Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Joelson Mpina akimwangalia farasi
anayetumika kwenye doria katika ranchi ya Kalambo Mkoani Rukwa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh Luhaga Joelson Mpina akiangalia nyama
inayochakatwa katika kiwanda cha SAAFI mkoani Rukwa kushoto kwake ni
mmiliki wa kiwanda hichi Dkt Chrisant Mzindakaya
![]() |
Kundi la Ng'ombe bora katika ranchi ya Kalambo mkoani Rukwa |
Na.John Mapepele - Rukwa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Luhaga Mpina ametangaza neema kwa
wafugaji kwa kugawa ekari 972, 500 za ardhi ajili ya wafugaji
wanaotangatanga kutafuta malisho ya mifugo yao ili kupata ufumbuzi wa
kudumu ambao utamaliza kabisa migogoro baina ya wafugaji na wakulima
iliyodumu kwa miaka mingi na kusababisha uvunjifu wa amani.
Akizindua zoezi la ugawaji wa ardhi hizo kwa wafugaji nchini katika
Ranchi ya Kalambo wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Waziri Mpina amesema
uamuzi huo wa Serikali umekuja kufuata wafugaji wengi nchini
kuhangaika kila mahali kutafuta malisho na kusababisha migogoro mingi
baina ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi.
“Pia wafugaji wengi walipata harasa kubwa kwa mifugo yao kutaifishwa
kutozwa faini kubwa na hata mingine mingi kufa kutokana na kukamatwa
kisha kushikiliwa kwa muda mrefu bila huduma muhimu ikiwemo maji,
malisho na matibabu kwenye hifadhi mbalimbali za taifa nchini.”
Alisisitiza Mpina
Alisema hadi sasa ekari
25,000 zenye uwezo wa kuhifadhi mifugo 6,000 katika Ranchi ya Kalambo
mkoani Rukwa wafugaji zimemegawiwa ambapo na jumla ya ng’ombe 3,000
wameshaingia kwenye ranchi hiyo wakati Serikali na wafugaji wenyewe
wakiendelea kutafuta suluhisho la kudumu la kupata malisho.
Amewataka wafugaji wote wanaohangaika kutafuta malisho kutumia fursa
hiyo iliyotangazwa na Serikali ya uwepo wa maeneo kwa ajili ya
kulishia mifugo ili wawe karibu pia huduma za tiba na chanjo pindi
mifugo yao inapopata maradhi.
Akiwa katika mkutano wa
pamoja baina ya Rachi ya Kalambo na wawekezaji Waziri Mpina
alipongeza Timu maalum aliyoiunda ya kutatua migogoro ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi kwa kufanikisha zoezi la upimaji na ugawaji
wa ardhi hiyo kwa wafugaji pamoja na kutatua migogoro yote iliyokuwepo
baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi katika mikoa ya Rukwa,
Katavi na Kigoma.
Aidha ailiiagiza Timu hiyo kuhakikisha
kwamba inazunguka nchi nzima kwenye migogoro na kuitatua ili kuboresha
mifugo iweze kuchangia katika viwanda hapa nchini.
Pia
alimwagiza Katibu Mkuu Mifugo kuhakikisha ukaratabi wa kituo cha
uchunguzi wa magonjwa ya wanyama cha Kanda ya Kusini Magharibi
kinakamilika ifikapo Februari mwakani ili kutokana na mikoa ya Katavi,
Rukwa kutokuwa na kituo hicho licha ya kuwepo mifugo mingi.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Halfan Haule alisema kutokuwepo kwa
maeneo ya malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo kumekuwepo na
migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na kumshukuru
Waziri Mpina kwa uamuzi wa kugawa vitalu kwa wafugaji.
