Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Azindua Udhibiti wa Uhalifu wa Vyombo Vya Moto Pikipiki na BajajiBalozi Seif  akizindua rasmi Mfumo wa Kieletroni  wa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya Moto {Usafiri} hususan Piki Piki na Bajaji.
Balozi Seif akikaribishwa kuingia katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam kuzindua Mfumo wa Kieletroni wa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya Moto { Usafiri} hususan Piki Piki na Bajaji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano Kampuni ya Ulinzi ya TAMOBA CITY FORCE juu ya Mfumo wa Kieletroni wa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya Moto { Usafiri} hususan Piki Piki na Bajaji hapo Makao Makuu ya
Kampuni hiyo Kurasini Jijini Dar es salaam.


Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati Ulimwengu umefika mbali katika mifumo ya Kiteknolojia ya Kisasa ya Ulinzi na Usalama, Tanzania haipaswi kuwa Kisiwa kilichojitenga katika Bahari ya Teknolojia hiyo.

Alisema Dunia hivi sasa imo katika zama ambazo uhalifu limekuwa tatizo kubwa linalorejesha nyuma Maendeleo ya Mwanaadamu. Hivyo Tanzania inalazimika kukimbia ili iwe mahiri katika matumizi ya Teknolojia hiyo yenye nguvu kuliko hata mapambano ya silaha za moto.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati  wa Hafla Maalum ya Uzinduzi wa Mfumo wa Majaribio wa Kielekroniki wa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya Moto { Usafiri} hususan Piki Piki na Bajaji hafla iliyofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini  Dar es salaam.

Alisema Teknolojia inayotumika  ya Ulinzi na Usalama  imechangia kutawaliwa na huduma duni hasa katika Sekta ya usafiri inayoibua kasoro tofauti akitolea mfano ajali mbaya za Bara barani, kuongezeka kwa uhalifu katika Miji tofauti pamoja na uvunjaji wa sheria za
Barabarani.

Balozi Seif alisema mapungufu hayo yote yanayojitokeza ni kinyume na Sera ya Taifa ya Usafirishaji ya Mwaka 2003 iliyolenga kuongeza Usalama, huduma ya kuaminika, ufanisi na kukidhi mahitaji ya usafiri na usafirishaji kwa gharama nafuu.

Alisema katika kukabiliana na changamoto hizo za ajali na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu Serikali zote mbili Nchini Tanzania zinaunga mkono jitihada zilizochukuliwa na Muungano wa Makampuni ya Kizalendo Nchini yaliyofikia hatua ya  kubuni Mfumo huo wa Kielekroniki wa kuzuia na kudhibiti uhalifu unaotokana na vyombo vya Moto.

“ Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa kazi yote hii ya Kielekroniki imefanywa na Wataalamu wetu wa Kitanzania kwa kiasi kikubwa. Huu ni Uzalendo wa kupigiwa mfano katika Taifa letu hili. Tunawashukuru sana wote waliohusika kwa ubunifu wao huu”. Alisisitiza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Serikali hizo ziko tayari kuanzia sasa kuyapatia Makampuni hayo ushirikiano wowote utakaohitajika katika kuhakikisha Mfumo huo unafanya kazi Nchini Tanzania na kuleta matokeo bora yanayotarajiwa kama Malengo ya Taifa yalivyo.

Alieleza kwamba Mfumo wa Kielekroniki wa kuzuia na kudhibiti Uhalifu unaotokana na vyombo vya Mtoto unakusudiwa kuepusha ajali nyingi kwa kufuatilia mienendo ya vyombo vya Usafiri ikiwa ni habari njema za kutia moyo zilizokuja kwa wakati muwafaka.

Balozi Seif alisema Watanzania hawatokuwa na hofu tena ya kutendewa vitendo vya uhalifu vinavyoendeshwa na wahalifu wachache katika baadhi ya maeneo yaliyoruhusiwa usafiri wa Boda Boda au Bajaji vyombo ambavyo siku hizi baadhi ya Wananchi huvitumia kwa usafiri.

Alieleza kwamba Sekta ya usafirishaji inaendelea kufanya vyema katika  kuchangia Ustawi wa shughuli za Kiuchumi na Kijamii katika Taifa la Tanzania hasa ndani ya Mkoa wa Dar es salaam na Miji mengine Mikubwa Nchini.

Balozi Seif  alieleza kwamba inapendeza kuona Sekta hii hivi sasa inatoa huduma katika maeneo ambayo ni shida kufikiwa na Usafiri wa Umma jambo ambalo Vijana wengi wameweza kujiajiri kupitia Sekta hiyo na kuwa Mkombozi wa Maendeleo yao Kimaisha.

