Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Akifungua Kongamano la Pili la Kiswahili Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil Kikwajuni. leo 12-12-2018.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati alilifungua Kongamanola Pili la Kiswahili la Kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa Zanzibar,(BAKIZA) katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar, na kuwashirikisha Watunzi wa Vitabu kutoka Sehemu mbalimbali. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Kongamano la Kiswahili linaloendelea lina mchango muhimu katika kuendeleza historia,  maendeleo  ya Kiswahili pamoja na kuitambulisha Zanzibar kimataifa.
Alisema  kongamano hilo  hutoa fursa ya kuendeleza uhusiano kati ya wataalamu  wa lugha hiyo popote walipo duniani .
Dk. Shein amesema hayo leo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni mjini hapa, alipofungua Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili.
Kongamano hilo la siku mbili, limeandaliwa na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) na kuwashirikisha wataalamu na mabingwa wa lugha ya Kiswahili, watunzi wa vitabu, waandishi wa riwaya;tamthilia na mashairi pamoja na wapenzi wa lugha hiyo kutoka maeneo mbali mbali ndani na nje ya nchi.
Alisema Zanzibar inatambulika duniani kote kuwa ndio  chimbuko la Kiswahili fasaha kinachotokana na lahaja ya Kiunguja mjini ambayo ilipitishwa  mwaka 1930, hivyo akatowa wito wa  Kongamano hilo litumike kuiendeleza historia hiyo.
Alisema  kukuwa, kuenea na kuimarika kwa matumizi ya kiswahili fasaha, kumechangiwa na sababu mbali mbali, na kubainisha kuwa hatua hiyo inategemea sana kuwepo kwa juhudi za makusudi za kitaasisi pamoja na makundi maalum ya wataalamu.
"Ni dhahiri kuwa jambo hili haliwezi kufanikiwa kwa sadfa au fuluku, bali ni lazima iwepo dhamira ya dhati, mipango na mikakati madhubuti pamoja na ari ya kuwa tayari katika utekelezaji wake", alisema.
Akinasibisha hali hiyo na kauli yake, Dk. Shein alisema Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na marehemu mzee Abeid Amani Karume walikuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha lugha hiyo na ndio maana  kwa nyakati tofauti lugha hiyo ilitangazwa kuwa lugha rasmi  ya Taifa na Zanzibar mwaka 1964 , sambamba na Lugha ya Taifa la Tanzania (1967).
Alisema Serikali zote mbili muda wote zimekuwa zikihikimiza matumizi sahihi ya lugha hiyo katika vikao vyote rasmi pamoja na mikutano ya Kimataifa ndani ya nchi.
Aidha alieleza kuwa ni jambo zuri kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki nayo kutambuwa jitihada zinazochukuliwa katika kukiendeleza kiswahili, hivyo kuchukua hatua ya kuanzisha Ofisi ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki hapa Zanzibar mwaka 2007.
Dk. Shein , alipongeza juhudi za nchi za Rwanda na Afrika Kusini katika kuimarisha matumizi ya lugha hiyo, kwa kuanza kufundishwa katika skuli zao.
Aliwataka vijana wanaochukuwa masomo ya Kiswahili katika vyuo vikuu mbali mbali nchini, kuchangamkia fursa za ajira zilizopo katika maeneo mbali mbali ya Ukanda wa Afrika Mashariki.
Vile vile alisisitiza haja ya taasisi zinazoendeleza matumizi bora ya lugha ya kiswahili pamoja na wasomi,  kutumia machapisho ya lugha hiyo  kufanya tafiti ili kujenga uwezo wa kiutafiti na kuandika mambo mbalimbali yanayohusu ukuaji wa lugha hiyo na utamaduni wake.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuelekeza nguvu  katika kufanya tafiti nyingi zaidi kwenye fani mbali mbali za Isimu, fasihi na Utamaduni wa kiswahili.
Alisema tafiti zitasaidia sana katika kufanikisha dhamira ya kuendeleza lugha hiyo pamoja na kuchangia upatikanaji wa maarifa mapya kwa wataalamu wa lugha na kujifunza matumizi fasaha ya ya lugha hiyo.
"Hali hiyo itapunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo liliopo la kulazimisha utowaji wa misamiati bila ya kurejea katika usuli wenyewe wa lugha", alifafanua.
Alibainisha kuwa utafiti utawasaidia wataalamu wa lugha hiyo kuzungumza kwa hoja na kusimamia hoja zao badala ya kuzungumza mambo kwa mazoweya.
