Habari za Punde

Zanzibar Kuendelea na Kuendesha Zoezi la Upigaji wa Dawa za Malaria Majumbani.

Na.Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar              22.02.2019
Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha kumaliza Malaria Zanzibar inatarajia hapo kesho February 23, kuanza zoezi la upigaji wa Dawa majumbani ili kutokomeza Malaria Zanzibar.
Akizindua zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Kati Mashavu Said Sukwa amewataka Wananchi   kuonesha ushirikiano wakati wa zoezi hilo ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huo.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Wananchi wa shehia ya Miwani, Wilaya ya Kati waliokusanyika katika uwanja wa mpira wakati wa uzinduzi huo kuhakikisha wanawafikishia Taarifa wengine ambao hawakuwepo ili kurahisisha Wapiga dawa kufanya kazi yao kwa ufanisi.
Amesema Serikali inafanya juhudi kubwa na gharama nyingi ili kuona Wananchi wake wanaishi kwa usalama wa afya zao hivyo Wananchi hao wanapaswa kuinga Mkono Serikali yao.
 “Serikali inatumia gharama kubwa katika kuliondosha tatizo hili hivyo Wananchi toeni ushirikiano kwa wapiga dawa ili muweze kuondosha kabisa ugonjwa huu ambao ni hatari sana”alisema Sukwa.
Amefahamisha kuwa Malaria ni ugonjwa hatari sana unaopelekea athari kubwa katika jamii ikiwemo na kuweza kusababisha ulemavu wa Viuongo pale unapopanda kichwani.
Aliwapongeza Wananachi wa Wilaya yake kwa kazi nzuri za kujitolea na mashirikiano wanayoyatoa katika shughuli za kitaifa na kijamii hivyo anaamini zoezi hilo litaenda vizuri  
Akielezea kuhusu Gografia ya Wilaya ya Kati Mkuu huyo amesema Wilaya hiyo ina jumla ya Shehia 31 na Nyumba 513 ambazo zinatarajiwa kupigwa dawa.
Akitoa nasaha kwa Wapigadawa Mashavu aliwaomba kuwa waangalifu katika Nyumba walizopangiwa  ili kuhakikisha zoezi hilo halileti madhara yeyote.
“Nakuombeni Wapiga dawa ndani ya nyumba mlizopangiwa hakikisheni mnapiga dawa kwa uangalifu mkubwa bila ya kuleta madhara yeyote”alisema Mkuu wa Wilaya.
Nae Afisa mipango wa Wilaya ya Kati Ali Omar Hamad alisema kila mwaka zoezi hili hufanyika kwa mafanikio makubwa mbali ya changamoto ndogo ndogo ambazo hujitokeza na kupatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake Kaimu Sheha wa Shehia ya Miwani Haji Shaabani Waziri ameahidi kusimamia vizuri zoezi hilo na kuhakikisha linafanyika kwa ufanisi mkubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.