Habari za Punde

JULUKIZA yatakiwa kukikuza Kiswahili

Na Mwashungi Tahir          Maelezo   
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud amesema Kiswahili kinachozungumzwa Zanzibar ndio Kiswahili fasaha zaidi kuliko cha mataifa mengine hivyo ameitaka Jumuiya ya Uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili Zanzibar (JULUKIZA) kuendelea kukikuza.
Hayo ameyasema katika Ukumbi wa Wasanii Rahaleo wakati alipokuwa akizungumza na wana jumuiya hiyo  ambayo imetimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa na kuzindua kitabu kipya kilichopewa jana la ‘Mjue Chimbeni bin  Kheir’ kilichotungwa na Bibi Mwanakombo Mwadini Sheha, ambae ni mwanachama wa Jumuiya hiyo.
Alisema lafdhi ya Lugha ya Kiswahili cha Zanzibar ni nzuri zaidi tangu zamani na ndio sababu vituo vingi vya Redio za nje zinazoanzisha matangazo ya lugha ya Kiswahili watangazaji walikuwa wakitoka Zanzibar na wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwenye vituo hivyo.
Ayoub alisema katika Barani la Afrika Lugha ya Kiswahili inashikilia nafasi ya kwanza kuzungumzwa na kinashika nafasi ya sita kuzungumzwa duniani kote na hii yote inatokana na umuhimu wake. 
Amewataka Wanajumuiya kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar  na sekta binafsi katika kuikuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili na kuwapa busara ya kukienzi Kiswahili kwani ni urithi wetu.
Hata hivyo amewataka  Wasani wa sasa kuwa na mashirikiano katika kufanya kazi zao na  kuungana na wasanii wa zamani kwani nao ni muhimu katika kukikuza na kukilinda Kiswahili.
Nae mjumbe wa JULUKIZA Dhalha Mohamed Muhsin akisoma risala  amesema  utamaduni wa mswahili unatokana na lugha ya Kiswahili hivyo amezitaka asasi za kiraia kutoa mchango wao kuhakikisha Kiswahili kinalindwa na kukuzwa ili kiwe moja ya chanzo cha ajira kwa wazanzibari.
Aidha  amesema Jumuiya ya uendelezaji lugha ya kiswahili Zanzibar itahakikisha inachukua juhudi mbalimbali katika kuona  lugha ya kiswahili inakuwa na kuenea zaidi  ndani na nje ya nchi ili  kuhakikisha utamaduni wa Mzanzibari usipotee. 
Dhalha amesema harakati za kukikuza kiswahili zinaendelea katika jumuiya hiyo ikiweno kuandaa majarida, makongamano na mafunzo ya lugha katika mataifa mbalimbali ili kusaidia jamii kuona umuhimu wa Kiswahili.
Akitoa changamoto zinazowakabili katika jumuiya hiyo ni pamoja na ukosefu  wa vitendea kazi kama  projeta , ajira kwa vijana waliosoma katika jumuiya hiyo na tayari wamepata shahada ya Kiswahili  na Mkuu wa Mkoa ameahidi kuwasaidia projeta .
Kwa upande wake Mshauri wa Rais katika masuala ya Utamaduni Chimbeni Kheri aliwashukuru wanajumuiya hiyo na kusema kazi ya Sanaa ameanza muda mrefu  na amewaomba wasanii wachanga kuendeleza fani hiyo ili iweze kuibua vipaji vyao.
Aliikumbusha hadhiri iliyiohudhuria uzinduzi wa kitabu na maadhimisho hayo  michezo aliyoigiza na kumpatia sifa kubwa kuwa ni pamoja na Talaka mpe jirani, Nia safi hairogwi  na nyimbo ni Kibali inayoghaniwa na Bi. Mwanacha Hassan na You are all well come to Zanzibar the Spice Island aliyoimba yeye mwenyewe.
Mwisho

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.