Aidha, aliagiza kutumiwa fursa ya kuwepo kwa Tume ya Taifa ya sayansi na Tdeknolojia katika kufanikisha tafiti hizo.
Alieleza kuwa katika kutilia mkazo suala la kufanya utafiti, kwa kuanzia katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 Serikali imetenga jumla ya shilingi Milioni 500 kwa ajili ya tafiti za aina zote, hivyo akatowa wito  kwa wanaohitaji kufanya utafiti kutumia fedha hizo zilizotengwa.
Dk. Shein aliwataka washiriki wa Kongamano hilo kujivunia lugha hiyo, kwa vile haiihitaji mwega wa kusaidiwa ili kukamilisha mawasiliano.
Alieleza kuwa Kiswahili ni lugha inayojitosheleza kwa msamiati na kuwezesha mawasiliano katika nyanja  zote, hivyo kukidhi haja na hoja za watumiaji wa lugha hiyo katika mawasiliano.
Aliwataka wataalamu wa lugha ya kiswahili kulitumia Kongamano lililoandaliwa ipasavyo, kwa kubainisha changomoto zilizopo na kupendekeza mbinu sahihi za kukabiliana nazo.
Alisema ni wakati muafaka wa kuangalia mafanikio yaliofikiwa na kuibuwa mbinu za kuyakuza na kuyadumisha.
Aidha, alisema amefurahishwa na hatua ya wandaaji wa kongamano hilo ya kuwahusisha wachapishaji wa vitabu, na kubainisha kuwa hatua hiyo itawezesha kuwatambuwa na kuona baadhi ya kazi zao.
"Ni matumaini yangu kuwa Kongamano hili la siku mbili lililosheheni wataalamu na mabingwa  wa lugha litazingatia hoja na ukumbi huu utarindima  mijadala moto moto ya kitaalamu", alisema.
Aidha alisema Kongamano hilo litatowa mbinu muafaka zitakazoweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoikumba lugha hiyo, ikiwemo uchapishaji wa kazi za waandishi, hususan wale wanaochipukia.
Katika hatua nyengine, Dk Shein aliwatunuku vyeti vya heshima, magwiji wa tungo za mashairi ya taarabu asilia Zanzibar, ambao kazi zao zimeendelea kutambulika kwa ubora  na kutumika hadi leo hii.
Aliowatunuku (kwa niaba) ni pamoja na Marehemu Bakar Abeid Ali, Marehemu Hijja Saleh Hijja, marehemu Idd Abdalla Farahan na Masauni Yussuf.
Aidha, aliwatunuku vyeti vya heshima waandishi wa Vitabu vya Riwaya maarufu, ambao ni Mohammed Said Abdalla, Mohamed Suleiman Mohamed, Pro. Said Ahmeid Mohamed, Adam Saffi Adam na Marehemu Seif Salim.
Mapema Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume alisema Wizara kupitia BAKIZA inaendelea na mchakato wa kukusanya orodha ya wataalamu wa lugha ya kiswahili, ili kuwa na kumbu kumbu sahihi kwa lengo la kuwatambuwa na kuwatumia pale watakapohitajika.
Alisema kiswahili ni bidhaa adhimu, hivyo ni vyema kwa wanafunzi kujifunza kutoka kwa watangulizi kupitia makala mbali mbali, ili kubaini chimbuko na asili ya Kiswahili fasaha.
Aliwataka vijana na wapenzi wa lugha hiyo kutumia fursa ya kujifunza kutoka kwa magwiji na wataalamu wa lugha hiyo kupitia kazi mbali mbali walizofanya.
Nae, Mwenyekiti wa Baraza la kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dk. Mohamed Seif Khatib alisema ni wakati muafaka kwa serikali kulazimisha matumizi fasaha ya lugha ya kiswahili, kwa kutambuwa kuwa ni bidhaa yenye thamani kubwa kiuchumi na utamaduni. 
Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwaenzi na kutahmini kazi za wataalamu w alugha ya kiswahili  kwa kuwawekea makumbusho pamoja na majina yao kutumika katika mitaa mbali mbali kutokana na mchango wao mkubwa wa kukuza lugha hiyo.
Aidha, Katibu mtendaji wa BAKIZA, Mwanahijja Juma Ali alisema uchapishaji wa vitabu kupitia lugha ya kiswahili unainuwa mapato na uchumi wa nchi, hivyo akaiomba Serikali kuendelea kuwahamasisha wananchi kusoma vitabu.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.