Alisema Mkoa wa Rukwa umekuwa ukikabiliwa na magonjwa ya mifugo
ikiwemo homa ya nguruwe(ASF), Homa ya Mapafu ya Ng’ombe(CBPP), Homa
ya mapafu ya mbuzi(CCPP), Ugonjwa wa miguu na midomo(FMD), Ugonjwa wa
mapele ngozi(LSD), Ugonjwa wa kichaa cha mbwa na ugonjwa wa
mdondo(ND).
Katibu wa Umoja wa Wafugaji Ranchi ya Kalambo,
Benuel Benzeth aliishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kugawa maeneo hayo ya
Serikali kwa wafugaji katika kipindi ambacho wanaendelea kutafuta
suluhisho la kudumu la changamoto ya malisho.
Alisema
mifugo yao mingi imekufa na mingine kudhoofika kutokana na kukamatwa
na kushikiliwa kwenye hifadhi bila matunzo na wakati wote Serikali
haijawahi kuchukua hatua za kuwasaidia wafugaji na kumshukuru Waziri
Mpina kwa uamuzi huo ambao umewezesha mifugo mingi kupona na kuendelea
na uzalishaji.
Awali akizungumza mara baada ya kutembelea
Kiwanda cha Nyama cha SAAFI kilichopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa,
Waziri Mpina amesema Serikali inafanya kazi usiku na mchana
kuhakikisha kiwanda hicho kinaanza kufanya kazi haraka ili kusaidia
upatikanaji wa mifugo takribani milioni 6 iliyoko katika mikoa ya
Rukwa, Katavi, Songwe na Mbeya.
Hivyo changamoto zote
zinazokikabili kiwanda hicho zitatatuliwa haraka ikiwemo ukosefu wa
mtaji pamoja na uongozi wa kuendesha kiwanda hicho jambo
linalosababisha kiwanda hicho kusimama kwa muda mrefu licha ya kuwa na
mitambo bora na ya kisasa ya uchinjaji na usindikaji wa nyama katika
ukanda wa Afrika Mashariki.
Waziri Mpina amesema ni jambo
la fedheha kuona kiwanda hicho chenye miundombinu yote kuendelea
kubaki katika hali hiyo huku wafugaji wakiendelea kuhaha kutafuta soko
la mifugo hali inayosababisha asilimia 80 ya mifugo hiyo kutoroshwa
kwenda nchi za jirani na kwenda kuyanufaisha mataifa hayo.
Hali hiyo inaifanya Tanzania kugeuzwa kuwa malisho ya mifugo hiyo
huku rasilimali hizo zikishindwa kunufaisha nchi kimapato jambo ambalo
Serikali ya awamu ya tano haiwezi kukubali liendelee.
Waziri Mpina pia alimpongeza Mwekezaji wa kiwanda hicho, Dk.
Chrisant Mzindakaya kwa ujasiri na uamuzi mkubwa wa kubuni wazo la
kuanzisha kiwanda hicho kwa gharama ya sh bilioni 9 na kuwepo na eneo
la malisho zaidi ya hekta 6,000 kwani watu wengi wanaweza kukopa fedha
na kisha kushindwa kutekeleza mipango yao kwa mujibu wa mpango kazi
alioombea mkopo.
Hivyo aliagiza taasisi zote za Serikali
kuhakikisha changamoto zote zinakwisha ili kuhakikisha kiwanda hicho
kinaanza kazi mara moja na kwamba kama uvunaji wa rasilimali za mifugo
hauko vizuri ni kipimo cha uwajibikaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
iliyopewa dhamana ya kusimamia ukuaji wa sekta hiyo.
Kwa
upande wake Mwekezaji wa kiwanda, Dk Chrisant Mzindakaya alisema licha
ya kiwanda chake kufanya kazi lakini uzalishaji wake ni mdogo kutokana
na changamoto ya mtaji na uendeshaji wa kiwanda na kumshukuru Waziri
Mpina kwa kutembelea kiwanda na kutangaza msimamo wa Serikali katika
kukinusuru kiwanda hicho.
No comments:
Post a Comment