Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, Ameitaka Wizara ya Afya Zanzibar Kuwasimamia Watendaji Wao

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar, kulia Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Harusi Sais Suleiman na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Ali Abdullah, wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais  wa Zanzibar, walipofika Ofisini kwake Vuga Zanzibar.
(Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameendelea kuuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar kuwasimamia watendaji wao kufanyakazi katika Hospitali na Vituo vya Afya vilivyopo Kisiwani Pemba.
Alisema wakati umefika kwa Viongozi wa Wizara hiyo kuacha tabia ya kuwabeba Wafanyakazi wanaotaka uhamisho wakati uajiri wao wa kazi kwa mujibu wa Mikataba yao na Sheria za Utumishi wa Umma uko Kisiwani pemba.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar ulioongozwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Harus Said Suleiman ulipofika kumpa Taarifa ya masuala mbali mbali yaliyochukuliwa hatua katika vitengo vya Wizara hiyo.
Alisema haipendezi kuona baadhi ya Watendaji wamesomeshwa na Serikali kwa gharama kubwa kwa lengo la kuwahudumia Wananchi lakini badala yake huamua kuchagua maeneo ya Kufanya kazi jambo ambalo Serikali Kuu haitakuwa tayari kuona linaendelezwa.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi wa Wizara ya Afya pamoja na Wafanyakazi wake kwa jitihada kubwa unazochukuwa za kukabiliana na changamoto zinazowakabili ambazo wakati mwengine huleta usumbufu kwa Jamii.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali Abdulla alisema Uongozi wa Wizara hiyo umeanza kujiwekeza utaratibu wa kujenga Utamaduni wa kutoa Taarifa ya mambo mbali mbali yanayotekelezwa na Wizara hiyo ili jamii ielewe kinachofanyika kwa kila hatua.
Bibi Asha alisema mfumo uliopo hivi sasa wa kusubiri kuripoti matatizo yanapotokezea hautoi nafasi nzuri kwa Serikali kujipanga vyema katika kukabiliana na changamoto kubwa zinazojichomoza kwenye Taasisi zake.
Alisema yapo masuala yaliyoanza kuchukuliwa  hatua na Uongozi wa Wizara katika azma ya kuondoa kero na hitilafu zinazoleta usumbufu kwa Uongozi wenyewe, Wafanyakazi sambamba na Wananchi wanaohitaji huduma kupitia Taasisi hiyo ya Kiafya.
Bibi Asha alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba matumaini ya ujenzi wa Nyumba za Wafanyakazi wa Hospitali ya Abdullah Mzee Mkoani yameanza kutoa matumaini kutokana na China kuonyesha nia ya kutaka kufadhili Mradi huo.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya alisema ipo miradi mengine ambayo kwa wakati huu iko katika hatua za utekelezaji akatolea mfano matengenezo ya Lifti ya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja yaliyokuwa katika hatua za mwisho yakienda sambamba na ununuzi wa Lifti nyengine Mpya ya Hospitali hiyo.
Alisema harakati za maandalizi ya Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa hapo Binguni zimeanza baada ya kukamilika kwa uchambuzi yakinifu wa eneo lote la mipaka, ujenzi wa Ghala ya kuhifadhia Dawa huko Vitongozji Kisiwani Pemba, Ujenzi wa jengo jipya la Hospitali ya Wagonjwa wa akili pamoja na kukamilika kwa Kitengo cha uchunguzi wa Vinasaba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.