RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amewasisitiza viongozi wa CCM wa Majimbo kisiwani
Pemba kwenda kwa wananchi waliowapigia kura kwa lengo la kuwasilkiliza
changamoto zinazowakabili.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya ya Wete Pemba
pamoja na kufanya Majumuisho ya ziara yake kwa Wilaya hiyo, yaliyofanyika
katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo
viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama
Mwanamwema Shein.
Makamu Mwenyekiti
alitumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi wa Majimbo wakiwemo Wawakilishi wote
ambao ni wa CCM na Wabunge wa Viti Maalum wa CCM kwenda kwa wananchi wao ili
wajue changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi sambamba na kuwa nao
karibu ili kukiimarisha chama chao.
Alieleza kuwa CCM
hatomridhia kiongozi wa Jimbo ambaye amechaguliwa na wananchi lakini kwa
kipindi hichi amekuwa haonekani Jimboni kwake kwenda kuwasaidia wananchi na
kusahau wajibu wake wa kwenda kuwatumikia wananchi.
Alieleza kuwa iwapo
viongozi hao wataendelea kuwa karibu na wananchi pamoja na kwenda kuwasikiliza
changamoto zinazowakabili hali hiyo itawapelekea wananchi hao waendelee
kukiunga mkono chama chao cha CCM na kuendeleza ushindi katika uchaguzi mkuu
ujao wa 2020.
Aidha, Makamu huyo
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inayoongozwa na CCM itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwapelekea
maendeleo endelevu wananchi wote wa Unguja na Pemba tena bila ya ubaguzi.
Alieleza kuwa CCM itahakikisha
wananchi wote wanapata huduma sawa na sio kwa upandeleo kama ilivyokuwa wakati
wa ukoloni ambapo huduma za maendeleo zilikuwa zikitolewa kwa upendelea
zikiwemo huduma za elimu,afya na nyenginezo.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliwataka viongozi wa Chama na Serikali kufanya ziara za kuwatembelea wananchi
ili kujua matatizo waliyonayo na kuyatafutia ufumbuzi badala ya kukaa ofisini.
Aliongeza kuwa
kuwafuata wananchi na kutatua shida zao ni agizo la CCM, ambalo lilitolewa
katika Mkutano Mkuu wa CCM huko Dodoma ikiwa ni moja ya Utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM.
Alisisitiza kuwa
viongozi wa Chama na Serikali kwa pamoja wanapaswa kwenda kwa wananchi kwa
lengo la kuwaeleza matatizo na mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na mipango ya Serikali.
Aliwataka viongozi hao
kuwa karibu na wananchi na kwenda kuwasaidia katika masuala yao ya kijamii hasa
wale Wawakilishi na Wabunge wa Viti Maalum kisiwani humo kwani chama chao ndio
kinachoongoza Serikali.
Rais Dk. Shein
aliwakumbusha viongozi wa CCM kufanya kazi za chama na kuwataka kwa kila mmoja
kufanya kazi kwa kuzingatia wadhifa wake ikiwa ni pamoja na kufanya ziara kwa
pamoja kati ya viongozi wa Chama na Serikali na baadae kufanya tathmini.
Dk. Shein aliwataka
viongozi hao wa Chama na Serikali kuwabainisha watendaji wote waliokuwa
hawafanyi kazi ipasavyo na wamekuwa wakifanya kazi kwa maslahi yao binafsi.
Makamu Mwenyekiti huyo
wa CCM alieleza kuvutiwa na taarifa ya Chama na Serikali ya Wilaya hiyo na
kutoa pongezi zake na kusifu ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo hatua
ambayo imepelekea mafanikio makubwa.
Sambamba ya hayo,
Makamu Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa kwenye siasa za vyama vingi hakuna
kutishana na wala kutukanana na kuwataka viongozi wa CCM Wilaya hiyo ya Wete na
Mkoa wote wa Kaskazini Pemba kufanya kazi zao za kukiimarisha chama chao bila
ya hofu.
Pia, Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Mkoa huo kwa kuendelea kusimamia amani na
utulivu na kuwaeleza wananchi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kusimamia amani na utulivu kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba popote pale
walipo.
Pia, aliupongeza
uongozi wa Serikali wa Wilaya hiyo kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya
CCM kwa kukusanya vyema mapato yake.
Nao uongozi wa CCM
Wilaya na Mkoa wa Kaskazini Pemba ulitoapongezi zake kwa Rais Dk. Shein kwa
jinsi anavyotekeleza Ilani ya Uchaguzi na kusisitiza kuwa CCM katika Wilayaya
Wete iko imara.
Rajab
Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment