisema ujenzi huo umefuata taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Nd. Mzee alisema wakati jengo hilo litakapoanza kazi muda wowote kuanzia sasa kwa vile limeshakamilika, wafanyabiashara wa Nyama ya Kuku watalazimika kuzingatia taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa mfumo wa kisasa wa Kitaalamu wa uchinjaji wa Kuku.
Alifahamisha kwamba jengo hilo litakapoanza kutoa huduma litakuwa na uwezo wa kupatikana ajira zisizopunguwa 120za Wafanyabiashara wakiwemo akina Mama watakaokuwa wakitoa huduma za vyakula vinavyotokana na Mali ghafi ya Kuku.
Mkuu huyo wa Idara ya Mipango Miji na Ujenzi ambae pia ni Mhandisi wa Baraza la Manispaa Zanzibar alisema ujenzi wa Jengo hilo umegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 186,000,000/- hadi sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.