Alisema Wananchi wengi kwa sasa wanaendelea kufaidika na Sekta hiyo kwa kuwahi kufika mapema katika harakati zao za Kiuchumi za kila Siku hasa kwa wale Watumishi wa Umma wanaohitajika kufika mapema katika maeneo yao ya kazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi wa Makapuni hayo kwamba Serikali itakaa pamoja na Wataalamu wao katika kutathmini na kuangalia jinsi Mfumo huo unavyoweza kuleta mafanikio katika kipindi hichi cha mpito cha majaribio na baadae kutoa mapendekezo yake.

Alisema nia ya Serikali ni kuona mfumo wa kufuatilia, kuzuia na kudhibiti uhalifu na mienendo ya vyombo vya usafiri hususan Piki Piki na Bajaji unaweza kutumika sehemu zote kwa kufuata Sheria za Nchi kwa kuutekeleza katika Wilaya zote  hapa Nchini.

Balozi Seif alitoa rai kwa Mikoa mengine Nchini kuongeza kasi ya kuyakaribisha  Makampuni Binafsi katika kubuni, Kuibua na kutekeleza kwa pamoja Miradi inayoleta tija ya haraka kwa Maendeleo ya Wananchi walio wengi Nchini.

Alikumbusha kwamba Sekta zinazohitaji kuongezewa ufanisi wa Kiteknolojia chini ya Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Mwaka 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020 na Mpango wa Mapinduzi ya Viwanda  zipo nyingi ikiwemo Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi inayoajiri Wananchi wengi hasa wale waliopo Vijijini.

Akisoma Risala ya Madereva wa Boda Boda Jijini Dar es salaam Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Boda Boda Ndugu Msham Nassor alisema Wana Boda Boda wako tayari kufuata Sheria bila ya shuruti iwapo masuala yanayowahusu katika kuendesha kazi hiyo yatazingatiwa vyema.

Nd. Msham alisema ni jamo la msingi iwapo Serikali kupitia Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania {TRA} itajenga mazingira bora ya ulipaji kodi kwa Madereva wa Boda Boda katika masuala ya Leseni, Bima na mambo mengine huku ikizingatiwa kwamba huduma wanayotoa tayari inakubalika kwa Jamii katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Chama cha Waendesha Boda Boda Jijini Dar es salaam alisema kwamba kwa niaba ya wadau wake wameiomba Serikali Kuu kuzingatia utaratibu wa kuwapatia Vibali Maalum kama walivyofanyiwa Wafanyabiashara wadogo wadogo Nchini Maarufu Wamachinga.

Wamemshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Paul Makonda  kwa jitihada zake  anazoendelea kuzichukuwa  katika kuona Vijana wa Boda boda wanaendesha harakati zao za Kimaisha kwa kutumia biashara hiyo ya Boda Boda.

Akitoa Taarifa ya kuanzishwa kwa Mfumo huo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ulinzi Tanzania { TAMOBA CITY FORCE } Nd. Joseph Kimisa alisema wazo hilo limekuja kufuatia Mfumo  wa Dunia uliopo hivi sasa wa kutumia Boda boda na Bajaji kama Usafiri wa kawaida.

Nd. Joseph alisema Mfumo huo wa majaribio endapo utafanikiwa kutumika baada ya kipindi hichi cha mpito utamuwezesha muendesha Boda boda au Bajaj kufungiwa kifaa Maalum {GPS} kitakachokuwa na uwezo wa kutoa mawasiliano yatayowezesha kueleweka endapo yatakuwepo matukio yasiyo ya kawaida.

Alisema zipo faida mbali mbali zitakazopatikana katika matumizi ya Mfumo huo wa Kielekroniki akizitaja kuwa ni pamoja na kupunguza nguvu kubwa ya Jeshi la Polisi kufuatilia makosa mbali mbali ya waendesha Boda boda na Bajaji kwa kuwakamata wahalifu kirahisi kabisa.
 
Mkurungenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Ulinzi ya TAMOBA alifahamisha kwamba lipo wazo la kuwajengea uwezo zaidi wa waendesha Boda Boda na Bajaji la kuwafungulia Saccos itakayohusika na kwasaidia wadau hao katika njia mbali mbali za kuwatanzaua kiuchumi.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitembela Kituo Maalum cha mawasiliano kitakachotumika kuendesha Mfumo huo wa Kielekroniki kiliopo maeneo ya Kurasini Jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.